Zitto Kabwe kuibukia Kigoma kesho
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Dar/Kigoma. Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe kesho atatua jimboni kwake kuzungumza na wananchi
kupitia mikutano ya hadhara.
Uamuzi wa kumfukuza Zitto
(pichani) ulifikiwa juzi ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama Kuu
kutupilia mbali kesi aliyofungua Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya
Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema, iliyokuwa imeshikilia uanachama
wake.
Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ndiye
alitangaza kutimuliwa kwa Zitto akisema ni kutokana na kufungua kesi
mahakamani, kinyume na Katiba ya Chadema kipengele cha 8 (a) (x).
Jana,
Zitto ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) aliongoza kikao cha kamati hiyo, kilichojadili taarifa ya Tanesco
na baadaye alisisitiza kwamba hana taarifa rasmi ya uamuzi wa mahakama
na atakapoipata atazungumzia hatima yake.
“Kama
mnavyoona mimi naendelea na kazi na wala sina taarifa rasmi lakini
nikipata taarifa rasmi na mimi nitatoa taarifa rasmi, Ijumaa (kesho)
ninakwenda jimboni kuzungumza na wapigakura wangu ambao niliwaahidi
kufanya hivyo kabla ya vikao vya Bunge kuanza Jumanne ijayo,” alisema
Zitto ambaye taarifa zinasema alikuwa amepapanga kuwaaga wapiga kura na
baadaye kutimkia kwenye chama kipya cha ACT alichokiasisi.
“Muhimu
kwangu ni kufanya kazi ya Watanzania na nitafanya kwa mazingira yoyote
yale. Siasa yangu inajikita katika masuala, siyo watu, ukiandika kuhusu
Zitto siyo kwa ajili ya mtu bali masilahi ya Taifa.
“Nakuzwa, nakomazwa na hii ni changamoto, nitaendelea kufanya kazi zangu hadi nitakapopata taarifa rasmi.”
Mwanasheria
wa Zitto, Albert Msando juzi aliliambia gazeti hili kwamba, anafuatilia
uamuzi huo wa mahakama kabla ya kuona ni hatua gani watazichukua.
ACT wachekelea
Baadhi
ya wanachama na viongozi wa Chama cha ACT mkoani Kigoma wamedai
kufurahishwa na uamuzi huo, wakidai kuwa utakinufaisha chama hicho.
Mkazi
wa Mwandiga, Dunia Pemba alisema Zitto alipaswa kujiondoa ndani ya
Chadema pale tu alipovuliwa nyadhifa zake ili atazame sehemu nyingine
yenye demokrasia pana kwa vile chama hicho kilionyesha hakimhitaji tena.
“Sisi tulitangulia huku ACT na sasa tunamsubiri kwa
hamu, aje kujenga chama hiki ambacho ni tishio kubwa hapa nchini na bila
shaka kitachukua viti vingi vya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
huu, ndiyo maana kutimuliwa kwa Zitto Kabwe ni faraja kwetu kwa sababu
atapata muda wa kutosha kujenga chama,” alisema Pemba.
Pia,
mwenyekiti wa vijana wa ACT Tawi la Mwandiga, Stili Chuma alisema
anafurahia uamuzi ya Chadema ingawa kitendo cha jimbo lake kukosa
mwakilishi kinasikitisha.
Katibu Mwenezi wa Chadema
Jimbo la Kigoma Kaskazini, Shaban Kasugulu alipongeza uamuzi wa Mahakama
Kuu akidai haki imetendeka kwa vile suala la Zitto na Chadema
lilichukua muda mrefu na kusababisha watu kukosa mwelekeo.
Hata
hivyo, Boaz Chuma aliitupia lawama Mahakama Kuu kwa kuibeba Chadema
katika shtaka hilo kutokana na kutoa hukumu siku ambayo haikupangwa.
Dk Makulilo
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema
kufutwa uanachama kwa Zitto ni fundisho kwa wananchi ambao licha ya
kuchagua mbunge wanayempenda, lakini anaweza kuondolewa na vyama vyao.
“Wananchi
wanamchagua mbunge wao kupitia chama cha siasa lakini hawawezi
kumwajibisha hadi baada ya miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa ni
chama pekee kinachoweza kumwajibisha.
Dk Makulilo
alisema katika rasimu ya Katiba iliyokuwa ikipendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kulikuwa na kipengele kilichotaka wananchi wawe na
uwezo wa kuwajibisha wabunge wao, lakini kikaondolewa na Bunge Maalumu
la Katiba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk
Emmanuel Mallya kuondolewa kwa Zitto ni taratibu na kanuni za chama
kilichompitisha kugombea nafasi hiyo na hapo ndipo unaona umuhimu wa
kuwapo mgombea binafsi ili wananchi wawe na nguvu zaidi,” alisema
Mallya.
Mbunge wa Mbarali, Modesti Kilufi alisema bado wanaamini Zitto ni mbunge, bado ni mwenyekiti wangu na anaweza kukata rufaa.
Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Anthony Kayanda na Raymond Kaminyoge