Makada CCM wamvaa JK
Aliyekuwa Mwenyekitiwa CCM Mkoawa Dar es Salaam John, Guninita akizungumza na wandishi wahabari, Dar es Salaam jana kuhusiana na kutaka kumshitaki Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Makada wawili wa CCM wamemuomba Rais Jakaya
Kikwete kuhakikisha kabla ya Uchaguzi Mkuu, anaondoa makundi ndani ya
chama hicho, ambacho kinakabiliwa na kazi ngumu ya kumpata mgombea wake
bila ya kutokea mpasuko.
Kauli hiyo, ilitolewa jana na
wenyekiti wa wa zamani wa chama hicho wa Dar es Salaam, John Guninita na
Mgana Msindai wa Singida walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu
mambo mbalimbali ya kisiasa.
Wenyeviti hao wa zamani
walitishia kumpeleka mahakamani mkuu mpya wa Wilaya ya Kinondoni, Paul
Makonda kwa madai kuwa amekuwa akiwadhalilisha kwa kuwaita vibaraka wa
kada mwingine wa CCM, Edward Lowassa katika mikutano yake na waandishi
wa habari.
Tayari wameshamuandikia barua ya kusudio la
kumfungulia mashtaka iwapo hataomba radhi kwa vitendo hivyo, lakini
Makonda aliwajibu kuwa alitoa maneno hayo kwa niaba ya chama na kwamba
aliyetakiwa kufungua kesi ni Lowassa.
Jana kwenye
mkutano na waandishi wa habari, Guninita, ambaye alisema mwenyekiti
mwenzake alikuwa na udhuru, alidai kuwa katika kipindi cha hivi karibuni
chama hicho kimekumbwa na changamoto ambazo zinatakiwa kutafutiwa
ufumbuzi haraka kutokana na baadhi ya viongozi kutokuwa na uchungu na
kutotetea chama hicho kwa ajili ya kukijenga.
“Mwenyekiti
wa chama, Rais Kikwete kwa kutumia uzoefu anaoufanya wa kutafuta
maridhiano katika nchi mbalimbali za Afrika, atumie uzoefu huo kuondoa
mpasuko ndani ya chama chetu,” alisema Guninita.
“Hivi
sasa chama kinapotea, kila mtu anafanya anavyotaka. Chama cha miaka ya
nyuma si cha sasa, viongozi tulikuwa tukiandika barua za malalamiko na
yalikuwa yanashughulikiwa, lakini hivi sasa hata ukiandika hakuna
anayekusikiliza wala kukujibu.”
Hata hivyo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo haikupatikana.
Akizungumzia kukashifiwa kwao na makonda, ambaye pia ni
katibu wa hamasa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Guninita alisema:
“Licha ya kumtaka atuombe radhi, amekataa sasa tumepanga kwenda
mahakamani.
“Mimi siwezi kutukanwa na kijana mdogo,
nimekuwa mkuu wa wilaya miaka 25 iliyopita, nimekuwa mwenyekiti wa UVCCM
kwa miaka kumi... UVCCM ni sehemu ya kuwapika vijana kuja kuwa
viongozi, lakini sasa imekuwa sehemu ya kuzalisha watu wanaopiga
viongozi.”
“Taratibu za kuwasiliana na mawakili wangu
zimekamilika na Jumatatu tunatarajia kwenda mahakamani kwani
alichotufanyia Makonda hatuwezi kukiacha hivi hivi,” aliongeza
Guninita
alisema: “Eti Makonda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, Rais ana uhuru wa
kuteua lakini hapa niseme tu kuwa wanaomshauri walikosea kabisa kama
mtu anateuliwa kwa kumpiga mtu tena kiongozi mkubwa serikali iliyopita
ni jambo la hatari.”
Makonda alionekana kumfanyia fujo
mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba katika kongamano la kujadili Katiba Inayopendekezwa
lililofanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es salaam.
Hata
hivyo, Makonda alipoulizwa kuhusu uamuzi wa makada hao alisema: “Siwezi
kuzungumzia kitu ambacho hakinihusu. Mimi niulizie wananchi wa Dar es
Salaam wanapataje maji, migogoro ya ardhi inakwisha vipi na matatizo ya
machinga yatakwisha vipi.”
Aliongeza kusema: “Hata
kesho (leo) nitakuwa na ziara ya kutembelea ujenzi wa maabara kwa shule
mbili hivi maeneo ya Manzese kwani unaweza kusema ujenzi umekamilika
kumbe bado.”
Mwaka jana, Makonda aliwatuhumu makada hao
kuwa ni wahaini, waongo na wazandiki na kusema kama nia yao ni kusaka
urais kwa ajili ya mtu fulani basi watambue kuwa mtu huyo amekosa sifa
za katika uchaguzi mkuu wa mwakani.