Ni simanzi na vilio mazishi ya wanafamilia sita Dar
Ndugu wakimbeba Mwajuma Issa ambaye ni mama wa watoto wawili, Celine na Pauline Emmanuel waliofariki dunia katika ajali ya moto waliozikwa katika Makaburi ya Airwing Ukonga, Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam. Huzuni, simanzi na majonzi
jana vilitawala maeneo ya Kipunguni A na baadaye kwenye Makaburi ya
Airwing Ukonga, Ilala wakati miili ya watu sita waliofariki dunia kwa
kuungua moto Jumamosi alfajiri ilipozikwa.
Shughuli
zilisimama kwa muda katika maeneo hayo kati ya saa saba na nane mchana
wakati msafara mkubwa wa waombolezaji ulipokuwa ukielekea makaburini.
Wananchi
wengi waliokuwapo katika maeneo ambayo msafara huo ulipita, waliacha
kwa muda shughuli zao na kujongea pembeni mwa barabara kushuhudia umati
wa watu waliokuwa katika magari, pikipiki, baiskeli na wengine
wakitembea kwa miguu wakielekea makaburini katika mazishi ya watu sita;
Kapteni mstaafu, David Mpilla, mkewe Celina, mtoto wao Lucas, Shemeji wa
Mpilla, Samwel Yegeya na wajukuu wa Mpilla Paulina na Celina Emmanuel.
Katika
tukio hilo la Jumamosi, ni mtu mmoja pekee, Emmanuel Mpilla wa familia
hiyo alinusurika kwani wakati moto huo ulipoteketeza nyumba yao
hakuwapo.
Waombolezaji walianza kuwasili Kipunguni A
kuanzia saa tatu asubuhi. Ilipotimu saa tano asubuhi, idadi yao
iliongezeka kiasi cha wengine kukosa mahali pa kukaa na kuwafanya
waratibu wa mazishi hayo kuwataka waanze kuelekea eneo la makaburi.
Miili
ya marehemu iliondolewa nyumbani saa 7.20 mchana kwa gari la Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Wakati inapakiwa kwenye gari hilo, vilio na
simanzi vilitawala huku baadhi ya waombolezaji, wengi wao wakiwa kina
mama, waligaragara na kulia kwa uchungu.
Hali ilivyokuwa
Kutokana na umati wa waombolezaji, ilipotimu saa 9.20 alasiri, askari wa JWTZ, walifunga barabara inayoelekea eneo la makaburi.
Baada
ya miili hiyo kufikishwa makaburini, askari wa JWTZ waliipanga kwenye
meza maalumu zilizokuwa zimepambwa kwa maua na picha za marehemu hao
zikiwa mbele ya majeneza yao tayari kuanza kwa ibada ya mazishi
iliyoongozwa na Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigirwa.
Askofu Nzigirwa, aliwaongoza waombolezaji
akiwamo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kuaga miili hiyo ambayo,
tofauti na ilivyo kawaida kwa waumini wa Dini ya Kikristo, majeneza yao
hayakufunguliwa kutokana na miili ya marehemu kuharibika.
Katika
tukio hilo la kuaga, baadhi ya waombolezaji walipoteza fahamu kutokana
na uchungu hasa walipopita mbele ya majeneza yaliyokuwa na picha ya
watoto Celina na Paulina wakiwa wamekumbatiana huku wakitabasamu enzi za
uhali wao.
Miongoni mwa waliopoteza fahamu ni mama wa watoto hao, Mwajuma Issa.
Kiungo chapelekwa makaburini
Katika
tukio lisilo la kawaida, moja ya kiungo kinachoaminika kuwa cha Kapteni
Mpilla kilikutwa katika chumba chake, kiliwekwa kwenye jeneza lake
ambalo tayari lilikuwa limeshaingizwa kaburini. Awali, kiungo hicho
hakikuwa kimegundulika wakati miili ya marehemu hao ilipokuwa
ikikusanywa.
Wakusanya viongozi
Mazishi
ya marehemu hao ambao ni ndugu wa karibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya waliozikwa kuanzia saa 10.30
jioni yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
Mbali
na Dk Bilal, viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira,
Dk Makongoro Mahanga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki,
Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani, Mkuu wa Wilaya Ilala, Raymond
Mushi, Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Dar es
Salaam, Ramadhani Madabida na Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Mabere
Marando.
Akizungumza katika mazishi hayo, Dk Bilal
alisema: “Tumesikitishwa na vifo vya watu hawa kwa wakati mmoja.
Tunawapa pole wafiwa na tunawaomba wastahimili katika kipindi hiki
kigumu,” aliongeza: “Wakati umefika sasa watu kubadili mfumo wa ujenzi
wa madirisha ya nondo. Tunafahamu kuwa watu wanajilinda, lakini usalama
wetu wengi uko shakani hasa inapotokea dharura.”
Simulizi za majirani
Majirani
walileza jinsi walivyojitahidi bila mafanikio kuwaokoa na badala yake
wakaishia kusikiliza sauti za vilio vya uchungu wa maumivu makali ya
moto kisha vishindo vya kupasuka vichwa.
Mmoja wa majirani hao, Lusajo Mwaipopo alifika katika nyumba ya marehemu baada ya kusikia sauti ya vilio wakiomba msaada.
Alisema
alipofika eneo hilo alikuta moto ukiwa tayari umetanda katika sebule ya
nyumba hiyo. Anasema walianza kushauriana jinsi ya kutoa msaada hasa
namna ya kuuzima moto huo.
“Nilipata wazo la kujaribu
kuwashawishi wenzangu kutafuta sururu ili kuvunja. Tukapata mbili,
nikachukua moja na kuanza kuvunja kwenye kona ya dirisha nilifanikiwa
kutoboa lakini ghafla moto ulizuka kwenye tundu nikaogopa na kutimua
mbio,” alisema Mwaipopo.
Alisema hilo ni tukio baya
kulishuhudia katika maisha yake na inawaumiza karibu majirani wote
walioshuhudia hasa kutokana na vishindo vya kupasuka kwa vichwa.
Wasifu wa baba, mama
Akizungumza
katika mazishi hayo, Brigedia Jenerali Honoratus Lyamba alisema
marehemu Mpilla alikuwa mtumishi mwaminifu wa JWTZ Kikosi cha Anga hadi
alipostaafu 1994.
Mkurugenzi wa Swissport, Gaudence
Temu alisema mke wa Kapteni Mpilla, marehemu Celina ambaye alikuwa
mtumishi wa kampuni hiyo kabla ya kustaafu mwaka 2007, alikuwa mtumishi
mwadilifu.
Vifo vya ghafla
Jirani
mwingine, Christina Jabir alieleza kwamba mwaka 1989 familia hiyo
ilipatwa na msiba mkubwa wa ghafla baada ya mtoto wao wa kwanza kufariki
dunia kwa kugongwa na basi.
“Nakumbuka alikuwa anaitwa
Kabuta, aligongwa na kufa papohapo alipokuwa akivuka barabara katika
eneo la Banana, akitoka kanisani Ukonga,” alisema.
“Wakati
wa msiba ule mama yake alituambia kwamba siku hiyo mwanaye alimlilia
asubuhi akitaka waende wote kazini lakini alimbembeleza aende kanisani,
huku akishangazwa na hali hiyo maana hakuwahi kumlilia (kutaka waende
wote kazini),” alisema Jabir.
Mzazi atoa ya moyoni
Mama
mzazi wa marehemu Kapteni Mpilla, Felister Lonjini Masanja alisema sasa
amebakiwa na mtoto mmoja baada ya wengine wanne kufariki dunia. Mama
huyo aliyekuwa na watoto wote wa kiume, alisema sasa amebakiwa na mtoto
wake mkubwa.
Alisema kifo cha moto ni kibaya kwa sababu humkuta mtu huku akifahamu kuwa kifo chake kinakuja.
Alisema anamhurumia mjukuu wake, Emmanuel ambaye amebaki peke yake katika familia ya baba yake.