Adam Kimbisa awawakia watendaji ‘wanaokumbatia wagombea urais’


Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa.PICHA|MAKTABA
Dodoma. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amewataka watendaji wa CCM kukaa ofisini kufanya kazi badala ya kuzunguka mikoani kusafisha njia ya wagombea urais.
Kauli hiyo ya Kimbisa imekuja siku chache kabla ya CCM kupuliza kipenga cha kuchukua fomu za kuwania uongozi katika Uchaguzi Mkuu.
Kimbisa alisema hayo alipofungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa(Nec) ya chama hicho jana.
Alisema baadhi ya wajumbe wa chama hicho wametwishwa mgombea urais wanayezunguka naye kila mkoa kumfanyia kampeni.
“Kuna watu wanapita huko wanahangaika, wanasumbuliwa na posho za wagombea urais. Sasa wewe kama ni M-nec au katibu unaachaje eneo lako tupu unahangaika na la wenzako?” alihoji.
Pia alihoji kuwa wanapofanya hivyo, madiwani wao watawapitishaje kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama wao wanahangaika na wagombea urais.
“Ningependa kuona mnahangaika katika kata zenu badala ya kwenda Mwanza na wagombea urais. Nasema hangaikieni kule kwenye kata na mitaa tulikopigwa katika uchaguzi uliopita, fanyeni ‘mishemishe’ tupite huko,” alisema na kuongeza kuwa:
“Sasa unajitwishaje mgombea urais aliyetoka madongo kuinama, humjui, hakujui, unahangaikia posho, njaa imekubana, unamsimulia mambo ya mgombea urais mchana kutwa... ya kwako yamekushinda. Tuache njaa na tamaa, tushughulike na maeneo tuliyokabidhiwa na wananchi.”
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Mkoa wa Dodoma, Donald Mejitii alisema kikao hicho kimetokana na azimio la kuwataka viongozi kufanya kazi katika maeneo yao.
ADVERTISEMENT
“Fanya siasa za nyumbani, simamia utekelezaji wa maendeleo ya wananchi wako na chama katika wilaya yako badala ya kwenda Tanga na kuanza kuwanadi wagombea urais,” alisema.
Katika kikao hicho Kimbisa alisema wanachama wanaofanya hivyo, wanaua Mkoa kichama kwa kuendekeza tamaa na njaa.
Alisema viongozi wanaofanya hivyo, wanatumia matumbo kufikiri kuliko kichwa na hivyo kulifanya tumbo kuwaendesha.
“Nawaombeni sana tusitumike, mapenzi yako yasikuhamishe kwenye eneo la kazi, sasa unakwenda Mtwara unajaa vumbi hadi kope zote za macho hazionekani tena, huku ukimnadi mgombea wako,” alisema.
Pia aliwataka viongozi wa CCM kujisahihisha kwa kuvunja makundi ndani ya chama.Alisema kwa bahati mbaya wanamakundi mengi yanayoanzia katika ngazi ya matawi hadi Wilaya.
“Kwenye Wilaya tuna makundi mengi sana, unaweza kuwakuta pia viongozi tunaowategemea wamo, katika sehemu nyingi watu hawaelewani hawasikilizani na hasa kipindi hiki,” alisema na kuongeza:
“Ni lazima tujitahidi tusipovunja makundi, tukienda vipande vipande nafasi ya ushindi ni ndogo sana.”
Alisema kwa kuvunja makundi itawasaidia katika kuondoa kero za wananchi, huku akiwataka kuacha siasa za mazoea ili kujiweka sawa katika siasa za mapambano na watani zao.
Kimbisa aliwataka viongozi hao kutumia haki na kuacha kushupalia ndugu na jamaa hata kama hawafai kugombea katika uchaguzi.
Powered by Blogger.