Wakulima wa chai wanajiandaa kuimarika kiuchumi baada ya kusota miaka miwili


mkulima akivuna chai.
Mkutano wa wanachama wa Chama cha Wakulima wa Chai (Utega), uliofanyika Mei, 2013 na kwa kauli moja walichukua uamuzi wa kukifunga kiwanda walichokuwa wanamiliki kwa ubia na mwekezaji.
Haukuwa uamuzi rahisi kwa sababu walijua wazi kuwa baada ya kukifunga hawatakuwa tena na sehemu ya kuuzia mazao ya ambayo yaliwapatia kipato cha kuendesha familia.
Wakifunga kiwanda hicho, wakulima hao waliazimia kuacha kuuza majani mabichi ya chai kwa kiwanda hicho kushinikiza Serikali kumwondoa mwekezaji kwa kile walichodai ni kutowapa haki zao kwa mazao yao na hata faida ya kiwanda, wakati wao ni miongoni mwa wanahisa.
Wanasema kufungwa kwa kiwanda hicho kwa takriban miaka miwili kumeleta athari kubwa miongoni mwao.
Ilifika mahali, mwaka juzi wakatoa siku 20 kwa Serikali kufungua kiwanda ama sivyo wangefungua wao wenyewe. Hii ilitokana na hali ngumu ya kiuchumi waliyokuwa wanakabiliana nayo kwa kufungwa kiwanda hicho.
Ilibidi Serikali iunde kikosi kazi cha wadau wa chai, Julai mwaka 2013 chini ya uongozi wa Shirika Hodhi la Taifa (CHC), kikiwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo wa Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania.
Kikosi kazi hicho kilipendekezwa kama hatua za muda mfupi kuunda timu ya muda ya kusimamia uendeshaji wa kiwanda.
Kiligundua kuwa Utega ilikuwa tayari imekiuka masharti ya mkataba wa mauzo, ambapo imebainika kuwa chama hicho na mbia wake hawajamaliza kulipia mauzo ya kiwanda hicho.
Januari 4, mwaka huu ni siku ambayo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwapelekea wananchi hao ujumbe wa Serikali.
Kinana anasema kuwa kiwanda kilifungwa Mei 26, 2013 kutokana na wakulima zaidi ya 4,000 kutoridhika na mwenendo wa kiwanda hicho hasa katika mfumo wa kuwapatia masilahi ya mauzo yao ya chai.
Isitoshe, anasema wakulima hao wanalalamika kuwa menejimenti ya kiwanda haiweki wazi mapato na faida ya kiwanda hicho wakati nao ni wanahisa.
Kinana alisema kuwa katika uamuzi wake, Serikali imeamua kununua hisa za mwekezaji ili aondoke.
Alisema ili kiwanda kiweze kuanza kinahitaji mtaji, Serikali imeona haiwezi kuwachangisha wananchi na badala yake yenyewe itabidi itenge fedha kwa ajili ya kukiimarisha ili kianze kazi haraka iwezekanavyo.
Kinana anasema ili wakulima wawe na nguvu, inabidi wale wa Lushoto kuungana na wenzao wa chai Korogwe ili kuweza kukiendesha kiwanda hicho kwa ufanisi.
Anasema kabla ya mgogoro huo kuanza, wilaya hizo mbili zilikuwa zinashirikiana kuendesha kiwanda hicho.
Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania, Mhandisi Mathias Assenga anawataka wakulima hao kuandaa mashamba kwa ajili ya kuanza ukurasa mpya.
Anasema kinachotakiwa ni kuongeza juhudi ili wahakikishe kinazalisha kwa wingi na wanapata faida kubwa.
Lengo ni kuhakikisha zao hilo linawanufaisha na kuwainua kiuchumi kwa ustawi wa familia zao.
Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba ameshukuru mgogoro huo kumalizika kwa amani kwa sababu ulianza kuzua maneno yanayoelekea kumharibia sifa mbele ya wapiga kura wake.
Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia anasema: “Baadhi ya watu walikuwa wanataka kutumia mgogoro huu kupata ubunge, lakini wanajisumbua.”
Mwenyekiti wa Kijiji cha Balangai, Issa Zayumba anasema wakulima wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kuwarudishia Kiwanda hicho cha Mponde.
Mwenyekiti wa wakulima hao, Almasi Kassim anasema kuwa uamuzi huo wa Serikali utakuwa ni ukombozi mkubwa wa wakulima hao ambao walikuwa wakinyonywa.
“Kwa kuchukua uamuzi huo tunaona Serikali hatimaye imesikia kilio chao na kujali maslahi ya wakulima,” anasema Almas ambaye pia alitoa
pongezi pekee kwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba kwa jitihada zake za kuwa bega kwa bega na wakulima hao ili kuhakikisha kiwanda kinarudi mikononi mwao chini ya mfumo mpya wenye manufaa kwa wananchi.
“Tumefurahishwa sana na uamuzi wa serikali kwa sababu tulikuwa tunanyanyasika hasa kwa upande wa kimaisha. Watoto wetu walikuwa
hawaendi shule kwa kukosa ada,” anasema.
Anasema licha ya kiwanda hicho kufungwa na wananchi wenyewe, ili kujikomboa, athari za kifamilia zilikuwa kubwa kwa sababu mapato waliyokuwa wanayategemea walikuwa hawayapati.
Hata hivyo, baada ya kiwanda kurudi mikononi mwao, wanaamini kwamba sasa watapata mapato makubwa ikiwa ni pamoja na hisa kukua na kugawana faiada.
Wanaamini mapato yatakuwa makubwa zaidi na yatazifanya familia zao kuwa na maisha bora zaidi. Kilichopo ni wakulima hao kuongeza juhudi.
Powered by Blogger.