Rais Kikwete akubali utendaji wa Chadema Manispaa ya Moshi
Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Dkt.Ramadhan Dau
pamoja na wadau wengine wakitazama ramani ya jengo jipya la kitega
uchumi la NSSF mjini Moshi Kilimanjaro Commercial Complex wakati wa
hafla ya ufunguzi. Picha na Ikulu
Moshi. Rais Jakaya Kikwete, amempongeza Meya wa Manispaa ya
Moshi, Jaffar Michael kwa kile alichosema ni kusimamia vizuri na
kutekeleza Ilani ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kauli
hiyo ya Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa taifa wa CCM ni nadra
sana kutolewa na kiongozi wa CCM, akipongeza utendaji mzuri wa viongozi
wanaotoka vyama vya upinzani.
Meya huyo anatokana na
chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho ndicho
kinachoongoza Baraza la Madiwani kwa kuwa na theluthi mbili ya madiwani
wote wa Halmashauri.
Rais Kikwete alitoa pongezi hizo
juzi wakati akifungua jengo la kisasa la kibiashara lililojengwa
katikati ya mji wa Moshi na Shirika la Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF)
kwa gharama ya Sh64 bilioni.
“Hata Mstahiki Meya
nakupongeza kwa sababu nyinyi hamna Serikali sisi (CCM) ndio wenye
Serikali,”alisema Rais Kikwete huku akicheka kwa furaha na kuongeza
kusema;
“Kwa hiyo tunawashukuru kwa utekelezaji mzuri
wa ilani ya CCM na kwa sababu mnatekeleza vizuri, tutaendelea kuwapeni
pesa ya kuhudumia wananchi wa Tanzania,” alisema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete alitumia tukio hilo kuuagiza mkoa wa Kilimanjaro, kutenga
maeneo ya uwekezaji na kumtaka Meya huyo awe ni Meya wa maendeleo kwa
kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji.