Lumbesa: Mbinu za kibiashara zinazotishia kuangamiza kilimo
Kwa miaka mingi, mikoa ya Njombe na Iringa ambayo awali
ulikuwa mkoa mmoja ina sifa moja inayofanana na inayoweza kuitambulisha
kirahisi.
Sifa hiyo ni uchapakazi wa wananchi wake
kiasi kwamba haikuwa bahati mbaya kwa Iringa kutambulika kama mojawapo
ya mikoa minne maarufu kwa kilimo, hasa mahindi na mazao mengine ya
chakula.
Tofauti na mahali kwingine ambako mahindi
limekuwa zao kuu la chakula kwa wakulima wa Njombe na Iringa, zao hilo
pia ni la biashara.
Wakulima wamejikuta wakilazimika
kuuza mazao yao yakiwamo mahindi, viazi kwa wafanyabiashara kutoka ndani
na nje ya mikoa hiyo miwili.
Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa wamefanya hivyo kwa ujazo usiotakiwa kisheria, yaani lumbesa ambao umewasababishia hasara.
Siku
zote, mwenye kulaumiwa ni Serikali kwa maana ya Wizara za Kilimo,
Chakula na Ushirika na pia ile ya Viwanda, Biashara na Masoko ambazo
zimeshindwa kusimamia Sheria ya Mizani na Vipimo ya mwaka 1982. Wakulima
wameilalamikia Serikali kwa kutotilia mkazo sheria hiyo na kukamata
bidhaa zote zinazosafirishwa zikiwa katika ujazo usiotakiwa na pia kuwa
na utaratibu wa kukagua bidhaa za kilimo zinazosafirishwa bila
kuzingatia sheria hiyo.
Ushuhuda wa mkulima
Rehema
Ngoda ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Lidodolelo wilayani Makete
mkoani Njombe anasema, msimu wa kilimo wa 2013/14, alilima ekari tatu za
viazi mviringo na kupata magunia 200 yenye ujazo wa kilo 100 kila moja.
“Sina
hamu tena na kilimo, baada ya kuvuna nilijua najikomboa katika
umasikini, kumbe ndiyo naingia katika umaskini, nilijikuta sijui cha
kufanya baada ya kuvuna viazi na kuvijaza kwenye magunia kwa ujazo
unaotakiwa na kuvipeleka sokoni, hakuna mteja aliyeshawishika kuvinunua
viazi vyangu, alisema na kuongeza;
“Wafanyabiashara
wengi walikuja na kuuliza bei na kuondoka bila kununua wakidai kuwa
ujazo nilioweka siyo ule wa kibiashara, yaani haukuwa wa lumbesa.”
Mkulima
huyo anaeleza kuwa baada ya kuona hapati mteja katika ujazo huo wa
kawaida aliamua kubadili msimamo ili viazi visioze na kumwingizia hasara
nyingine.
Anasema kutokana na uamuzi huo alijikuta
anapata magunia 98 baada ya kuyajaza kwa ujazo wa lumbesa na kuyauza kwa
bei ileile na kumfanya apate hasara.
Anasimulia kuwa,
alilazimika kuuza viazi hivyo kwa hasara kwa kuwa hakuwa na mahali
pengine pa kuvipeleka vikiwa na ujazo unaotakiwa kisheria na kuitaka
Serikali kuitilia mkazo Sheria ya Mizani na Vipimo ya mwaka 1982.
Anaeleza
kuwa mwaka 2007, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Mrisho alitoa
agizo linalohusisha Polisi kuanza kukamata magari yote yaliyokuwa
yanasafirisha mazao yalikuwa na vipimo batili.
Msimamo wa TCCIA
Kwa awamu
tofauti tangu mwaka 2005, TCCIA (Chama cha Wafanyabiashara Kilimo na
Viwanda) Mkoa wa Iringa wamekuwa wakifuatilia matumizi ya sheria hiyo na
mwaka 2013 walitoa mapendekezo ya kuboresha sheria hiyo ili iwe na
nguvu zaidi.
Mwenyekiti wa TCCIA Iringa, Lucas
Mwakabungu anasema wakati mikoa hiyo ikielekea kuamsha mapambano dhidi
ya lumbesa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wake
linatakiwa kuifanyia marekebisho sheria hiyo ya mwaka 1982 kwa kuwa
muswada wake wa marekebisho upo tayari.
“Muswada wa
marekebisho ya sheria hiyo uliandaliwa mwaka 2013. Katika muswada huo
inapendekezwa adhabu na faini kwa asiyefuata sheria iongezwe,” anasema
Mwakabungu na kuongeza kwamba faini kwa kosa hilo kwa sasa ni Sh100,000.
Anasema
utafiti wao kuhusu vipimo vya lumbesa unaonyesha kuwa Serikali imekuwa
ikipoteza zaidi ya Sh14.8 bilioni kama mapato ya kodi huku wakulima
nchini kote wakipata hasara ya zaidi ya Sh 174 bilioni kila mwaka.
“Mikoa
ya Iringa, Njombe, Serikali imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh2.5 bilioni
kila mwaka huku wakulima wakipoteza zaidi ya Sh14.7bilioni,” anasema.
Mwakabungu
anashauri vyombo vya umma vinavyosimamia sheria hiyo viongeze juhudi.
Vyombo hivyo ni pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Anataja pia Wakala wa
Mizani na Vipimo (WMA), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mamlaka
ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Ewura), Serikali za Mitaa na Polisi.
Mshauri
wa mradi huo wa ufuatiliaji matumizi ya sheria hiyo, Profesa Enock
Wiketie wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCO), anasema msingi wa kuiendeleza
Tanzania umejikita katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
Profesa
Wiketie anasema Tanzania inatakiwa iwe katika uchumi wa kati kwa kuwa
na viwanda vingi na kilimo chenye tija huku wastani wa pato la kila mtu
lifikie Dola 3,000 wakati uchumi ukikua kwa asilimia 10.
Mkulima,
Boniface Mlole analalamika: “Tunalima kwa kutumia zana duni, tunanunua
pembejeo kwa bei kubwa na gharama nyingine kama za kutunza mashamba yetu
zikiongezeka; pamoja na hayo yote tunajikuta katika mazingira ya kuuza
tunachozalisha kwa kuzingatia vipimo vinavyoelekezwa na wafanyabishara.”
Jackson
Mduda anapendekeza adhabu kubwa itolewe kwa watakaokamatwa
wakisafirisha mazao yaliyofungwa kwa mtindo wa lumbesa. Anataka wakulima
wawe wamoja kukabili tabia hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa
Njombe, Dk Rehema Nchimbi amewaonya viongozi wa Mikoa ya Iringa na
Njombe kuacha tabia ya kudai nyongeza wanapokuwa katika ununuzi kwa
wakulima.
“Ni kama tumelala katika vita hii inayotishia
uhai wa maendeleo ya mkulima. Nakumbuka miaka fulani vita dhidi ya
vipimo batili vya mazao ya mkulima ilianza kuleta mafanikio, lakini
tukajisahau imerudi. Muda wa kuamka umefika,” anasema.