CCM yapata pigo, nani ataimba kama Komba?
JOHN DAMIANO KOMBA 1954 Alizaliwa 1963-70 Shule ya Msingi Lituhi 1971-74 Shule ya Wavulana Songea 1975-76 Chuo cha Ualimu Kleruu 1988-90 Chuo cha Magdeburg path 1978-79 Chuo cha Kijeshi Monduli 1978-92 Ofisa wa JWTZ 2006-08 Chuo Kikuu cha Washington 2005-15 Mbunge Mbinga Magharibi
Mbunge wa Mbinga Magharibi na mkurugenzi wa kundi la
uhamasishaji la CCM, Tanzania One Theatre (TOT), Kapteni mstaafu John
Komba (61), amefariki dunia jana.
Akithibitisha kifo
hicho Dk Elisha Ishan alisema; “Nilimpokea na kuanza kumpima shinikizo
la damu na vipimo vingine lakini tayari vilikuwa havifanyi kazi na hapo
ndipo tukathibitisha kuwa ndugu yetu ameaga dunia.”
Dk
Ishan wa Hospitali ya TMJ alisema kuwa, Kapteni Komba alifikishwa
hospitalini hapo saa 10:00 jioni akiwa amebebwa katika machela.
Dk
Ishan alisema hawezi kujua kilichomuua lakini akaongeza alikuwa na
tatizo la shinikizo la damu na hivi karibuni alikwenda kwenye kiliniki
yake.
“Kwa kifupi ni hayo na kwa sasa mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.”
Akizungumzia
msiba huo, Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel alisema
Komba aliyekuwa nyumbani kwake Tangi Bovu jijini Dar es Salaam alianza
kujisikia vibaya kutokana sukari yake kuwa juu wakati huo huo presha
yake nayo ilikuwa imepanda, hivyo walimpeleka Hospitali ya TMJ iliyopo
Upanga kwa matibabu.
Alisema kwa sasa mwili wa mbunge
huyo ambaye ni kada wa maarufu wa CCM umehifadhiwa Hospitali ya Lugalo
na kwamba taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwake.
Nape amzungumzia
Awali
Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye alisema kuwa
Kamati Kuu (CC) ya chama hicho imepokea kwa mshituko taarifa ya kifo
hicho iliyotokea ghafla.
“Pengo lake ni vigumu
kuzibika nikinukuu maneno ya Mwenyekiti wa chama chetu Taifa, Jakaya
Kikwete; “ Chama kimepata pigo kubwa ukizingatia kwamba alikuwa kada na
mhamasishaji mkubwa wa chama na kwamba atabaki kuwa historia
iliyotukuka.”
Mtoto wake asimulia
Mtoto
wa marehemu, Claudia alisimulia kifo cha baba yake kuwa: “Baba alianza
kujihisi vibaya wiki iliyopita na walimpeleka Hospitali ya Sanital,
Mikocheni na alionekana shinikizo la damu na sukari vipo juu.”
Alisema
hali ilibadilika baadaye (leo) jana na walipokuwa wanamuwahisha
hospitali, alikuwa akipiga kwikwi na alipofika hospitali alipopimwa
alikuwa ameshafariki dunia.
Claudia alisema kuwa
Februari 26 alifanya sherehe ya kuzaliwa na baba yao aliwaita pamoja na
kuwaambia wapendane. “Siku hiyo baba alituambia wanangu mpendane…
akanipa zawadi ya laptop,” alisema.
Nyumbani
Nyumbani kwa marehemu, waombolezaji walianza kumiminika jioni na wengi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM jana.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana alikuwa mmoja wa waombolezaji waliofika nyumbani kwa marehemu kuhani msiba huo.
CCM Zanzibar wamlilia
Viongozi
wa Serikali na wanasiasa Zanzibar wamesema CCM kimepata pigo kwa
kupoteza nguzo yake ya kisiasa kufuatia kifo cha Komba aliyefariki
wakati chama hicho kikiwa katika matayarisho ya kuelekea Uchaguzi Mkuu
mwaka huu.
Waziri wa Fedha Zanzibar, Omary Yussuf Mzee
alisema Komba alikuwa mtu wa watu kiongozi anayejiamini akijua kazi yake
na ameacha pengo kubwa kwa CCM wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Wasanii wamlilia
Kiongozi
wa TOT na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Khadija Kopa akimuelezea
marehemu, alisema: “Alikuwa kiongozi, alionyesha njia lakini sasa
ametoweka.
“Alitushikia mshumaa, aliwasha taa mbele ya safari, lakini sasa taa imezimika,” alisema.
Naye
Abdul Misambano, mwimbaji wa taarabu mahiri wa TOT, alisema: “Kwa kweli
mimi naona haya ni kama majanga...tulikuwa tunajipanga kwa kampeni,
lakini sasa sioni mbele.
Baadhi ya wasanii mbalimbali
waliowahi kufanya naye kazi za sanaa kwa miaka ya nyuma wameelezea
kuguswa na msiba huo huku wakielezea jinsi walivyomfahamu wakati wa uhai
wake.
Msanii mkongwe wa nyimbo za dansi, Hamza Kalala
alisema ameshtushwa sana na msiba huo huku akibainisha kumfahamu tangu
mwaka 1985, alipokuwa akitumikia bendi ya JWTZ.
Alisema,
marehemu Komba kwa mara ya kwanza walifahamiana naye kwenye sherehe za
mbio za Mwenge, uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba mkoani Kagera.
“Tuliongea
sana kuhusu muziki, mpaka anaondoka kwenda CCM hakuwa amebadilika uwezo
wake wa kisanaa, kuwa na kipaji kikubwa cha ubunifu wa kutunga
mashairi…kwa kweli tumempoteza mtu muhimu sana katika tasnia ya muziki
huo wa dansi,” alisema Mzee Kalala.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya Aset na Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka
alisema:“Miaka ya ushindani wa bendi 2000/03 tulikuwa wote mpaka
tukajenga mahusiano makubwa sana, alininshauri kama kaka yangu kwenye
muziki na ndani ya chama, Nec, mpaka hatua ya mwisho alitaka kuivunja
TOT. Kwa kweli sijui niseme nini yaani nimeishiwa nguvu kabisa, siyo
rahisi kusahau msiba wake,” alisema Asha.
Naye msanii
mkongwe wa bendi ya Magereza, Mafumu Bilali ‘Mbombenga’ alisema Komba
alikuwa na mchango siyo CCM tu, bali kwa taifa na jamii kwa ujumla na
kwamba mchango wake hautasahaulika.
Imeandaliwa na Ibrahimu Bakari, Tausi Mbowe, Kalunde Jamal, Ibrahimu Yamola na Mwinyi Sadallah