Cheyo atafuta wagombea urais kupitia UDP
Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha UDP
Dar es Salaam. Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo
ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha UDP, amesema wanamkaribisha mwanachama
wa chama chochote cha siasa nchini kuwania nafasi ya urais kupitia
chama hicho.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam,
kiongozi huyo alisema chama hicho bado hakijateua mgombea urais, hivyo
milango iko wazi kwa wanasiasa ambao wako tayari kujiunga na chama hicho
kwa lengo la kuwania nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Hiki
chama ni cha Watanzania wote, tunatoa rai kwa mtu yeyote aliye tayari
kuwa mwanachama wetu, milango ya kuwania urais kupitia chama hiki iko
wazi,” alisema Cheyo.
Alisema yeye bado hajaamua kuwania nafasi hiyo kwa sasa, bali muda ukifika atasema, huku akidai kuwa kwa sasa ni mapema kutamka.
Wakati
huohuo, Cheyo alisema anasikitishwa na Ukawa kuendelea kuwahamasisha
watu wasiipigie kura Katiba Inayopendekezwa, kwani kufanya hivyo ni sawa
na kuwanyima haki wananchi.
“Raia wote wana haki ya
kupigakura, kama Ukawa wanatembea kila kona ya nchi kuwahamasisha
wananchi kuacha kuipigia kura katiba hiyo ni kosa,” alisema Cheyo.
Kiongozi
huyo wa UDP alisema Tume ya Uchaguzi ndiyo yenye majibu ya mashine za
BVR zinazotumika sasa kuandikisha wapigakura kwenye Daftari la Kudumu
kama zinafaa au laa.
Alisema anashangazwa na baadhi ya
watu, hususan wanasiasa na wasomi wanaojitokeza na kusema mchakato wa
kuandikisha wapigakura usimamishwe kwa sababu wanazozijua wao.
“Kwa nini tunatoa majibu ambayo Tume inatakiwa kuyajibu,
ikiwa mashine hazitoshi au ni mbovu, basi yenyewe ndiyo ituambie. Sasa
kama kila mtu anasema lake huo siyo ustaarabu mzuri, tuache Tume ifanye
kazi yake,” alisema Cheyo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema bado mashine za
uandikishaji wa Daftari la Wapigakura walizoziagiza kutoka nje ya nchi
hazijafika na wanatarajia zitafika ndani ya wiki mbili zijazo.
Alisema
kwa sasa Tume inatumia mashine 250 na kazi ya uandikishaji mkoani
Njombe inaendelea, ikikamilika watatangaza ratiba ya mikoa mingine.
Awali,
Rais Jakaya Kikwete alitangaza rasmi kwamba tarehe ya upigaji kura ya
maoni ya wananchi kuamua kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa,
itafanyika Aprili 30, mwakani huu.
Alisema upigaji wa
kura ya maoni kuhusu katiba hiyo utafanyika Aprili 30, baada ya elimu na
kampeni juu ya kura hiyo kuanza rasmi Machi 30 na kuhitimishwa Aprili
29, mwaka huu kama sheria ya kura ya maoni inavyoelekeza.Alitoa rai kwa
wananchi kuhakikisha wanaipata katiba hiyo, kuisoma na kuielewa ili
waweze kufanya uamuzi sahihi badala ya kusubiri kuelezwa na watu
wengine.
Alisema tayari katiba hiyo imeshachapishwa
kwenye Gazeti la Serikali, hivyo akaagiza sasa ianze kusambazwa kwa
wananchi mara moja.
Aliwataka Watanzania kutokubali
kulaghaiwa na watu wachache wanaotaka kuwarudisha nyuma na kutaka kuona
katiba iliyo bora inakosekana.
Alisema sheria ya
kura ya maoni inamuagiza Rais kutangaza katiba kwenye Gazeti la Serikali
siku 14 baada ya kupokea ndani ya siku hizo atangaze kura ya maoni na
matokeo yake yajulikane ndani ya siku 70.