Moto mwingine waleta hasara Dar na Mwanza
engo lililopo Mtaa wa Libya na Mosque likiwaka moto jijini, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
-
Dar es Salaam / Mwanza. Siku nne baada ya
kuungua kwa nyumba iliyosababisha vifo vya watu sita wa familia moja,
Dar es Salaam, moto mwingine umeteketeza sehemu ya juu ya jengo la
ghorofa mbili la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo katikati ya
jiji.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova, alisema hakuna mtu aliyefariki wala kujeruhiwa
katika tukio hilo lililotokea kwenye makutano ya Mitaa ya Libya na
Mosque, Wilaya ya Ilala.
Kamanda Kova alisema Polisi
walipata taarifa jana saa 5.30 asubuhi kuwa kunguru ndio walisababisha
hitilafu ya umeme na jengo hilo kushika moto na kutekekeza mali ambazo
thamani yake haijafahamika.
Alisema moto huo ulioanza taratibu na kuongezeka ghafla kutokana na mitungi ya gesi iliyokuwamo kwenye jengo hilo.
Meneja
wa NHC Mkoa wa Dar es Salaam, Jackson Maagi alisema jengo hilo lilikuwa
na familia zaidi ya 10 na kwamba shirika hilo litahakikisha kuwa
waathirika wanapatiwa nyumba za kuishi wakati utaratibu mwingine
ukiendelea kufanyika.
“Tungekuwa sisi ni chanzo cha
tukio hilo tungesema tuwafidie lakini kwa kuwa sisi siyo chanzo,
tutawapa nyumba kwa ajili ya kujihifadhi, labda pengine chanzo halisi
kitakapopatikana ndipo tutajua tufanye nini,” alisema Maagi.
Hata
hivyo, mmoja wa wakazi katika jengo hilo, Ahlim Abdullah alisema jengo
hilo lilikuwa na familia nne katika ghorofa ya kwanza na ofisi kadhaa
katika ghorofa ya pili iliyoteketea kwa moto.
Akizungumzia
chanzo cha moto huo, alisema: “Waliokuwa nje wanasema walimwona kunguru
akisababisha shoti na moto kuanza kusambaa.”
Kamanda
wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Jeswald Nkongo alisema baada ya kupewa taarifa kuwa kuna moto, walituma
gari la kwanza kwa ajili ya kufanya tathmini ya ukubwa wa moto ndipo
walipobaini kuwa ulikuwa mkubwa na tayari ulikuwa umeshaanza kusambaa.
Wananchi walalamika
Baadhi
ya wananchi waliofika mapema katika eneo hilo walikitupia lawama Kikosi
cha Zimamoto kwa kufika mapema lakini kilichelewa kuanza kuuzima moto
kwa sababu ambazo hazikufahamika.
“Jengo limeanza
kuungua limekuja gari likiwa na maji kidogo, wamekaa muda mrefu hawajui
wafanye nini hadi tulipoanza kusaidia kuwatoa watu waliokuwa ndani.
Kama
wangekuwa na miundombinu mizuri jengo hili lisingeungua kiasi hiki,
Serikali ina mbinu za kukamata Wamachinga,” alisema mmoja wa wananchi
waliokuwapo katika tukio hilo, Selemani Vitus.
Shuhuda
mwingine wa tukio hilo, Abubakar Ali alisema hasara hiyo ingeweza
kudhitibiwa iwapo Serikali ingekuwa na vifaa vya kisasa vinavyowezesha
watu kuzima moto kwenye majengo marefu.
Ilivyokuwa
Wakati
mwandishi wa habari hii alipokuwa akiwasili katika eneo la tukio,
alishuhudia moshi mkubwa ukitoka ndani ya jengo hilo sehemu ya juu huku
polisi wakiweka uzio kuzuia mamia ya watu waliokuwa wakisogea karibu.
Ghafla
moto huo uliongeza kasi na kuezua mabati upande mmoja wa jengo hilo,
jambo lililowalazimisha askari kuwataka watu waliokuwa kwenye majengo ya
karibu kuondoka.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
watu wawili waliokuwa katika jengo la jirani walikuwa wakikataa kutoka
huku wakikitaka Kikosi cha Zimamoto kuhakikisha kuwa moto huo haufiki
mahali walipo. Hata hivyo, askari waliingia katika jengo hilo na
kuwatoa.
18 wanusurika Mwanza
Watu
18 wamenusurika baada ya moto kuteketeza nyumba moja na maduka katika
Mtaa wa Igoma Magharibi B, Kata ya Igoma jijini Mwanza na kusababisha
hasara ya zaidi ya Sh50 milioni.
Moto huo ulioanza jana
saa 11.00 alfajiri, uliteketeza nyumba ya Fares Peter iliyokuwa na watu
wanne na duka la Raphael Lukigwa likiwa na bidhaa mbalimbali.
Akizungumza
kwenye eneo la tukio jana, Lukigwa alisema chanzo cha mto huo ni
hitilafu ya umeme na kwamba uliteketeza nyumba na duka lote.
Mkazi
wa Mtaa wa Igoma Magharibi, Mussa Iddi alisema: “Umeme ndiyo chanzo
kwani miundombinu iliyopo hapa siyo bora. Tunaomba Tanesco iboreshe
miundombinu ya usambazaji.”
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Igoma Magharibi, Edwin Shija alisema hakuna kifo kilichotokea.
Imeandikwa na Raymond Kaminyonge, Kalunde Jamal na Beatrice Moses, Goodluck Eliona na Aidan Mhando, Mwananchi.