Jaji Mkuu aitaka dola ijipange kesi za mauaji ya albino
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman
Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman
amevitaka vyombo vya dola vinavyohusika na uhalifu, kujipanga kikamilifu
kushughulikia kesi za mauaji na ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa
ngozi.
Jaji Chande alitoa wito huo jana wakati akijibu
maswali ya waandishi wa habari baada ya hafla ya kuwaapisha Manaibu
Wasajili 43 wa Mahakama ya Tanzania kwenye Viwanja vya Mahakama ya
Rufani, Dar es Salaam.
“Taasisi zinazohusika na uhalifu
zinapaswa zijiandae. Sisi Mahakama tumeshaanza kuchukua hatua na
tutazipa kipaumbele kesi za mauaji ya albino na tutazipa kipaumbele hata
katika ngazi ya rufaa,” alisema Jaji Chande na kuongeza:
“Bidii
lazima zifanyike katika kufanya upelelezi mzuri na mashahidi
wajitokeze. Sisi Mahakama tuko tayari kushughulikia mashauri hayo.”
Akionyesha
jinsi ambavyo Mahakama imechukua hatua katika kushughulikia kesi hizo,
Jaji Chande alisema kesi hizo zilikuwa zimeshafikia 90, lakini hadi sasa
zimebaki kesi mbili katika Mahakama Tabora na tatu Mwanza.
Akizungumzia
uteuzi wa manaibu wasajili hao, Jaji Chande alisema kuwa wameteuliwa na
Tume ya Utumishi wa Mahakama, ikiwa ni hatua ya kutekeleza muundo mpya
wa utendaji wa Mahakama baada ya kutenganisha shughuli za utoaji haki na
shughuli za utawala.
Alisema manaibu wasajili hao
watapelekwa katika vituo mbalimbali vya Mahakama, ambapo wawili kati yao
ni manaibu Wasajili Waandamizi wa Mahakama ya Rufani.
Alisema
wengine watapelekwa katika Masjala Kuu, Masjala za Divisheni za
Mahakama Kuu na katika Masjala ya Wilaya ya Mahakama Kuu katika kanda
mbalimbali.
Kwa upande wake, Jaji Kiongozi Shabani Lila
alisema vipaumbele ambavyo wateule hao watapaswa kuzingatia katika
utendaji wao ni pamoja na kusikiliza na kuamua mashauri kwa wakati,
kuwawezesha wananchi kuifikia Mahakama kwa urahisi na kupafanya kuwa
mahali pa kukimbilia.
Alivitaja vingine kuwa ni kutoa
kwa wakati huduma, ambazo mwananchi anahitaji, mfano nakala za hukumu,
utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama na nyinginezo.
Naye
mmoja wa wateule hao Hakimu Richard Kabate, alisema licha ya kupewa
majukumu magumu, lakini watajitahidi kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni
na sheria za utumishi wa umma.