Kontena lalalia basi, laua 42, lajeruhi 23
Basi la Majinja likiwa limeangukiwa na kontena na kusababisha vifo katika eneo la Changalawe mafinga. Picha na Francis Godwin
Mufindi. Watu 42 wamepoteza maisha na wengine 23 kujeruhiwa
baada ya lori la mizigo kugongana na basi na kontena lililokuwa
limebebwa kuangukia gari hilo la abiria, katika ajali ya aina yake
iliyotokea eneo la Mafinga Changalawe mkoani Iringa.
Watu
37 waliokuwa kwenye basi hilo la kampuni ya Majinjah Express lililokuwa
likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam, walifariki papo hapo na wengine
watano kufariki wakiwa Hospitali ya Mafinga. Dereva wa basi na wa lori
hilo la kampuni ya Cipex, pia wamefariki.
Shuhuda mmoja
wa ajali hiyo, Nyasio Pascal, aliyekuwa akiendesha basi la Saibaba,
alisema aliliona lori hilo likijaribu kukwepa mashimo kwenye barabara
hiyo ambayo ni nyembamba, na mara likaanza kuyumba kulia na kushoto
baada ya kukanyaga shimo na ndipo lilipolifuata basi na kugongana nalo.
Alisema
kontena lililokuwa limebebwa na lori hilo, liliangukia juu ya basi na
kulikandamiza, jambo ambalo lilisababisha vifo vya watu wengi na pia
kuzuia watu waliokuwa karibu na ajali kuokoa watu waliojeruhiwa hadi
tingatinga lilipowasili. Hata hivyo, alisema mtoto mmoja mwenye umri wa
mwaka mmoja, alinusurika kwenye ajali hiyo bila ya kudhurika.
Miili
ya waliokufa imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mafinga, ambayo ina
chumba cha kuhifadhia miili ya watu saba tu, na mingine imepelekwa
Hospitali ya Rufaa ya Iringa.
“Hii ni ajali mbaya
ambayo haijawahi kutokea mkoani hapa,” alisema mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Amina Masenza aliyefika eneo hilo la ajali.
Wanaume saba na wanawake 35 wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo, iliyochukua maisha ya watoto watatu.
Katika
eneo hilo ambako ajali hiyo imetokea hali ilikuwa mbaya kutokana na
kontena la lori hilo kulalia basi na kukandamiza miili ya abiria, jambo
ambalo lilisababisha ugumu katika kuokoa abiria waliokuwemo ndani ya
basi.
Polisi wakishirikiana na watoa huduma ya afya
kutoka Mufindi walifika kusaidia katika kutoa huduma ili kuokoa wale
ambao walikuwa wamejeruhiwa na kuhitaji matibabu ya haraka.
Tingatinga
lilifika na kusaidia kulinyanyua kontena na hivyo kurahisisha kazi ya
kutoa miili ya wale waliokuwa wamebanwa na miili ya waliokufa pia.
Majeruhi wazungumza
Kevin
Humprey, aliyekuwa amekaa viti vya nyuma kwenye basi hilo, alisema
alisikia kishindo kimetokea na kuona kontena limelalia sehemu kubwa ya
basi.
“Baada ya kuona hivyo, nilianza kupiga kelele za kuomba msaada kwa kuwa tulikuwa porini,”alisema Humprey.
Abiria mwingine aliyekuwa amekaa viti vya nyuma, Josam Obel, alisema alishtukia tu kontena likiwa limelalia gari lao.
Alisema
lori lililokuwa linakwenda Mbeya liliacha njia kutokana na mashimo
yaliyokuwepo barabarani na kugongana uso kwa uso na kusababisha kontena
lililokuwa limebebwa na lori kuangukia kwenye basin a kulikandamiza.
Alisema
basi hilo lilikuwa na abiria wengi kuliko uwezo wake kwa kuwa lina
uwezo wa kubeba abiria kati ya 50 na 54, lakini lilibeba zaidi ya abiria
60.
Hali mbaya katika Hospitali ya Mufindi
Hali
katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi ilikuwa mbaya kutokana na watu
wengi kufurika kutaka kujua kama ndugu zao ni kati ya hao walikufa au
kujeruhiwa kwenye ajali hiyo.
Vilio vilitanda kila kona
ya hospitali hiyo hasa wakati miili ya waliokufa ilipokuwa ikishushwa
na kuwekwa eneo maalumu kwa ajili ya utambuzi, jambo lililofanya kazi
hiyo kuwa ngumu kutokana na kila mtu kutaka kuona maiti hizo.
Mganga
mfawidhi wa hospitali hiyo, Boaz Mnenegwa alisema walipokea miili ya
watu 37 ambao walikufa kwenye ajali na kwamba wengine watano walifia
hospitalini.
Alisema majeruhi 23 walifikishwa
hospitalini hapo na kati yao watano walifariki na wengine zaidi ya 10
wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
“Majeruhi hao wameumia maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo kichwani, miguuni na mikononi,” alisema.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari hayo mawili.
Alisema
madereva wa magari yote waliofahamika kwa majina ya Baraka Gabriel wa
basi na Makka Sebasian wa lori walikufa papo hapo na haikuweza
kujulikana idadi ya watu waliokuwamo kwenye lori hilo.
Hata
hivyo, Kamanda Mungi alisema ni vigumu kupata majina ya waliokufa na
majeruhi kutokana na shughuli za kutafuta kuendelea ili kuweza
kuwatambua.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa ajali hiyo ni mbaya ambayo haijawahi kutokea katika mkoa huo
“Tuko hapa kwa ajili ya kuhifadhi maiti na kutambua ndugu wa marehemu,” alisema.
Masenza
aliongeza kuwa barabara hiyo imekuwa na ubovu kila mara, hasa wakati wa
mvua inapochimbika na kuweka mashimo ambayo yalichangia ajali ya jana
kwa sababu gari zote zilikuwa zikipishana na kukwepa mashimo hayo.
Dereva
wa basi la Saibaba, Nyasio Pascal aliungana na mkuu huyo wa mkoa
akisema: “Sisi kama madereva ambao tunatumia barabara hii, kiukweli
tunakerwa na kipande hiki cha barabara kwa sababu ya mashimo na ni finyu
hamuwezi kupishana kwa hiyo ajali hii imetokea kwa sababu ya ubovu wa
barabara,” alisema.