Ushahidi upande wa mashtaka kesi ya Ponda wafungwa
Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
akisalimiana na mkewe kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi yake katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, jana. Picha na Juma Mtanda
Morogoro. Upande wa mashtaka katika kesi ya jinai
inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh
Ponda Issa Ponda, umefunga ushahidi wao baada ya kupeleka mashahidi
tisa.Shahidi wa mwisho wa upande wa mashtaka askari E.9295 D/CPL, Juma
Koroto kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(RCO),
Morogoro ambaye alikuwa mpelelezi wa kesi hiyo.
Akiongozwa
jana na Wakili wa Serikali, Benard Kongola katika Mahakama ya Mkoa wa
Morogoro, shahidi huyo alidai kuwa Agosti 11, 2013 alipokea jalada la
kosa la uchochezi lenye namba Moro/IR/ 4473 /2013 lililomtuhumu Sheikh
Ponda kutoa maneno ya uchochezi Agosti 10 mwaka 2013.
Shahidi huyo alidai kuwa Agosti 19, 2013 mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kujibu mashtaka yote matatu yanayomkabili.
Upande
wa utetezi ukiongozwa na Wakili Juma Nasoro ulimuuliza shahidi huyo
maswali ya msingi ikiwa ni pamoja na kutaka kujua kama Sheikh Ponda
alihojiwa baada ya kukamatwa na nani ni mlalamikaji sahihi katika kesi
hiyo.
Akijibu maswali hayo, shahidi huyo alidai kuwa
hakuwahi kumuhoji mshtakiwa kutokana na kushindikana kukamatwa katika
eneo la tukio.
Alisema hata alipokamatwa baadaye, mshtakiwa alikataa kuhojiwa mkoani Morogoro.
Mahakama
ilielezwa kuwa mlalamikaji ni Jafert Kibona aliyekuwa RCO kwa wakati
huo, lakini kesi hiyo ipo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo alihairisha kesi hiyo hadi
Machi 9 kwa ajili ya kuanza kusikiliza upande wa utetezi.