Shule binafsi zatesa matokeo kidato cha nne
Mwanafunzi aliyeongoza kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne kitaifa mwaka jana, Nyakaho Marungu akipongezwa na mama yake Celestina Maro, nyumbani kwao Kitunda Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya mtihani huo. Picha na Goodluck Eliona
Dar es Salaam. Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato
cha nne umeongezeka kwa asilimia 10, chini kidogo ya viwango vya Matokeo
Makubwa Sasa (BRN), lakini shule za Serikali za vipaji maalumu, kongwe
na za seminari zimeendelea kuporomoka.
Katika matokeo
hayo, Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa
mwaka 2010, ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio baada
ya mwaka jana kushika nafasi hiyo lakini kwa upande wa shule zenye
watahiniwa chini ya 40. Shule iliyoshika mkia ni Manolo iliyopo Tanga,
mkoa ambao umetoa shule tano miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za
mwisho.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza
kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA)
ambao unaonyesha shule zote 10 za kwanza ni za binafsi.
Akitangaza
matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani
huo ni wanafunzi 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247
waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227, sawa na asilimia
58.25 ya waliofaulu mwaka 2013.
Dk Msonde alisema wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61.
Kwa mujibu wa maelekezo ya BRN, ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo ilipangiwa malengo tisa, ulipaswa uwe asilimia 70.
Hata
hivyo, pamoja na kuwa chini kidogo ( asilimia 1.7) kufikia wastani wa
ufaulu kitaifa, Msonde alisema: “Tumejitahidi kwani ni asilimia kama
moja na ushee ilibaki, walimu walifanya kazi nzuri na nina imani
tutaifikia.”
Alisema watahiniwa 297,365 waliandikishwa
kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 139,400 sawa na asilimia 46.88 na
wavulana 157965 sawa na asilimia 53.12. Watahiniwa wa shule walikuwa
244,902 ikilinganishwa na watahiniwa 367,163 walioandikishwa kufanya
mtihani huo mwaka 2013.
“Idadi ya watahiniwa wa shule
walioandikishwa kufanya mtihani huo ilipungua kwa asilimia 33.3
ikilinganishwa na watahiniwa walioandikishwa mwaka 2013.”
“Mwaka
2012 kati ya watahiniwa 386,355 waliofanya mtihani wa kidato cha pili,
watahiniwa 136,243 walirudia kidato cha pili na watahiniwa 250,112
waliendelea na kidato cha tatu ambao ndiyo waliosajiliwa kufanya mtihani
wa kidato cha nne mwaka 2014,” alisema na kuongeza:
“Kati
ya watahiniwa 297,365 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne
2014, watahiniwa 288,247 sawa na asilimia 96.93 walifanya mtihani na
watahiniwa 9,118 sawa na asilimia 3.07 hawakufanya mtihani kutokana na
sababu mbalimbali.”
Alisema watahiniwa wa shule, kati
ya watahiniwa 244,902 waliosajiliwa watahiniwa 244,410 sawa na asilimia
98.17 walifanya mtihani ambao wasichana walikuwa ni 110,603 sawa na
asilimia 98.13 na wavulana ni 129,807 sawa na asilimia 98.19. Watahiniwa
4,492 sawa na asilimia 1.83 hawakufanya mtihani.
Kwa
upande wa watahiniwa wa kujitegemea, alisema kati ya watahiniwa 52,463
waliosajiliwa, 47,837 ambao ni sawa na asilimia 91.18, walifanya mtihani
na ambao hawakufanya ni 4,626 sawa na asilimia 8.82.
Ufaulu wa masomo
Dk
Msonde alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo ya msingi
umepanda kati ya asilimia 1.28 na 11.22 ikilinganishwa na mwaka 2013.
“Ufaulu
wa juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili na asilimia 69.66 ya
watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hili wamefaulu na ufaulu wa
chini kabisa ni ule wa somo la hisabati ambalo asilimia 19.58 ya
watahiniwa wote waliofanya somo hili wamefaulu.”
“Ufaulu katika masomo ya sayansi yaani fizikia, kemia na
baiolojia umeendelea kuimarika kidogo kwa kulingana na ufaulu wa masomo
hayo mwaka 2013,” alisema.
Katika matokeo hayo, ufaulu
wa kila somo na asilimia katika mabano ni Kiswahili (69.66), kemia
(56.73), Kiingereza (55.10), baiolojia (48.30), fizikia (46.71),
jiografia (37.96), uraia (37.70), historia (37.41), biashara (34.29),
uhasibu (42.20) na hisabati (19.58).
Matokeo yaliyozuiwa, kufutwa
Dk
Msonde alisema baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 184 waliobainika
kufanya udanganyifu. Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya
udanganyifu, 128 ni wa kujitegemea na 56 ni watahiniwa wa shule.
Alisema
kati ya watahiniwa hao, 128 wanatoka vituo viwili vya Kisesa mkoani
Mwanza na Ubago visiwani Zanzibar, huku wengine 56 wakitoka shule
mbalimbali.
“Tumeagiza mamlaka husika kuwachukulia
hatua za kinidhamu waliohusika katika vituo hivyo vya Kisesa na Ubago
kwani udanganyifu uliofanyika ni karatasi moja ya kujibia mtihani
imeandikwa na watu watatu tofauti jambo ambalo linaonyesha hakukuwa na
umakini,” alisema.
Shule kongwe na za vipaji hoi
Shule
za vipaji kama Ilboru, Mzumbe, Msalato, Kilakala, Tabora Boys, Kibaha
na Tabora Girls na Shule kongwe zinazomilikiwa na Serikali kama Pugu,
Zanaki, Bwiru Boys, Minaki, Azania na Jangwani, kwa mara nyingine
zimeshindwa kufua dafu kwa shule za binafsi.
Katika
orodha ya shule 10 bora shule binafsi zilizotamba katika matokeo hayo ni
Kaizirege (Kagera), Mwanza Alliance (Mwanza), Marian Boys (Pwani), St.
Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza Girls (Dar es Salaam),
Canossa (Dar es Salaam), Bethel Sabs Girls (Iringa), Marian Girls
(Pwani) na Feza Boys (Dar es Salaam).
Shule 10 za
mwisho ni Manolo (Tanga), Chokocho (Pemba), Kwaluguru (Tanga), Relini
(Dar es Salaam), Mashindei (Tanga), Njelekela Islamic Seminari (Kigoma),
Vudee (Kilimanjaro), Mnazi (Tanga), Ruhembe (Morogoro) na Magoma
(Tanga).
Watahiniwa 10 bora kitaifa
Dk
Msonde aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa ni Nyakaho Marungu
(Baobab), Elton Jacob (Feza Boys), Samwel Adam (Marian Boys), Fainess
Mwakisimba (St. Francis Girls), Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial),
Paul Jijimya (Marian Boys), Angel Mcharo (St. Francis Girls), Atuganile
Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St. Francis Girls) na Mahmoud Bakili
(Feza Boys).
Wasichana 10 bora kitaifa
Katika
matokeo hayo mwanafunzi bora kwa wasichana ni Nyakaho Marungu (Baobab),
aliyefuatiwa na Fainess Mwakisisimba (St. Francis Girls), Angel Mcharo
(St. Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St.
Francis Girls), Levina Ndamugoba (Msalato), Veronica Wambura (Canossa),
Sifaely Mtaita (St Maris Mazinde Juu), Catherine Ritte (St. Francis
Girls) na Anastazia Kabelinde (Kaizerege).
Wavulana 10 bora
Dk
Msonde alimtangaza kinara kwa wavulana kuwa ni Elton Jacob (Feza Boys)
akifuatiwa na Samwel Adam (Marian Boys), Mugisha Lukambuzi (Bendel
Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys), Mahmoud Bakili (Feza Boys), Amani
Andrea (Moshi Technical), Mahmoud Msangi, Elias Kalembo, Haji Gonga na
Kelvin Sessan wote kutoka Feza Boys.