Kipengele cha Taswira katika Ushairi
SURA YA PILI
Viko vipengele vingi vya fani katika ushairi. Kati ya hivyo, vifuatavyo vimeshughulikiwa hapa na pale katika tahakiki mbalimbali humu kitabuni:
1. Tamathali za semi
2. Misemo na nahau
3. Mcthali
4. Matumizi ya fumbo au tambo
5. Vina na mizani
6. Umbo na muundo
7. Mitindo
8. Taswira
9. Ishara
10. Kejeli na dhihaka.
Mara kwa mara vipengele hivi vinaingiliana sana. Kwa mfano, tuongeapo kuhusu taswira ya safari ilivyotumiwa na Kahigi na Mulokozi kweoye mashairi yao katika Malenga wa Bara, hapohapo tunaonyesba jinsi taswira bu ilivyo ishara ya uhuru, na jinsi hii imefichwa katika matumizi ya tambo au fumbo.
Katika sura zifuatiazo hii, mifano mingi ya vipengele tulivyooro-dbesha hapo juu imejadiliwa; kwa hivyo hakuna haja ya kutoa maelezo na mifano mingme hapa. Hata hivyo, kwa vile kati ya vipengele hivyo cha taswira ni muhimu sana, na aghalabu katika kukijadili hapohapo huingiza na vingine, tutakichambua kwa kirefu kidogo katika sura hii.
Tulipotoa maana ya ushairi katika sura ya kwanza tuliongelea lugha ya mkato ambayo imepangwa kwa njia iletayo mizani au mapigo yanayolandana na maudhui aliyokusudia kutoa mshairi. Lugha hii ili iwe ya kishairi mara nyingi huwa ya kitaswira, nayo ni mbinu kuu itumiwayo na washairi kuufanya ushairi wao uwe hai zaidi. Washairi huitumia ili kuzinasa hisia za hadhira kwa kuwapangia maneno yanayoweza kuumba picha kamili katia akili zao.
Swali muhimu kujiuliza kabla y kuangalia matumizi ya taswira ni: Je, istilahi hu ioa maana gani? Kwa kifupi taswira ni maneno ambayo yalivyopangwa katika shairi huweza kuchora picha kamili ya kitu, hali, wazo, dhana au uzoefu fulani wa jamii au sehemu ya jamii katika mawazo ya wanaopokea shairi linalohusika.
Matumizi ya taswira mara nyingi huambatana na yale ya ishara ambazo nazo aghalabu hufichwa ndani ya tamathali za semi. Ishara ni dhana au mawazo mbalimbali anayotumia msanii katika kazi yake ya fasihi kuwakilisha vitu, dhana au mawazo mengine. Mathalani, katika shairi la Abdilatif Abdalla la "Mnazi: Vuta N'kuvute" (Sauti ya Dhiki), mshairi katika kuzisawiri hali za uchumi na kisiasa zilivyo Afrika ametumia taswira ya mnazi na walanazi, ambayo ni ishara ya invutano uliopo baina ya akina ALII na BADI; na katika shairi la M.M. Mulokozi na K.K. Kahigi la "Barua Kwa... (Malenga wa Bara uk. 39), nguvu za mapenzi zimedhihirishwa kwa matumizi ya taswira za aina mbalimbali za vifaa vya kukatia na kuumiza:
Majisu hukata
Mafito na mbata
Sime hudengua
Gumu kupitia,
Mapanga hufyeka
Miti na vichaka,
Misumeno pia
Miti nusu huwa;
Mashingo miguu,
Hukatwa munduu,
Wengi wamewaza
Hivi vyaumiza!
Mpaka hapa, washairi, kwa kutumia mbinu ya taharuki, wametuacha tukining'inia kwa kusubiri jambo wanaiotaka kutueleza. Je, si ni kweli kuwa majisu, sime, mapanga, misumeno na miundu hukata na kufyeka vitu kama tulivyoorodheshewa? Lipi jipy, basi? Jibu tunalipata katika sehemu inayofuatia:
Sikia nakana,
Sikia nakana!
Visu, sime vyote,
Havitii kite
Na havijakata
Kuumiza hata
Kama hilijibu
Lako e muhibu
Lilokata moyo
Kwa mwingi mgwayo,
Moyo nimekatwa,
Vipande, vipande,
Moyo unasongwa
Lolote nitende!
Wanalotutaka washairi tufanye hapa ni kuzichukua taswira za kukata zilizoko katika beti mbili za mwanzo, tuziweke sambamba na ya ubeti huo hapo juu ambayo ni ya kukata pia. Hapo tutaona ukali na uchungu wa kukataliwa katika mapenzi.
Shairi lingine ambalo ni zuri kulinganishwa na hili la "Barua Kwa..." ni lile la "Wimbo wa Moyo" (Kunga za Ushairi na Diwani Yetu, uk. 85). Katika shairi hili, taswira tuipatayo si ile ya kukata maini kwa uchungu bali ile iliyotuiia, ambayo inashirikisha fahamu zote tano za mtu: kuonja, kuhisi, kunusa, kuona na kusikia:
Njoo hapa tuketi pamoja
katika uwanja wa ujana mpevu;
Njoo hapa tuimbe pamoja
katika uwanja wa majani
mabichichini ya mwembe huu
wenye matunda mabivu
.........................................
Njoo hepa, ukae nami:
Chini ya mwembe huu
Uliojaa matunda mabivu,
tutamenya embe tamu
nikulishe,nawe unilishe
tufurahie mwonjo mtamu
utakaotuliza hamu yetu...
Taswira tuipatayo hapa, ya mwembe wenye matunda mabivu ni ishara ya ujana uliokwishafikia kilele; na inaashiria wapenzi wawili walio tayari kukutana na kushirikiana katika mapenzi.
Matumizi mazuri ya taswira na ishara hutegemea ufundi wa mshairi wa kuchota mambo mbalimbali kutoka katika mazingira yaliyomzunguka yeye na jamii yake, na pia kutoka katika historia na sehemu zingine za maisha azijuazo. Lakini kuchota tu hakutoshi. Linaloifanya taswira iwe nzuri ni ule ufundi wa mshairi wa kuiunda taswira hiyo kwa namna ya kuivutia hadhira, huku ikiyatumikia vizuri maudhui yaliyolengwa kutolewa katika shairi. Matumizi ya taswira ni sawa na yale ya vina na mizani. Vina na urari wa mizani haviwezi kujitegemea vyenyewe bila kuyatumikia vizuri maudhui ya shairi.
Labda tumchukue Mathias Mnyampala katika Diwani ya Mathias Mnyampala kuwa kielelezo cha matumizi ya taswira na ishara. Katika diwani hii tunaweza kusema kuwa taswira azitumiazo mshairi huyu ziko katika mafungu makuu matatu:
(i) Taswira zionekanazo
(ii) Taswira za mawazo
(iii) Taswira za hisi
(i) Taswira Zionekanazo
Shairi la "Daima Pima Upepo" (uk. 27) ni shairi linalohusu mawaidha ya namna ya kuishi vizuri. Linamtahadharisha msomaji kuwa lazima ayachunguze mazingira yake na watu anaoishi nao awafahamu yizuri ili aweze kuishi nao vyema. Pia tunaweza kusema kuwa shairi hili linamuasa mtu awe na uangalifu na uhakika kamili kabla ya kufanya jambo lolote.
Ubeti wa pili wa shairi hili ni kielelczo kizuri cha matumizi ya taswira zionekanazo:
Piga ngoma za makopo, waite wasokuwapo,
Na nyumba ziunguapo, nao panya wahamapo,
Vyombo viteketeapo, ndipo shida yangukapo,
Chungua sana upepo, ni wapi welekeapo.
Hapa ni dhahiri kuwa akilini mwa msomaji taswira kadhaa zinachoreka, kuanzia ile ya mpiga ngoma - tena ngoma yenyewe ya makopo - halafu watu wanavyokusanyika, huku nyumba zikiungua na panya wakiutoroka moto. Wakati huo huo vyombo vya humo ndani ya nyumba vinateketea na shida nazo zinaanza. Kwa ubeti huu mmoja tu Mnyam.pala katuchorea picha nzito ambayo inaonekana kwa urahisi sana mawazoni mwetu. Mshairi amefaulu kuleta matukio mbalimbali katika ubeti huu ambayo yameumba taswira zinazooana na kueleza maudhui ya shairi lake.
Shairi lingine ambalo pia limetumia taswira ionekanayo ni lile la "Chawa Hatoki Nguoni" (uk. 44). Katika shaiti hili tunaipata taswira ya chawa aliyeng'ang'ania nguoni na ambaye anamnyonya na kumghasi mwanadamu:
Mwili huwa mnato, akuumapo kwapani,
Usingizi hata ndoto, hupotea kitandani,
Kwa wazee watoto, chawa adui jamani,
Chawa hatoki nguoni, shuti kwa chomo la moto.
Ili kukamilisha taswira yake, mshairi katupa mifano ya wadudu wengine sawa na chawa:
Chawa ni mwana zoloto, mfanowe kungum,
Kama mende wa mfuto, wajifichapo chooni,
Wanaokula mseto, na wali wenye maini,
Chawa hatoki nguoni, shuti kwa chomo la moto.
Katika taswira hizi za majificho na bughudha za wadudu mbalimbali, mshairi pia ametumia taswira za hisi kwani tusomapo kuhusu tabia za mende hapo hapo tunasikia kinyaa na hata kutaka kutapika.
Katika shairi la "Bahari Kuwaka Moto," (uk. 110) Mnyampala ametumia pia taswira za kuonekana. Mshairi ametumia mbinu ya ndoto ambayo yenyewe ni fumbo, kutupatia mfululizo wa taswira zinazoeleza hiyo bahari iwakayo moto. Labda tulifasili shairi hili tangu mwanzo hadi mwisho wakati tukijaribu kutafuta maana za taswira azitoazo mshairi.
Shairi linaanza na ndoto ambayo inamrusha mshairi juu angani ambako anaweza kuiona "Ramani" yenye kumkidhi "tilabani" na kumlisha "mchanyato."
Bado ni vigumu kupata maana ya taswira hii ya ramani ya bahari iwakayo moto hadi mshairi anapotugsia juu ya "hurulaini": hapo tunaanza kupata kidokezo juu ya maudhui - kuwa yanahusu schemu za siri za mwanamke, na namna ambavyo zimetumiwa vibaya na baadhi ya wanawake katika mambo ya umalaya:
Vilijiepusha motoni, kukoa hapo mkito,
Vilikimbia majini, sambamba vyenda mseto,
Kuepuka nukusani, japo vyapata masuto,
Bahari kuwaka moto, ajabu ya Buruhani.
Kwa matumizi haya ya taswira ambazo zinaonekana dhahiri mawazoni mwetu, tunapata picha na maana ya "Ramani ya kwato" ambayo ni ya "Bahari" iliyo asili ya mioto (vurugu) mingi duniani.
Kati ya taswira zionekanazo anazotumia Mathias Mnyampala liko kundi la zile za harakaharaka ambazo mshairi kaziunda ndani ya tamathali za usemi. Taswira hizi znajitokeza katika lugha inayohusianisha vitu, mambo, mawazo, au hata watu mbalimbali. Kwa mfano, ubeti wa pili wa shairi la "Kifo cha Bwana Robert" (uk. 151) unasems:
Ni hasara kwa nchi nzima, ninayosema kwa dhati,
Ni kama taa kuzima, usiku wa katikati,
Kiswahili tainama, kwa kukosa kalafati,
Kifo cha Bwana Robert, hasara kwa Kiswahili.
Kufariki kwa Shaaban Robert kunafananishwa na kuzimika kwa taa iliyokuwa ikitoa mwangaza katikati ya usiku. Taswira hii inatuonyesha nafasi ya kwanza aliyokuwa kashika Shaaban Robert katika ulimwengu wa lugha na fasihi ya Kiswahili. Kwa kuwapo kwake Kiswahili kilikuwa kimenyooka na kusimama wima. Kifo cbake kitakifanya Kiswahili kiiname kama vile jani la nunea uliokosa maji ya kutosha.
Mbinu hii ya kutumia taswira kwa kuziunda ndani ya tamathali za usemi imetumiwa sana na washairi wengi maarufu, kwa mfano, Shaaban Robert. Ni njia inayowezesha picha igande vizuri akilini mwa mpokeaji wa shairi. Baadhi ya wataalamu wa fasihi wameitaja njia hii ya matumizi ya tamathali za usemi kuwa ya maana na umuhimu mkubwa katika ujengaji wa taswira; na hata baadhi yao wamesema kuwa maana ya taswira ni matumizi ya tamathali za usemi.
Mfano wa shairi lingine la Mnyampala ambalo limetumia tamathali za usemi katika uundaji wa taswira ni lile la "Nionjeshe Lako Titi" (uk. 49), hasa ubeti wa tano:
Nimekuwa kama panzi, kuyaguguna makuti
Nimekuwa kama nzi, kidondani kutafiti,
Kimenipata kisunzi, naitafuta bahati
Taswira za panzi anayeguguna makuti, na nzi anayehangaika kujitafutia chochote katika kidonda, zinasadifu sana kueleza hali ya kutotulia, na hali ya kuhaogaika aliyo nayo mshairi.
(ii) Taswira za Mawazo
Mnyampala amezoea katika ushairi wake kutumia taswira ambazo hasahasa ni za kuwazika tu. Mara nyingi taswira hizi huwa katika mashairi ya tambo, nazo husaidia kulifanya fumbo la shairi liwe zito.
Shairi la "Nchi Gani Ilotoweka" (uk. 55) ni mfano mzuri wa matumizi ya taswira za mawazo. Linamfanya msomaji awaze juu ya hiyo nchi iliyotoweka baada ya dunia kuwapo. Taswira hu inatoa upana wa tafsiri mbalimbali za hili tambo kufuatana na imani ya kila msomaji na mazingira yake.
Mathalani, kwa waumini wa dini nchi hiyo ilotoweka inaweza kuwa bustani ya Edeni inayoongelewa katika misahafu; Edeni ambayo ilijaa amani na furaha:
Ilikuwa ya amani, tena nchiyenye baraka,
Ilikuwa ya hesani, wema walinufaika,
Hata sasa watamani, nchiyao ikivumbuka
Nchi gani ilitoweka, baada dunia kuwa?
Ni wazi kuwa "nchi" hiyo anayoiongelea mshairi hapa ni "nchi" ya kuwazika tu. Si ajabu mshairi anaongea juu ya "furaha" na jinsi ambavyo haipo tcna duniani na badala yake zimebaki vurugu na karaha tupu. Huu basi ni mfano mzuri wa taswira ya kuwazika tu.
Shairi la "Bahari Kuwaka Moto" tuliloliangalia ni mfano mzuri pia wa matumizi ya taswira za mawazo kwani hushughulisha bongo za wasomaji kwa kuwachorea picha za kuwazika tu; mambo ya kinadharia ambayo wakati huohuo huleta tafsiri mbalimbali za maudhui.
(iii) Taswira za Hisi
Taswira za hisi zina nguvu kubwa ya kuganda akilini na kunasisha ujumbe kwa wasikilizaji au wasomaji wa shairi lake. Ijapokuwa taswira hizi huingiliana na zile zinazoonekana, hasa hasa hizi hushughulikia hisi za ndani. Hizi huweza kufanya msomaji au msikilizaji awe na wasiwasi, aoue woga, apandwe na hasira, asikie kinyaa, na kadhalika.
Nitachukua mifano michache ya mashairi ya Mathias Mnyampala ambayo yametumia taswira za hisi. Shairi la "Wakati Titi la Nyati" (uk. 78) linafananisha hali ya wasiwasi na ile ya hofn ya mtu anayejaribu kukamua titi la nyati. Anasema, " Wakati titl la nyati, hukamuliwa kwa shaka."
Tunajua ukali wa nyati ulivyo. Nasi tunapojaribu kupiga picha ya mtu anayejaribu kukamua titi la nyati tunaweza kuona dhahiri wasiwasi na mashaka aliyo nayo mtu huyo. Sitiari hii ya kufananisha wakati na ukamuaji wa titi la nyati inaongeza uzito wa maudhui ya shairi hiii kuhusu maisha. Mshairi anaonyesha kuwa maisha ya mtu ni ya wasiwasi na kutotulia. Hapa imeundwa taswira inuiayo kuonyesha umuhimu wa uvumilivu kutokana na mabadiliko mengi yanayoambatana na wakati.
Katika shairi la "Ua Hili Ua Gani?" (uk. 85), hisi za kunusa zinahusishwa wakati mshairi anapotoa tambo kuhusu ua. Beti za 3 na 4 zinasaidia katika kujenga taswira hiyo ya hisi:
3. Sio ua la mdimu, ninalijua zamani,
Si la maji zamuzamu, lililopandwa bondeni,
Ama lanitia hamu, kuchuma ni mashakani,
Ua hili ua gani, ihwani niambieni.4. Si ua la mchongoma, ama la mdalasini,
.....................................................................
Kutokana na ufundi wa mshairi wa kutoa mifano mingi ya maua ya aina mbalimbali, taswira ya ua katika shairi hili imefaulu sana kugusa hisi za kunusa za msomaji.
Mifano mingine ya mashairi yenye taswira zinazoshughulikia hisi ni "Nionjeshe Lako Titi" (uk. 49), "Je Asali ai Halali?" (uk. 51), na kadhalika.
Tumeyaangalia matumizi ya taswira katika kitabu cha Diwani ya Mnyampala kwa kifupi tu. Huu ni mfano mmoja tu wa jinsi ya kuchambua matumizi ya taswira katika ushairi. Mgawanyo tulioufanya hapo juu si lazima uwe huobuo kwa washairi au mashairi yote, au sio huo tu ambao uko katika matumizi ya taswira. Kugawanya huku kutategemea shairi, mshairi, na pia msomaji au msikilizaji anavyoliona, kwani vionjo hutofautiana. E. Kezilahabi, kwa mfano, kagawanya matumizi ya taswira katika ushairi wa Shaaban Robert katika mafungu matatu:
(i) Picha za Maumbile: (hali ya hewa angani, hali ya nchi... juu ya ardhi, chini ya ardhi).
(ii) Picha za viumbe: (watu, wanyama, wadudu, na kadhalika).
(iii) Picha za viumbe visivyo mwili: (majini, mashetani na kadhalika).
Kezilahabi kazichunguza taswira hizo na kuzihusisha na maudhui ya mashairi ya Shaaban Robert.
Hatuna budi kusema kuwa, kwa mshairi mzuri, taswira daima huonekana waziwazi; nayo hutumiwa kiukamilifu katika kujenga utajiri na uzito wa maudhui ya shairi lake. Matumizi mazuri ya taswira huweza kumfanya msikilizaji au msomaji wa shain aupate vizuri ujumbe wa shairi. Humfanya mpokeaji wa shairi ayaelewe maudhui ya shairi kikamilifu na kwa njia fupi.
Baadhi ya washairi hufikin kuwa uzito wa shairi upo katika fani ngumu; kwa hiyo hunuia daima kutumia taswira ngumungumu zinazoficha ujumbe wa mashairi yao. Lakini hapa inabidi ifahamike wazi kuwa madhumuni ya taswira si kulifanya shairi liwe gumu au liwe pambo tu. Madhumuni ya taswira yanatakiwa yawe yale ya kurahisisha njia ya kumfanya msikilizaji au msomaji aupate ujumbe wa shairi kwa kuhusisha taswira hiyo na hali halisi za jamii; na kufaulu ama kushindwa kwa taswira kutegemea vile ambavyo taswira hiyo na maana yake vitaganda mawazoni mwao msomaji au msikilizaji.
Tunaweza kuona utekelezaji mzuri wa madhumuni hayo ya taswira katika baadhi ya mashairi ya K.K. Kahigi na M.M. Mulokozi katika kitabu chao cha Malenga wa Bara. Shairi la "Jua la Dhahabu" (kur. S 8-19), laweza kuwa mfano mzuri. Washairi wanatueleza kuhusu "Jua la Dhahabu" waliloliona "katika mji wa Arusha." Wanasema:
Miali yake imepenya
Anga la Nchi yangu
Na kukifukuza kiza
Mbele ya macho yangu
Shairi zima linafaulu kutuwekea mbele ya macho yetu taswira ya jua lenye miali mizuri ya rangi ya dhahabu - miali ipenyezayo kila mahali katika anga la nchi. Ni dhahiri kwamba hapa hii miali ya jua imetakiwa iwakilishe nguvu za Azinuo la Arusha; nguvu ambazo twadezwa kuwa huleta mwanRaza wa matumaini kwa wakulima na wafanyakazi; na wakati huo huo hufukuza giza la kudharauliwa, kunyonywa oa kugandamizwa kwa watu wanyonge. Ni jua linalowasha tabasamu katika nuoyo ya wanyonge. Japokuwa hili oi shairi fupi sana, taswira yake imeeleza mambo mengi na marefu ambayo humpa msomaji uwanja mpana wa kuyaeleza na kuyafafanua. Mawazoni mwa msomaji, picha ya pambazuko inajichora baada ya kusoma shairi hili. Picha inayotoa rangi nzuri za dhahabu huku wanyonge wakimulikiwa ili wapande katika ngazi na vidato vya kuushikilia uchumi wa nchi na madaraka yote mikononi mwao.
Kinyume cha taswira hizo zinazoeleza ujumbe wa shairi kwa urahisi na kwa undani, zipo taswira dhahnia ambazo ni ngumu kueleweka. Hizi zinaufanya ujume wa shairi uwe na ukungu, oa usieleweke vizuri. Njia hii ni mojawapo ya matumizi mabaya ya fani ya kazi ya fasihi - matumizi yanayopofusha welekeo wa maudhui badala ya kuupa mwanga mzuri.
Matumizi mengine mabaya ya taswira ni yale ya kusisitiza kuwa taswira iwe ni pambo tu katika shairi. Taswira inaweza kuwa na uzuri mwingi sana wa kimapambo; lakini hapo hapo inaweza ishindwe kuyafanya maudhui ya shairi yalete maana kamili akilini mwa msomaji ama msikilizaji. Ni afadhali mshairi atumie taswira na ishara chache zinazosadifu na kuongeza uzito wa maudhui ya shairi, kuliko kutumia mapambo tu ambayo wakati mwingi hutibua welekeo mzima wa maudhui ya shairi.
Tulisema kuwa taswira ni mbinu itumiwayo na mshairi kuumba picha kamili ya kitu, wazo au dhana, hali, na uzoefu fulani wa mtu katika akili ya msomaji au msikilizaji wa shairi. Ni wazi kuwa hali, mawazo, dhana, na kadhalika, hazitapimwa kutokana tu na kuwapo kwa taswira, bali zitapimwa kutokana na vile ambavyo taswira hiyo au hizo huoana na maudhui na uhalisi wa mambo. Taswira inaweza kuwa nzuri sana lakini ikashindwa kunasa hisi za watu kama msimamo wa mwandishi au wa mshairi unalegalega katika maudhui ya kazi yake. Kwa mfaao, japokuwa shairi la Shaaban Robert la "Kufua Moyo" (Kielelezo cha Fasili, uk. 48), linatuchorea taswira nzito inayoonyesha vita, damu ichuruzikayo, na kadhalika, bado haigusi sana mawazoni kwani hatuelezwi kama vita ni vya nani au vya kumpigania nani, na kwa hiyo hata huo ushujaa unaosifiwa hatuuthamini sana kwani haupewi uelekeo kamili.
Yote haya yanamaanisha kuwa ukuu wa taswira hauamuliwi na taswira yenyewe bali unaamuliwa na maudhui yaliyojengeka katika taswira hiyo. Kwa sababu hii, katika baadhi ya mashairi yapatikanayo kwenye kitabu cha Mashairi ya Miaka Kumi ya Azimio la Arusha, itaonekana wazi kwamba kwa sababu ya uwoogo na pia unafiki wa baadhi ya washairi ambao wanaimba siasa ya Ujamaa kikasuku tu, picha nzima waitoayo kuhusu maisha ya Tanzania miaka kumi baada ya Azinuo la Arusha haisadifu uhalisi wa mambo yalivyo. Kwa mfano, shairi la kwanza na K.O.M. Shaki (Ngariba) (uk. 15) linasema katika baadhi ya beti zake:
Faida zajulikana, tangu mirija kukata
Fedha haziendi tena, Ulaya kwa kwa
Pita Zatufaa sisi sena, uchumi tumekamata
Picha hii ya kujitegemea na kuukamata uchumi mikononi mwetu si picha ya kweli kwani tunajua wazi kuwa leo hii Tanzania, kama nchi zote "zinazoendelea," bado imo katika kunyonywa na mfumo wa uchumi wa kibepari. Y.S. Ndevumbili hali kadhalika anatoa picha ya uwongo katika shairi la 30 (uk. 80) asemapo:
Kwa faidaze twadara, viumbe ajimaina,
Waliokuwa kuchara, sasa tumevimbiana,
Si uvimbe wa harara, ni dhiki hakuna tena,
Haki limezikomboa, Azimio la Arusha.
Hii oi taswira ya uwongo inayotutaka tuamini kuwa ati leo hii Tanzania hakuna dhiki tena; hakuna matabaka. Ati leo hii Watanzania wote "wamevimbiana," na haki ioatawala. Kitakuwa kichekesho tukizilinganisha taswira hizi za uwongo na taarifa ya Mwl. J.K. Nyerere katika kijitabu cha Azimio lo Arusha Baada ya Miaka Kwni ambayo inaonyesha wazi kuwa bado hatujaenda mbali, bado hatujajitegemea, bado yako matatizo mengi; na si kweli kuwa dhiki hakuna tena au kuwa Watanzania wote tumevimbiana kwa afya bora na utajiri mwingi. Kwa hiyo hapa inaonekana wazi kuwa japokuwa shairi kama hilo la Y.S. Ndevumbili linatoa taswira nzuri ya maisha ya Mtanzania, taswira hiyo inatoa maudhui ya uwongo, kitu kinachoifanya ikose uzito.
Ufundi wa mshairi wa kuweza kufanya taswira aitumiayo iwe na sifa za uzuri na kueleweka haraka sana unategemea kama taswira hiyo imechotwa kutoka katika mazingira na maisha ambayo wasikflizaji ama wasomaji wa shairi lake wameyazoea oa wameyaishi.
Shairi lililo kielelezo kizuri cha ufundi huo ni lile la M.M. Mulokozi la "Maisha Yako" (Kunga za Ushairi na Diwani Yetu, uk. 107). Shairi hili linatoa taswira ya maisha ya mtu mnyonge wa tabaka la chini; taswira ambayo ikilinganishwa na hizo zilizotolewa katika Mashairi ya Miaka Kumi ya Azimio la Arusha, inaonyesha dhahiri jinsi hali ya Mtanzania ilivyopambwa kwa kutiwa chumvi mno na akina Shaki na Ndevumbili.
Mulokozi anaanza kwa kutupa taswira ya umasikini ambayo majengwa katika maelezo ya makazi ya mtu mnyonge na familia yake:
Ugali mchungu na kauzu wenye mchanga wamekwisha chunguni.
Watoto wanane wamezagaa sakafuni juu ya mkeka unaowazidi umri
Moshi wa kibatari ni mwingi kuliko mwanga wake..
Kitanda cha miyaa kinachoalika pembeni
Mbu waliovimba matumbo wanazuzuma ndaniya moshi
Buibui na mende watambaa ndani ya masizi
Panya kaangusha kawa kakojoa ndani ya majiya kunywa mtungini.
............................................................................................................
Kelele za magari mbali na karibu
Kelele za malaya na mteja chumba cha pili..
Hapa kuna mchanganyiko wa taswira za kuonekana na zile za hisi kwani tuwaonapo mbu, buibui na mende wakiishi pamoja na mume, mke na watoto wanane katika chumba kimoja, hapohapo tunaguswa hisi zetu kuhusu umasikini; na hao mende na panya wanatupa kinyaa.
Maelezo yatolewayo baada ya hapo kuhusu aina mbalimbali za milalo ya watoto pamoja na majina yao, yanakamilisha taswira hiyo ya umasikini:
Saburi amejikunja kama kamba
Mtihani kalala mguu mmoja juu ya kamba,
Mchago wa Sambusa ni matako ya Sikudhani,
Fujo anakoroma na amekwishamkojolea Majaliwa
Taabu amemkumbatia Tabia ambaye amevunja ungo ndotoni
Kaolewa na Sheikh mwenye volvo na majumba ya kupangisha
Kutokana na majina hayo tunaelezwa na mshairi kuwa masikini wanajaribu kuwa na saburi katika mtihani mkubwa wa maisha; na mara nyingi hawadhani wala kutumaini kuwa wataendelea kuishi katikati ya fujo na taabu za unyonge wao japo wanafaulu kufanya hivyo kwamajaliwa tu.
Katika sehemu ifuatiayo beti hizo tulizofdondoa tunaona matumizi ya taswira na ishara kueleza jambo ambalo kama lingeelezwa kwa lugha ya kawaida lingekuwa matusi makubwa. Mshairi ametumia picha mbalimbali kulieleza tendo la kukutana baina ya mume na mke. Katikati ya taswira hizi Mulokozi anatoa vidokezo juu ya kiini cha shairi hili, vidokezo ambavyo vinatakiwa vitutahadharishe kuwa maelezo na taswira mbalimbali ambazo huweza kutusisimua ndani ya shairi hili zisiishie tu katika kusisimua bali ziyatoe hayo maudhui yaliyokusudiwa. Jambo hili tunaliona katika marudio ya kauli ya "Maisha ya mfanyakazi huanza baada ya kazi." Katika kauli hii mmekusudiwa mambo makuu mawili: Kwanza, mshairi anaonyesha vile ambavyo kazi ielezwayo kuwa ni msingi wa uhai, hapa si hivyo; badala yake uhai wa mfanyakazi unaanza baada ya kazi. Pili, ni kauli ya kikejeli kwani taswira nzima tuonyeshwayo kuhusu hayo "maisha'' ya mfanyakazi ni ya kukatisha tamaa kwani imejazana dhidi, unyonge na umasikini. Kwa hakika kauli ya "kifo cha mfanyakazi huanzia kazini na baada ya kazi" ndiyo hasa ingesadifu hapa.
Maudhui hayo yameendelezwa katika ubeti wa nne:
Mwaka juzi mapacha, mwaka huu nini?
Nyama ya mifupa Sh. 18.
Mkizaa binti mnunulie opena
Mkizaa mwana mpe bastole na mtarimbo.
Hii ni taswira ya mzunguko wa balaa: mtoto atakayezaliwa na masikini hawa hatakuwa na maisha mazuri zaidi yao, mwanamke atakuwa mwuza baa, na mwanamume jambazi Tendo lenyewe la kujamiiana ambalo linatakiwa liwe chanzo cha furaha linakuwa kiini cha mashaka.
Mistari minne ya mwisho wa shairi hili inahitimisha taswira ya unyonge wa mfanyakazi, nayo inasisitiza mviringo huo wa balaa:
Lakini una maslahi gani wewe
Mwenye juhudi isiyo na riziki
Mwenye uzazi usio na malezi
Mwenye warithi wasio na urithi?
Mashairi mawili yatakayotuhitimishia maelezo yetu kuhusu matumizi ya taswira na ishara kauka ushairi ni lile la Kahigi na Mulokozi la "Vita" (Malenga wa Bara, uk 19) na la 'T. Mvungi la "Daktari Askari" (Chungu Tamu, uk. 11). Taswira ipatikanayo katika mashairi haya mawili ni ya ubwege wa vita. Washairi wanatuonyesha kuwr vita havina faida yoyote kwa mtu. Ni hasara tupu tena ya kipumbavu.
Katika "Vita" washairi wametumia taawira mbalimbali, hasa za kuonekana, kudharau vita.Hizi zimeongezewa uzito kwa matumizi ya tamathali mbalimbali, hasa ya tanakali ya sauti. Kwa mfano:
Boom- Mwaa! maiti mamia,
katika majia, - pote yamejaa!
Dhihaka kuhusu vita inajitokeza moja kwa moja katika beti kadhaa za shairi hili, hasa zifuatazo:
Rafiki wa leo, adui wc kesho,-
Vita mwenzi leo, vyakuua kesho!
Kukuru kakara! tufani ya vita
Ilikuja mara, halafu kupita!
Maiti twazika, fajaa ya vita,
Yaliyoondoka, yameshakupita!
Twavuta pumzi, ya nzuri amani,-
Ya wema mapenzi, vita kisirani!
Je, wewe mwanetu, vita vimeleta,
Heshima ya watu - pia kutakata?
Taswira hii inayokebehi na kudharau vita inajitokeza pia katika shairi la Mvungi la "Daktari Askari" ambalo pia linaonyesha jinsi rafiki wa leo awezavyo kugeuka kuwa adui wa kesbo katika vita. Shairi hili linaonyesha jinsi kijana Mtanzania aliyesomea udaktari Makerere ambako alikutana na kupendana na msichana wa Uganda, Eva (ambaye pia alikuwa akisomea udaktari), anavyokutana na mpenzi wake huyo vitani, kila mmoja akiwa upande wake. Urafiki na mapenzi baina yao, vyatakiwa sasa vigeuke na kuwa uadui kutokana na vita. Hatimaye, baada ya vita, wapenzi hawa wawili wanaungaoa tena, na mshairi anahitimisha kejeli na dhihaka yake juu ya vita kwa kusema:
Eva alilalama,
Akaninong'oneza, Sasa wewe huru mimi mateka,
Hapana tesa mimi,
Nipomweleza Camp David alicheka kwa dhati,
Alitushika vichwa mie na Ew akasema,
"Two doctors fighting for no reason,"Camp David hana akili, Moyoni nilisema,
Sisi tunalipwa,
Tunaponya watu,
Tunapigana kwa ajili ya nchi zetu...,
Tulirudish wa Bukoba, na Eva mateka,
Sasa nina mke.
Hapa mshairi kaikamilisha taswira ya vita iliyojaa dhihaka inayokebehi "uzalendo" wa "kuipigania nchi" ambako kunaongozwa na "utaifa". Matari wa mwisho wa "Sasa nina mke" unapiga muhuri dhihaka hiyo kuhusu vita kwa kuonyesha kuwa "uadui" baina ya watu katika vita hivi ni wa bandia tu.
Mashairi mawili tuliyoyaangalia mwishoni hapa ni vielelezo vizuri vya kazi za fasihi zitumiazo mbinu za kejeli, dhihaka na tashtiti katika kusawiri uhalisi wa maisha ya jamii; mbinu ambazo leo hii ndizo zimetawala katika fani na maudhui ya fasihi ya Kiswahili.
Turudie tena kusema kuwa mshairi mzuri hatumii taswira na ishara hivi hivi tu, bali huzitumia nyenzo hizi kusakafisha uzuri wa shairi lake kifani an kimaudhui. Mshairi adili hazingatii taswira na ishara hadi nyenzo hizo zikafunika kabua ukuu wa maudhni ya shairi lake. Mshairi mzuri daima huchagua taswira na ishara zielewekazo, au ambazo hata kama ni ngumu kidogo hata hivyo husaidia kulifanya shairi liwe oa maana na ujumbe mzito. Kwani kazi kuu ya taswira na ishara, kama viegezo vingine vya fani ya fasihi, ni kutumikia vema maudhui.
Maswali
1. Ijadili nafasi ya taswira katika taaluma ya ushairi.
2. Chagua mshairi mmoja kati ya wafuatao ujadili matumizi ya taswira katika kazi zake za ushairi. Unaweza kutumia muainisho uliotumiwa katika sura hii au wowote ule uonao unafaa:
a) Mulokozi na Kahigi
b) Saadani Kandoro
c) Theobald Mvungi
d) Akilimali Sno-White.