HII KALI YA MWAKA 2015,-Mzungu akamatwa na fuvu la binadamu
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
Dar es Salaam. Matukio ya wasafiri kukamatwa Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa na nyara za Serikali na
dawa za kulevya, yanazidi kuchukua sura mpya baada ya raia mmoja wa
Ubelgiji kukamatwa akiwa na fuvu la binadamu.
Raia
huyo, Balcjan Christine Weejktgns (49), alikamatwa Jumatatu saa 2.30
usiku wakati akiwa katika taratibu za kuingia uwanjani hapo tayari kwa
safari ya kuelekea Ubelgiji kupitia Zurich, Uswisi.
Tukio
la kukamatwa kwa Mbelgiji huyo ni mwendelezo wa matukio ya aina yake
uwanjani hapo baada ya watu wengine wawili kukamatwa kwa nyakati tofauti
kwenye uwanja huo wakiwa na kucha za simba na kenge walio hai.
Kamanda
wa Polisi Viwanja vya Ndege, Hamisi Selemani alisema mtu huyo alikutwa
ameficha fuvu hilo la binadamu kwenye mfuko wa plastiki.
“Alivyopita
kwenye mashine za ukaguzi tulimtilia shaka na tulipompekua tulimkuta
amebeba fuvu la kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa
plastiki ndani ya sanduku alimokuwa ameweka nguo zake na vitu
mbalimbali,” alisema Selemani.
Raia huyo anadaiwa kuwa
ni mkazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) mkoani Morogoro na inadaiwa kuwa
alikuwa nchini kwa ajili ya kufanya utafiti.
Kamanda
Selemani alisema baada ya askari wa kikosi cha polisi cha JNIA kumhoji
kwa undani madhumuni ya kubeba fuvu, alisema ni mali yake na kuwa
alikuja nalo nchini kutoka Ubelgiji.
“Kwa maelezo yake
alidai kuwa fuvu hilo analimiliki muda mrefu tangu alipoingia nchini
mwaka 2000 akitokea Ubelgiji akidai kuwa yeye ni mtafiti,” alisema.
Pamoja
na raia huyo wa Ubelgiji kujitetea kuwa ni mtafiti, Kamanda Selemani
alisema sheria za nchi haziruhusu mtu kumiliki viungo vya binadamu hivyo
anayekiuka lazima akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Jeshi
la polisi haliwezi kuona taratibu za nchi zikivunjwa hata kama ni raia
wa kutoka nje ya nchi ambaye amekuja kufanya utafiti nchini. Lazima
afuate sheria,” alisema na kuongeza:
“Wito wangu ni
kwamba watu wote wanatakiwa kufuata taratibu za nchi. Huyu raia ameona
kitu cha kawaida kuishi na fuvu la kichwa, lakini hapa ni tofauti na
nchini kwao,” alisema.
Alisema polisi inaendelea na
upelelezi ili kujua sababu ya Mbelgiji huyo kusafirisha fuvu hilo na
kuahidi kuwa uchunguzi ukikamilika, atafikishwa mahakamani.
Pamoja
na kuwa tukio hilo ni la aina yake, si geni kwenye uwanja huo ambao una
historia ya upitishaji wa vitu mbalimbali kinyume cha sheria.
Januari
7, Polisi wa JNIA walimkamata raia wa Kuwait akiwa na viumbe hai aina
ya kenge 149 wenye thamani ya Sh6.3 milioni ambao walikuwa
wakisafirishwa kwenda Kuwait.
Agosti mwaka jana, Raia
wa Vietnam, Dong Van (47), alikamatwa uwanjani hapo akiwa na meno 65 na
kucha 447 za simba zenye thamani ya Sh189.4 milioni.
Van alikamatwa akijiandaa kwa safari ya kuelekea Vietnam kwa kutumia ndege ya Shirika la Qatar kupitia Doha.
Raia
huyo alikamatwa na nyara hizo akiwa amepakia katika begi lake la nguo
huku zikiwa zimefungwa vizuri katika pakiti za mchele na kahawa. Baada
ya kupita kwenye mashine za ukaguzi ilibainika kuwa begi hilo lilikuwa
na pakiti 22, kati ya hizo saba zilikuwa na meno pamoja na kucha za
simba.