Pinda ashukiwa ndani na nje ya Bunge
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Dar es Salaam. Kauli ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kuwa wanafunzi walioshiriki gwaride na halaiki kwenye
sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea ni watoto wa wanachama wa chama
hicho, imekosolewa na wananchi na wabunge ambao walifikia uamuzi wa
kuomba mwongozo.
Sherehe hizo zilifanyika Jumapili ya
Februari Mosi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, zikishirikisha
makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
ambao walivalia sare za CCM na kuimba nyimbo za chama hicho huku
wakicheza gwaride na halaiki, ambayo kwa kawaida huchukua muda mrefu
kujifunza na kuielewa.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu (Chadema), Susan Lyimo, mtendaji huyo mkuu wa Serikali alitetea
ushiriki wa watoto hao wapatao 500 kwenye sherehe hizo akisema ni sehemu
ya mfumo wa wanachama wa CCM.
“Susan, utafikiri
tulikuwa pamoja. Nilijua tu swali hili lazima litaulizwa. Ila ‘mtoto wa
nyoka ni nyoka’. Chama hiki kina mfumo wake ambao umeshuka mpaka kwenye
ngazi ya kitu kinaitwa chipukizi,” alisema akijibu swali la mbunge huyo
aliyetaka kujua sababu za CCM kutumia watoto kwenye shughuli zake za
siasa wakati ina wanachama wapatao milioni 10 kote nchini.
“Chipukizi
hawa ni watoto ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana-CCM, ndiyo
maana chama kiliwatumia. Sherehe ilikuwa nzuri na ilipendeza sana. Kwa
kuwa hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, halina madhara
lile rafiki yangu, pia bado ni wadogo mno na walikuwa wanafurahia
gwaride na kuvaa sare tu.”
Lyimo hakuridhishwa na jibu
hilo la Waziri Pinda, akisema hakutakiwa kutoa majibu ya aina hiyo na
kwamba katika mkusanyiko huo, kulikuwa na watoto ambao wazazi wao siyo
wanachama wa CCM.
“Lengo la watoto hawa ni kusoma na
siyo kufanya siasa. Iweje mfanye mambo kwa double standard
(ndumilakuwili)?” alihoji na baadaye Pinda alitaka suala hilo
lisiendelee kujadiliwa.
“Naheshimu maelezo ya Susan,
lakini kiacheni chama kiendelee na utaratibu wake. Mfumo wake ndiyo huo,
ndivyo ulivyo na sidhani kama kuna haja ya kuendelea kubishana katika
suala hili,” alisema Pinda ambaye ofisi yake inasimamia elimu ya msingi
na sekondari.
Kabla ya nchi kuruhusu tena siasa za
vyama vingi mwaka 1992, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
walikuwa wakitumiwa kwenye shughuli za chama tawala na za Serikali,
lakini imekuwa ni nadra kuonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu uhuru
wa kidemokrasia ulipoanza.
Hata hivyo, ili kufanikisha
sherehe hizo za CCM ambazo zilifanyika Jumapili kutokana na siku ya
kuzaliwa chama hicho (Februari 5) kuwa katikati ya wiki, maofisa wa
elimu ya sekondari wa Manispaa ya Songea walielezwa kuwaandikia barua
wakuu wa shule zilizopo karibu na Uwanja wa Majimaji, wakiwataka
kuhudhuria pamoja na walimu na wanafunzi ambao waliagizwa kuvaa sare.
Mkosamali aomba mwongoza
Majibu
hayo hayakuwaridhisha wabunge wengine na baada ya kipindi cha maswali
ya papo kwa papo, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali
aliomba mwongozo wa Spika juu ya suala hilo.
Mkosamali
alisema kitendo cha kuwatumia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
katika sherehe hizo ni sawa na kuwalazimisha kukishabikia chama ambacho
hawakipendi.
“Kuna barua zinaonyesha jinsi wanafunzi
walivyolazimishwa kuvaa sare za chama na kuhudhuria sherehe hizo. Jambo
hili siyo sawa kwa sababu linawalazimisha wanafunzi kuwa wanachama wa
chama ambacho hawakipendi,” alisema Mkosamali.
Spika Makinda alisema kuwa suala hilo lingetolewa ufafanuzi baadaye.
Wanasiasa, wasomi wazungumza
Baadhi ya wasomi walipinga kauli hiyo ya Waziri Mkuu kuhusu matumizi ya watoto kwenye shughuli za kisiasa.
Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima alisema
wanafunzi wanatakiwa kufundishwa uzalendo, tunu za taifa na historia ya
nchi yao, lakini siyo itikadi za vyama vya siasa.
“Sasa
tupo kwenye mfumo wa vyama vingi. Tulishaachana na mfumo wa chama
kimoja ambao vijana waliandaliwa kukielewa chama tawala tangu wakiwa
wadogo,” alisema na kuongeza:
“Tunapaswa kujiuliza na
vyama vingine vikifanya kama hiki kilichofanywa na CCM hali itakuwaje?
Kilichofanywa na CCM ni makosa kwa sababu hata mzazi hutakiwi
kumchagulia mtoto chama cha kukipenda. Mzazi anamrithisha mtoto mila na
dini tu.”
Alisema ushirikishwaji wa wanafunzi katika
masuala kama hayo ndiyo chanzo cha watoto wadogo kuanza kutumika vibaya,
akitoa mfano wa watoto wanaopigana vita Sudan.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Chris Peter Maina naye
alitofautiana na maelezo ya Pinda akisema: “Si sahihi. Wanafunzi
wanatakiwa kushiriki shughuli za kitaifa kama sherehe za uhuru au
kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere. Kuwaingiza katika masuala
ya kisiasa mapema kiasi hiki ni hatari.”
Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema inashangaza kuona kwamba hadi leo
CCM wanadhani shule zote ni za chama hicho ndiyo maana wakaamuru walimu
za wanafunzi kushiriki.
“Watoto wanatakiwa kufundishwa
uraia na kusoma historia ya nchi yao na vyama vya siasa lakini siyo
kuwashinikiza kukishabikia chama chochote. Hii inaonyesha wazi kuwa bado
wenzetu wanadhani tupo katika mfumo wa chama kimoja cha siasa na ndiyo
maana wanatumia vyombo vya dola kudhibiti karibu kila jambo linalofanywa
na vyama vya upinzani.
“Kitendo kilichofanywa na CCM
ni kuingilia haki ya watoto. Wanafunzi hawa wanatakiwa kuachwa wasome na
kujichagulia mambo yao wenyewe.”
Makamu Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, Leticia Ghati alisema: “Kitendo walichokifanya si sahihi.
Wanafunzi ni wa watu wote na huwezi kusema kuwa wote walioshiriki katika
sherehe hizo ni watoto wa makada wa chama chao. Huu si mfumo mzuri wa
utawala bora.”