Polisi waanza kuchunguza madai ya Dk Slaa
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza
kuchunguza malalamiko ya Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbroad Slaa ya
kutaka kulishwa sumu na Mlinzi wake.
Madai hayo ambayo
yamekuwa gumzo katika vyombo vya habari wiki hii huku wananchi wakihoji
uhalisia wake, yamemuhusisha mlinzi huyo wa Dk Slaa huku yeye mwenyewe
akikataa tuhuma hizo na kudai kuwa ameteswa na walinzi wa chadema.
Kamanda
wa kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova amesema hayo leo
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu
taarifa hizo zilizofikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbey
kupitia wakili wa Chadema John Malya ambae aliambatana na mtuhumiwa
Khalid Kagenzi (48) ambaye ni mlinzi wa Dk. Slaa ili akatoe maelezo kwa
niaba yake.
Mlinzi wa Dk. Slaa alidai kuwa ana majeraha
mwilini yaliyotokana na mateso aliyofanyiwa akiwa chini ya ulinzi
mkali wa maafisa wa usalama wa Chadema ambao walikaa naye na kumhoji
kuanzia tarehe 07/03 saa tano asubuhi hadi tarehe 08/03 mwaka huu saa
kumi jioni.
Aidha Kamanda Kova amesema kuna mambo
mawili yanafanyiwa uchunguzi likiwemo la mlinzi Khalid Kagenzi na la
pili ni dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia mlinzi
huyo na kumsababishia majeraha mwilini mwake.
Kova
aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la
shambulio la kudhuru mwili ni Boniface Jacob, (32) mkazi wa kisiwani
Ubungo, ambae ni diwani kata ya Ubungo kupitia Chadema,Hemed Ally Sabula
(48) mkazi wa Tandale kwa Tumbo ambae Afisa Usalama wa Chadema,Benson
Mramba (30)mkazi wa Tabata Kisukuru ,Afisa Utawala wa Chadema.
Aliongeza
kuwa watuhumiwa hao watatu wapo chini ya ulinzi kwa makosa yaliyotajwa
dhidi ya Khalid Kagenzi na shauri litafikishwa mahakamani kupitia kwa
wakili wa serikali ili kujiridhisha kisheria na hatimaye kutoa maamuzi
kuhusu mashtaka yao.