Dk Hoseah akiri Takukuru ‘kunuka’ rushwa
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, Dk Edward Hosea.
Kigoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
imekiri kuwapo kwa baadhi ya watumishi wake wanaojihusisha na vitendo
vya kupokea rushwa, hivyo kuchafua sifa ya taasisi hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Kigoma jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,
Dk Edward Hoseah alisema tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na taasisi
zilizofanya utafiti juu ya masuala ya rushwa nchini, baadhi yake zina
ukweli.
Dk Hoseah alisema wanapokea utafiti huo kama
changamoto na watatumia sheria, kanuni na taratibu kuwapa adhabu
watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Takukuru
siyo malaika, iwapo nitasema hakuna kabisa rushwa ndani ya taasisi hii
nitakuwa ninajidanganya kwani hili tatizo lipo sehemu zote, inawezekana
maofisa wasio waadilifu wanapokea rushwa lakini ninawahakikishia kwamba
tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika,” alisema Dk Hoseah
na kuongeza:
“Serikali imefanya jitihada kubwa
kuhakikisha Takukuru inaboreshwa, ndiyo maana bado sielewi kwanini kuna
baadhi ya watumishi wanalalamikiwa kujihusisha na ulaji rushwa,
wanalipwa vizuri na kuna mazingira mazuri ya kufanya kazi. Nitafanya
jitihada kuondoa changamoto hizi.”
Pia, alitoa
tahadhari kwa wananchi kuwa makini na matapeli wanaojitangaza kwamba wao
ni maofisa wa Takukuru, hivyo kuomba rushwa kwa baadhi ya maofisa wa
Serikali na watu wengine ambao wanabainika kufanya makosa yanayohusiana
na ubadhirifu mbalimbali.
Dk Hoseah alisema ili
kupambana na rushwa lazima Serikali iwe na uongozi bora na imara,
ambao utasaidia kuweka mipango thabiti kwa maendeleo ya wananchi,
kufanya mambo kwa uwazi, kuwajibika kwa umma, kuwashirikisha watu katika
mipango mbalimbali na kusimamia utawala wa kisheria.