Chadema Mbeya yasema mwisho wa CCM Oktoba
Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi
Mbeya. Mwenyekiti wa Chadema mkoani hapa, Joseph Mwachembe
maarufu kwa jina la China amesema chama chake hakina ndoto ya kuwapo kwa
serikali ya mseto awamu ya tano ya uongozi wa nchi, kwa vile
kimejiandaa kushinda kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani .
China
alisema Chadema inaamini kwa niaba ya Watanzania kwamba mwisho wa
utawala wa CCM ni Oktoba mwaka huu, hoja za baadhi ya watu kwamba CCM
ikikosa wabunge wengi ikubali kuunda serikali ya mseto ni propaganda za
wafuasi wa CCM.
Alitoa kauli hiyo alipoulizwa maoni ya
chama chake kuhusu taarifa kwamba upinzani watapata wabunge wengi,
lakini rais atatoka CCM katika uchaguzi ujao na kuishauri CCM ijiandae
kuunda serikali ya mseto.
Hivi karibuni mwanasiasa
mstaafu Kanali Edmund Mjengwa (68) aliishauri CCM iwe na mawazo ya
kujiandaa kuunda serikali ya mseto ikiwa rais atatoka CCM na wabunge
wengi ndani ya Bunge wakawa ni wa upinzani.
Naye Mbunge wa zamani wa Musoma Vijijini, Paul Ndobho alitoa kauli kama hiyo alipozungumza na mwandishi wetu Kanda ya Ziwa.
Akifafanua
hoja zake jana, China aliwasihi Watanzania kushika moja la kuwachagua
wagombea wa chama kuanzia rais hadi madiwani ili kuundwa kwa serikali
itakayofanya kazi kwa uhakika zaidi .
Alisisitiza kwamba Chadema itashinda kwa wingi viti vya udiwani, ubunge na urais na kwamba hawana ndoto za kuwapo kwa mseto.
Naye
Mwenyekiti wa CUF mkoani hapa Yassin Mrotwa akitoa maoni yake alisema
CUF ina uhakika kwamba CCM imefika kikomo kwa sababu Watanzania
wamechoshwa na ufisadi uliopo serikalini.
Wafanyakazi
wamechoshwa na kukopwa fedha zao kupitia mishahara hata mifuko ya
hifadhi, wakulima wamechoshwa kukopwa mahindi na mpunga,” alisema na
kuongeza: “Kibaya zaidi ni kwamba CCM haina mgombea safi na makini.”
Mrotwa alisema mazingira ya chama chake kushinda urais
ni makubwa kuliko hesabu za wabunge na madiwani na kwamba kinachotakiwa
ni CCM kujiandaa kukabidhi madaraka kwa utulivu.
Kuhusu
maoni ya kuwapo kwa serikali ya mseto, alisema haiwezekani kwa vile
katiba iliyopo na hata inayopendekezwa haijaruhusu kuwapo kwa serikali
ya aina hiyo. Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM mkoani
Mbeya, Bashiru Madodi alipoulizwa maoni yake kuhusu suala hilo alisema
chama chake hakina ndoto ya kuwapo kwa serikali ya mseto kwani kitapata
ushindi wa kishindo kuanzia madiwani, wabunge hadi rais.
Madodi alisema CCM imejipanga kuwakata ngebe wapinzani kwa kuwapoka baadhi ya majimbo na kwamba imejipanga haina wasiwasi.
“Kwa CCM kufikiria kuunda serikali ya mseto hiyo haitatokea ni ndoto za wachache’’ alisema.
Naye
mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Stephen Mwakajumulo alipouulizwa
kuhusu suala hilo alisema pamoja na kukua kwa demokrasia, CCM ikijipanga
kwa kuteua wagombea wanaopendwa na wananchi itapata wabunge wengi
kuliko wa upinzani.
“Lakini CCM itaingia mkenge kama
itawateua wagombea watakaopendwa na wapiga kura za maoni badala ya
wananchi wengi, lakini ikiwateua wapendwa wa wananchi itashinda majimbo
na kata nyingi sana,’’ alisema. Alisema serikali ya mseto kwa CCM
haitakuwapo mwaka ujao kwa vile upo uhakika wa CCM kushinda sana
wagombea wake.
Lakini Mwenyekiti wa Chama cha APPT
–Maendeleo mkoani hapa, Godfrey Davis alisema mawazo ya serikali ya
mseto ni mazuri na changamoto kwa vyama vya siasa kuweka mazingira
mazuri ya kudumisha amani ya nchi.
Davis alisema
serikali ya mseto ni nzuri katika nchi za kidemokrasia na kwamba ndiyo
maana hivi sasa waziri mkuu anapigiwa kura na wabunge ya kukubalika.
Alisema
kama Serikali ya mseto haitakuwapo upo uwezekano wa kuchafua nchi kwa
vile wabunge wanaweza kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais au waziri
mkuu mara tatu jambo ambalo rais anaweza kulivunja bunge.