Mifumo hii mibovu ya kodi inazigharimu halmashauri


Eneo la katikati ya jiji la Dar es Salaam lipo wilaya ya Ilala.
Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam ndiyo inayotajwa kuongoza kwa mapato kulinganisha na zingine kutokana na kuwa na vyanzo mbalimbali vilivyopo na ukweli kuwa ndio kitovu cha biashara nchini.
Hata hivyo, siku za karibuni mambo yameanza kwenda kinyume kutokana na sababu nyingi, lakini kubwa ikiwa ni pamoja na matumizi ya mawakala katika ukusanyaji wa mapato na mianya mingine ya uvujaji wa mapato.
Tatizo jingine linatajwa ni kuingiliana kwa mamlaka kama vile jiji na manispaa katika mfumo wa ukusanyaji. Takwimu za Sensa ya Mwaka 2012, zinaonyesha Manispaa ya Ilala ina wakazi wapatao milioni 1.2.
Kupotea mapato
Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Kheri Kessy akiwasilisha Makisio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti 2015/2016 wakati wa kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani, anasema ushuru wa masoko na vizimba mwaka wa fedha uliopita, uliwaingizia Sh800 milioni, lakini sasa wameambulia Sh374 milioni kutokana na kazi hiyo kufanywa na mawakala.
Anasema kiwango cha awali kilikuwa kinapatikana kutokana na kukusanya wenyewe jiji kupitia watumishi wake, lakini uamuzi wa karibuni wa kuwatumia mawakala kukusanya ndiko kunakowafanya wakaambulia mapato hayo ambayo hayalingani na ya awali.
“Fedha hizo ni taslimu ambazo tumepata kutoka kwa mawakala baada ya makusanyo, hali ambayo ni kushuka ingawa halmashauri inakuwa imejiondoa katika gharama zingine,” anasema na kuongeza, fedha hizo ndizo ambazo huwasilishwa na mawakala kwa manispaa.
Mapato mengine ambayo yameporomoka ni za maegesho ya teksi kutoka Sh85 milioni kipindi kilichopita hadi Sh42 milioni.
Mwingiliano wa ukusanyaji
Kipindi kirefu sasa kuna vuta nikuvute baina ya mamlaka mbili, jiji na manispaa, kuhusiana na nani ambaye anawajibika kukusanya mapato ya magari ya kukodi (teksi).
Jambo hili limewagawanya pia wafanyabiashara hao wa usafiri ambao kuna wanaolipa jiji na wengine Manispaa Ilala.
Hali hiyo inachangiwa na mwingiliano na Jiji la Dar es Salaam ambao nao wanakusanya fedha za maegesho ya huduma hiyo ya teksi. Eneo lingine ambako mapato ya halmashauri yameporomoka ni katika kodi zake za nyumba ambazo wamepangisha.
Kushuka mapato
Naibu Meya anasema, awali walikuwa wanakusanya Sh640 bilioni kila mwaka, lakini hivi sasa wanapata Sh30 milioni pekee na jengo linalotegemewa kwa sasa ni la Anaoutoglou, ambalo wamewapangisha benki ya DCB na majengo mengine yamechakaa na hayafai kwa matumizi ya binadamu.
“Majengo mengine hayafai kwa matumizi ya binadamu na mipango inafanywa kukaribisha uwekezaji,” anasema na kuongeza kuwa kimsingi kuna nakisi ya mapato ya manispaa, lakini hata hivyo anaamini kuwa matarajio ya makusanyo yatatimia na malengo yaliyowekwa yatafikiwa.
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa anasema katika bajeti yake, linatarajiwa kutumia zaidi ya Sh112 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, shughuli za utawala na matumizi ya kawaida na Sh11.1 bilioni ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi.
Vilevile, wamekusudia kutumia Sh19.3 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh12 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na bajeti hiyo inapitishwa, huku watendaji wakihimizwa kuhakikisha malengo yanafikiwa ili kuhimiza maendeleo.
Mtandao wa rushwa
Diwani wa Kata ya Segerea, Azuri Mwambagi anasema kuwa ukusanyaji wa mapato hivi sasa kuna ahueni kubwa hasa kwa upande wa masoko kwani, awali fedha zote walizokuwa wanakusanya ziliishia katika ukusanyaji wa taka na gharama zingine.
“Siku za nyuma kabla ya makandarasi, fedha zote zilikuwa zinaishia katika kulipia gharama za ukusanyaji wa taka na mambo mengine yasiyoeleweka,” anasema na kubainisha kuwa mgogoro na Jiji kuhusiana na teksi unashughulikiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Anasema mkuu wa mkoa aliwaahidi kuwa suala hilo atalifanyia kazi.
Mfumo mbovu leseni
Diwani huyo anasema mapato mengi ya jiji yanapotelea katika mifuko ya wachache kutokana na mtandao wa rushwa uliopo katika manispaa na ukiritimba wa kimfumo.
Anatoa mfano: “Leseni ya vileo ipo wazi kuwa ada yake ni Sh40,000 kwa maeneo ya pembezoni, lakini ili mwananchi aipate kutoka ofisi ya manispaa itamgharimu hadi Sh350,000.”
Anafafanua kuwa vishoka wa uchafu huo wamekita kambi nje ya ofisi za jiji wakishirikiana na baadhi ya wafanyakazi.
Anasema kitendo cha kung’ang’aniwa kwa mfumo wa sasa wa kutaka wafanyabiashara wanaotaka leseni kufika ofisi za manispaa moja kwa moja, kinachochea rushwa.
“Mtendaji angekusanya fomu na kuzileta halmashauri ambako angelipa na leseni kutolewa na hali hiyo ingesaidia pia utambuzi wa walipa kodi na wafanyabiashara wengine wa ngazi ya kata hali ambayo ingesaidia pia ukusanyaji wa mapato,” anasema.
Anabainisha kuwa hivi sasa, hakuna diwani hata mmoja ambaye ana orodha ya wafanyabiashara walipa kodi katika kata yake. Ukusanyaji huo mbovu wa kodi ndio unaoathiri shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye halmashauri nyingi nchini kama vile maji na barabara.Athari nyingine ni kushindwa kununua dawa za kutosha kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali. Athari nyingine ni kwa elimu, kushindwa kujenga vyumba vya kutosha vya kusomea.
Powered by Blogger.