Mabilioni yahitajika kunusuru homa ya bonde la ufa
“Haya ni magonjwa hatari kwa binadamu na mifugo, tuliomba tangu Novemba lakini bado hatujapata, tukichelewa kufanya chanjo mifugo yetu ipo hatarini,” alisema Telele.
Dar es Salaam. Wizara ya Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi imeomba Sh30.2 bilioni Hazina kwa ajili ya chanjo ya
ugonjwa wa bonde la ufa ambao ni hatari kwa binadamu na wanyama.
Wizara
hiyo imesema ugonjwa huo ambao ulikuwa tishio mwaka 2006/07 hujirudia
kila baada ya miaka mitano na unaweza kutokea mwaka huu kama mvua kubwa
zitanyesha.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk
Titus Kamani alithibitisha wizara hiyo kuomba fedha hiyo ili kuendesha
chanjo za magonjwa manne ya mifugo lakini bado Hazina haijawapatia.
Magonjwa mengine ni homa ya mapafu ya ng’ombe, magonjwa ya miguu na midomo na sotoka kwa mbuzi.
Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Kaika Saning’o Telele naye
alithibitisha wizara hiyo kuomba Sh30 bilioni kwa ajili ya kufanya
chanjo nchi nzima.
“Haya ni magonjwa hatari kwa
binadamu na mifugo, tuliomba tangu Novemba lakini bado hatujapata,
tukichelewa kufanya chanjo mifugo yetu ipo hatarini,” alisema Telele.
Habari
za uhakika kutoka wizarani hapo zinasema wizara hiyo iliomba fedha hiyo
kupitia barua ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,
Yohana Budela yenye kumbukumbu namba PD/185/471/01/07 ya Novemba 10,
2014.
“Kuna uwezekano wa kutokea mlipuko wa Homa ya
Bonde la Ufa katika msimu wa mvua za masika zinazotarajia kuanza
mwishoni mwa Februari,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Hata
hivyo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Naibu wake, Mwigulu Nchemba
walipotafutwa kuzungumzia suala hilo, simu zao zilikuwa zikiita bila ya
kupokelewa.
Katika maombi hayo kwa Katibu Mkuu, wizara
ilisema ugonjwa wa homa ya bonde la ufa ni hatari kwa mifugo na binadamu
umekuwa na tabia ya kujirudia kila baada ya miaka mitano na mara ya
mwisho ulitokea mwaka 2006/07.
Takwimu za wizara hiyo
zinaonyesha kwamba Tanzania ina ng’ombe milioni 22.8, mbuzi milioni 18
na kondoo milioni 7 na kwamba mifugo hiyo iko katika hatari ya kupata
magonjwa hayo.
Kuhusu homa ya mapafu ya ng’ombe
inaelezwa na Katibu Mkuu kwamba wilaya 45 zimethitishwa kuwa na
maambukizi na kwamba ng’ombe milioni 15 wako katika hatari ya kupata
maambukizi ya ugonjwa huo.
Pia, ugonjwa wa miguu na
midomo nao tayari umeripotiwa kuwapo kwenye mikoa 16 ya Tanzania Bara na
ng’ombe 513,867 wameshapata maambukizi. Ng’ombe milioni 11 wako katika
hatari ya kuambukizwa kama chanjo haitapatikana mapema.
Kuwapo kwa ugonjwa huo kutasababisha biashara ya mifugo na mazao yake kwenda nje ya nchi usitishwe.
Pia,
ugonjwa wa sotoka ya mbuzi unaendelea kusambaa. Hadi sasa ugonjwa huo
umeripotiwa kwenye wilaya 33 na mbuzi milioni 10 wako katika hatari ya
kuambukizwa.
Ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaendelea kusambaa kwa kasi katika wilaya zote.
Takwimu
kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa watu wengi
wanapata maambukizi kutokana na kuumwa na mbwa ambao tayari
wameshaambukizwa.
Idadi ya mbwa walio katika hatari ya kupata maambukizi hayo ni kati ya milioni 3.5 hadi milioni 4.
Njia
kuu ya kuzuia kuenea na kusambaa kwa maambukizi ya magonjwa hayo ni
kuchanja mifugo yote kwa wakati. Alisema magonjwa manne yaliyoanishwa
ukiacha ugonjwa wa miguu na midomo, yapo kwenye orodha ya magonjwa
ambayo yameorodheshwa kama majanga kwa kitaifa.
“Ni
wajibu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kuagiza chanjo hizo
mapema iwezekanavyo na kuzisambaza kwenye wilaya zote na kisha kusimamia
shughuli za uchanjaji wa mifugo yote iliyo kwenye hatari ya kupata
maambukizi.