Wizara ya Nishati yaahidi kusimamia ushindani wa haki
Dar es Salaam. Serikali imesema
itasimamia ushindani wa kibiashara wa haki na kutengeneza mazingira
wezeshi kwa waagizaji wa mafuta nchini ili kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara hao wananufaika na biashara hiyo.
Akifungua semina ya waagizaji wa mafuta
iliyofanyika jana, jijini hapa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Charles Mwijage alisema wizara yake kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati, Maji na Mafuta (Ewura) itazingatia ubora wa bidhaa na gharama
nafuu za uagizaji wa mafuta.
Mwijage aliongeza kuwa sasa ni wakati ambao
waagizaji wanahitaji kwenda kwenye mfumo wa kuwa na mlipaji mmoja wa
mafuta yanayoagizwa, tofauti na mfumo uliopo sasa wa kuagiza pamoja
lakini kila mmoja analipa peke yake.
“Pia, itaondoa usumbufu kwao kuanza kumfuatilia
mfanyabiashara mmoja mmoja,” alisema Mwijage na kuipongeza Benki ya FNB
kwa kudhamini semina hiyo muhimu.
Aliwataka wadau waliohudhuria semina hiyo kuanza
pia kusomesha wataalamu wazawa ili waweze kufanya kazi katika sekta ya
gesi na mafuta.
Alisema Watanzania watatakiwa kujaza nafasi za kazi zinazopatikana nchini na siyo watu wa nje.
“... inahitaji mafunzo ili kuinua uelewa wa watu juu ya suala la kuomba mikopo na dhamana,” alisisitiza Waziri Mwijage.
Meneja Mkuu wa Umoja wa Waagizaji wa Mafuta nchini
(PIC), Michael Mjinja alisema semina hiyo inalenga kuwaleta pamoja
waagizaji wote wa mafuta zaidi ya 40 ili kuangalia uwezekano wa kulipa
kwa pamoja.
Aliongeza kuwa sekta ya mafuta ni sekta ambayo ina watumiaji wengi hivyo wanajaribu kuweka nguvu zaidi ili wadhaminiwe na benki.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa FNB, Dave Aitken
alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa
benki hiyo, ajenda yao imekuwa ni kusaidia watu kwa kuwajengea uwezo.
Alisema benki hiyo ambayo ndiyo pekee Afrika
inayofanya kazi India, imeanzisha warsha ya kutoa mafunzo kwa waagizaji
wa mafuta kwa sababu ndiyo wadau wao muhimu.
Aliwataka wadau wa mafuta kushirikiana na benki yake katika kutengeza fursa.