Dk Kone akemea mila potofu
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk
Paseko Kone amewaonya wale wote wanaokosoa uumbaji wa Mungu kwa
kisingizio cha kutekeleza mila na desturi za makabila yao.
Hayo
aliyasema hivi karibuni mkoani Singida katika kongamano la kitaifa la
kupiga vita mila potofu ya ukeketaji lililoandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa kushirikiana na
Shirika la Kimataifa Linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).
Alisema
Mungu alipomuumba mwanamke na mwanaume alikuwa na makusudi yake,
kitendo kinachofanywa na baadhi ya makabila kuwakeketa wanawake kwa
kisingizio cha kutaka kuwaondolea hamu ya kufanya tendo la ndoa ni sawa
na kukosoa uumbaji wake.
“Mungu alikiweka kiungo hicho
kwa makusudi yake, inakuwaje sisi binadamu tunaamua kukwangua na
kukiondoa kwasababu za kibinadamu,” alihoji.
Hata
hivyo, alisema imefika wakati kwa wadau wanaoendelea kutoa elimu dhidi
ya mila hiyo kuwaeleza wote wanaotekeleza mila hiyo hoja za kiimani.
“Lazima
tutumie hoja zitakazomuingia mtu kiimani, tutafute maneno
yatakayowagusa katika imani zao yatakayowafanya waachane na vitendo
hivyo, tusimkosoe Mungu kwa kisingizio cha kutekeleza mila,” alisema Dk
Kone.