Mbinu sita za kukifanya kilimo kiwe na tija, kiwavutie Watanzania wengi
Kwa muda mrefu sekta ya kilimo imekuwa ikizungumziwa kuwa ni
uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kwa kuwa ndiyo imeajiri asilimia
80 ya wananchi wote.
Watu wengi, wakiwapo wasomi,
wachumi, wanasiasa na hata wa kawaida, wamekuwa wakijiuliza kama kweli
kauli hiyo ni kweli. Kwa kuchambua mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya
kilimo wamekuja na majibu mbalimbali yakijumuisha changamoto zake.
Serikali
nayo kwa kutambua umuhimu na unyeti wa sekta hii, mwaka 2010
walitangaza mkakati unaolenga mapinduzi ya kisekta kwa kutangaza “Kilimo
Kwanza.” Kwa Mujibu wa Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anazindua mpango
huu alisema unalenga mapinduzi makubwa ya kisekta.
Mapinduzi
hayo yakalenga kukifanya kilimo kijiendeshe kibishara kwa maana kwamba
kilete tija itakayomwondoa mkulima kwenye umaskini na kumfanya tajiri.
Mikakati hiyo kama vile Mapinduzi ya Kijani na Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) imeweka michakato ya kuboresha maisha ya Watanzania maskini
wanaokadiriwa kufikia asilimia 80, sawa na walio kwenye sekta ya kilimo.
Hivi karibuni, ulifanyika mkutano hapa nchini ambao uliwahusisha wataalamu wa uchumi wa nje na ndani ili kujadili kilimo.
Kilimo kimeshuka
Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Benno Ndulu anasema hali siyo
nzuri kwa sekta ya kilimo kwa kuwa baadhi ya wakulima wameona hakina
tija.
Anasema sababu kuu ni kwamba mpaka sasa, kilimo
kinaonekana kuwa ndicho kimeajiri watu wengi lakini kimetoa mchango
mdogo sana katika kupambana na umaskini nchini. Anasema tafiti za
karibuni zinaonyesha sekta ya huduma ndio inayotoa mchango mkubwa katika
kupunguza umaskini.
“Mchango wa kilimo katika
kupunguza umasikini umeshuka kutoka asilimia 30 mwaka 1998 hadi asilimia
21 mwaka 2014, wakati mchango wa viwanda umeongezeka kutoka asilimia
17.7 mwaka 1998 hadi asilimia 22 mwaka 2014,” anasema Profesa Ndulu.
Profesa
Ndulu anasema hata mfumo mzima wa kupata mapato kupitia fedha za kigeni
nao umebadilika, huku pia sekta ya kilimo ikionekana kupigwa kikumbo na
sekta za Utalii, dhahabu, viwanda na usafirishaji wa mizigo nje ya
nchi.
Anasema hivi sasa watalii wanaliingizia taifa
Dola za Marekani 2 bilioni (Sh3.6 trilioni), dhahabu Dola 1.7 bilioni
(Sh3 trilioni), viwanda Dola 1.3 bilioni (Sh2.3 trilioni), huduma za
usafirishaji mizigo nje ya nchi Dola 860 milioni (Sh1.5 trilioni)
ikifuatiwa kwa ukaribu kabisa na kilimo kinachoingiza Dola 830 milioni
kwa mwaka.
Hata hivyo, gavana huyo anashauri Serikali
kusogeza huduma za viwanda karibu na mashamba ili wakulima waweze
kunufaika zaidi na mazao kuliko ilivyo hivi sasa na mazao mengi
huharibika kutokana na kuchelewa ama kushindwa kupelekwa kwenye viwanda
kwa ajili ya usindikaji.
Profesa Ndulu anasema kuwa
ingawa mfumo wa kuingiza mapato ya fedha za kigeni nchini umebadilika,
kama mabadiliko hayo yatatumika vyema yanaweza kutoa fursa kwa Tanzania
kuhudumia nchi za jirani zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam.
Msukumo kwenye kilimo
Mwenyekiti
wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, anasema tatizo
kubwa lililopo kwenye sekta ya kilimo nchini ni kushindwa kuweka tija
katika kilimo, kama ambavyo nchi za Asia zimefanya na kufanikiwa.
“Ukiongeza
tija kwenye kilimo, unapunguza gharama za kuajiri kwa sababu chakula
kinakuwa bei ya chini, pia unapunguza gharama za wafanyakazi kwa sababu
wanaweza kununua chakula cha kutosha kwa fedha wanazozipata,” anasema
Profesa Lipumba. Anasema wasiwasi wake ni kuwa kama sekta ya huduma
inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umasikini kuliko kilimo,
msisitizo katika kilimo unaweza kupungua pia.
Anapendekeza
serikali kuendelea kuwapa msaada wakulima kwa sababu wana mchango
mkubwa katika kupatikana kwa malighafi nyingine zinazotumika viwandani.
Kurahisisha usindikaji
Mkurugenzi
Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe, anasema idadi ya watu
wanaoishi vijijini imepungua kutoka asilimia 80 hadi asilimia 65, lakini
hata hivyo siyo wote wanajishughulisha na kilimo.
“Takwimu
zinaonyesha kuwa karibu asilimia 40 ya kipato kinatoka nje ya kilimo,
lakini bado kuna malalamiko kwamba hakijaongeza tija. Watu wanatoka
kwenye kilimo siyo kwa sababu wanakimbia umasikini bali kwa sababu
wanaobaki pale wanatosheleza kuzalisha mazao yanayohitajika,” anasema
Profesa Wangwe.
Wanafaidi wachache kiuchumi
Mwenyekiti
wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, anasema matokeo
yaliyotolewa na BoT yanaonyesha kuwa uchumi hivi sasa unakwenda kwa watu
wachache na kuondoka kwa watu wengi ambao ndiyo wapo kwenye sekta ya
kilimo, hivyo siyo jambo la kulifurahia.Anasema kitu kinachotakiwa
kufanyika kwa sasa ni kuendelea kuwekeza kwenye kilimo ili kuwanufaisha
wananchi wengi, tofauti na mchango unaotolewa na sekta ya utalii
inayowagusa wananchi wachache.
“Lazima tuendelee
kuwekeza zaidi kwenye kilimo wala tusibabaike wala kutetereka kwa
kudhani kwamba sasa miaka kumi iliyopita tulikuwa tunategemea dhahabu,
sasa tutegemee utalii, hapana. Kilimo kinakuwa kwa asilimia tatu na nne
kwa mwaka inabidi tulime kikue kwa zaidi ya asilimia 10,” anasema Zitto.
Zitto
anapendekeza kuwa huduma za kifedha ziwafikie wakulima kwa kuwa
hawakopesheki, hawana bima na pensheni. Wachambuzi wote wa uchumi
wameweka bayana kuwa mikakati ya kuinua kilimo bado haijafanikiwa. Hata
kasi ya kukua kwa sekta hii imekuwa ni ya kuchechemea na ndiyo maana
haiwavutii watu wengi, hasa binafsi, kuwekeza.
Mbinu
sita zimetajwa na wachambuzi hao wa uchumi kama njia mwafaka ya kutia
msukumo wa sekta hii. Hizi ni ujenzi wa viwanda uwe karibu na mashamba,
wakulima wapewe ruzuku za kuwahamasisha na mazingira ya vijijini
yaboreshwe ili kuzuia wimbi la wanaokimbilia mijini.
Jambo
jingine ni kuthaminisha mashamba kwa kuwa na hati miliki
zinazowawezesha wakulima kwenda kukopa na vilevile zianzishwe bima za
kilimo ili kufidia hasara wanazopata.
Mifuko ya akiba
ya jamii nayo iweke mfumo ambao utawawezesha wakulima kuweka akiba ya
uzeeni ili wakulima nao wawe na muda wa kustaafu na wawe wanalipwa
pensheni.