Mwenyekiti UVCCM kizimbani kwa kumtwanga makonde katibu wake
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa Hamis Juma. Picha ya Maktaba
Misungwi. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Mansoor Mohamed
(25) amefikishwa Mahakama ya Wilaya kwa tuhuma za shambulio la kudhuru
mwili.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Eliasha Kisura
alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Februari 10 saa 7:00 mchana kwa
kumshambulia kwa mateke na ngumi Katibu wa UVCCM Wilaya, Nassoro
Mohamed kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka,
mshtakiwa alikanusha na Hakimu Mfawidhi, Godfrey Mwambapa aliahirisha
kesi hiyo hadi Februari 25 itakapoanza kusikilizwa.
Mshtakiwa
aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini
wawili wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya Sh700,000.
Chanzo cha ugomvi
Chanzo
cha ugomvi inadaiwa ni kambi za ubunge ndani ya UVCCM wilayani humo,
hali inayoonyesha Mwenyekiti wa umoja huo, Mansoor Mohamed kutofautina
na Katibu wake, Mohamed Nassoro.
Mohamed inadaiwa alishtukia kikao cha makatibu wa vijana ambacho kiliitishwa na Nassoro bila kumtaarifu yeye kama mwenyekiti.
Inadaiwa
Mohamed alivamia kikao hicho cha makatibu wa kata wilayani hapa,
kilichokuwa kinafanyika Ukumbi wa CCM na baada ya kumhoji katibu wake
sababu za kuitisha kikao bila kumpa taarifa, walianza kurushiana maneno
makali na kuanza kupigana.
Akizungumza kwa simu jana
baada ya tukio hilo, Mohamed alisema alipata taarifa za kikao hicho
kutoka kwa wajumbe, hivyo akalazimika kwenda ukumbini kujua sababu za
katibu wake kushindwa kumpa taarifa.
“Nimepokea ujumbe
wa simu kutoka kwa makatibu wa UVCCM kuwa kuna kikao, mimi sina taarifa
yoyote nilikwenda kufahamu sababu za kunificha taarifa hizo,” alisema
Mohamed.
Mohamed alisema kinachoendelea ni suala la
makambi ya wagombe ubunge kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba, kwani akiwa
kiongozi wa UVCCM hawezi kukubali kuona kanuni na taratibu zikikiukwa
wilayani kwake akanyamaza.