Pumzi ya mwisho Lowassa, Membe
Mwenyekiti
wa CCM, Jakaya Kikwete akipiga makofi wakati alipowasili katika mkutano
wa chama hicho Mjini Dodoma hivi karibuni. Picha ya Maktaba,
Dar es Salaam. Wakati makada wa CCM wakivuta pumzi ya mwisho
kwa matarajio ya kuondolewa kifungo cha miezi 12 ili wajitose rasmi
kuwania urais, Kamati Kuu ya chama hicho inakutana leo kukiwa na habari
kuwa itatumia muda mwingi kujadili mwelekeo wa mchakato wa Kura ya Maoni
na badala wa wanachama hao sita.
Adhabu ya makada sita
wa CCM ya kufungiwa miezi 12 ilishaisha tangu kastikati ya mwezi huu na
sasa wanasubiri kwa hamu tangazo la Kamati Kuu la kumalizika kwa adhabu
yao ili wawe huru kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama
hicho na kuendelea na shughuli nyingine za kujiandalia mazingira ya
kupitishwa na Halmashauri Kuu.
Makada hao ni Bernard
Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, ambao waliwahi kuwa mawaziri wakuu,
William Ngeleja, Steven Wasira, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula,
na January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.
Hadi
sasa makada hao, ambao walituhumiwa kuanza harakati za kampeni kabla ya
muda, hawajatangaza rasmi nia ya kuwania urais na habari zinasema kuwa
wamekuwa kwenye maandalizi ya kufanya hafla kubwa ya kutangaza mpango
huo.
Lakini habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema
kuwa kuna uwezekano mdogo wa Kamati Kuu kuzungumzia suala hilo kwa kuwa
kikao hicho kitajikita zaidi kuzungumzia mwenendo wa mchakato wa Kura ya
Maoni ambao unaonekana kuyumba.
“Watu wameandika sana
kuhusu Kamati kufanya uamuzi wa wagombea urais waliofungiwa, lakini
nakuhakikishia suala hilo halitazungumzwa labda iweje sijui,” alisema
mpashaji habari wetu aliye ndani ya chama hicho.
“Suala linalosumbua kwa sasa ni Kura ya Maoni na hilo ndilo litachukua muda mwingi.”
Alisema
kamati Kuu itatoa mwelekeo wa Kura ya Maoni, ambayo mchakato wake
unapingwa vikali na vyama vya upinzani ambavyo vinasema uchache wa
vifaa, muda mdogo wa maandalizi, watendaji na matumizi ya teknolojia ya
uchukuaji wa taarifa za wapigakura kuwa vinaweza kfanya kazi ya
uandikishaji kuchukua muda mrefu na hivyo Kura ya Maoni isipigwe Aprili
30 kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kada
mwingine wa chama hicho pia aliidokeza Mwananchi kuwa wagombea hao
waliofungiwa watabidi kuvuta pumzi zaidi kabla ya kuachiwa huru rasmi.
Mmoja
wa wasaidizi wa kada aliyefungiwa alipoulizwa kuhusu mipango ya bosi
wake kutangaza rasmi kugombea, alisema: “Sisi tunaisubiri Kamati Kuu tu.
Ikitangaza kumalizika kwa adhabu tu, hata wiki ijayo tutatangaza
rasmi.”
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho cha leo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuzungumzia ajenda.
Hivi
karibuni, Nape alithibitisha kuwa muda wa adhabu hiyo ulikuwa ukingoni
na kuwa viongozi hao sita wangefanyiwa tathmini na kamati ndogo ya
maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa ipasavyo.
Kikao
hicho kinafanyika wakati upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho ukiwa
haujatulia na ikionekana wazi kuwa makada waliofungiwa wameanza kupoteza
uvumilivu na sasa wafuasi na mashabiki wao wanajitokeza waziwazi
kutangaza misimamo yao kwa mtu wanayeona anafaa kuteuliwa na chama hicho
kugombea urais.
Hivi karibuni, Dk Raphael Chegeni
aliiambia Mwananchi kuwa ametumwa na wanachama wa CCM kutoka Kanda ya
Ziwa kwenda kumshawishi Lowassa ajitokeze kuwania urais, ikiwa ni
kuitikia wito wa Rais Kikwete ambaye aliwataka wana-CCM kuwashawishi
watu wanaowaona wanafaa kugombea nafasi hiyo kubwa nchini.
Habari
hiyo pia iliambatana na taarifa kuwa baadhi ya wafuasi wa mbunge huyo
wa Monduli walienda kuangalia uwezo wa kutumia Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid mjini Arusha kwa ajili ya hafla ya kutangaza nia.
Hata hivyo, zikiwa zimesalia siku chache kabla ya
harakati za kugombea urais na ubunge kuanza na ukweli kwamba wanachama
wengine wanaendelea kujinadi, Kamati Kuu inaweza kutoa msimamo kuhusu
adhabu za makada hao.
Kikao hicho kitakachoongozwa na
mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ni cha pili kufanyika mwaka huu.
Katika kikao cha kwanza kilichofanyika Kisiwandui, Zanzibar Januari 13,
kiliagiza adhabu kali zichukuliwe dhidi ya vigogo watakaobainika kukiuka
masharti ya adhabu ya mwaka mmoja waliyopewa ambayo ilimalizika
Februari 18.
Kikao hicho pia kiliahirisha kutoa ratiba
ya mchakato wa uchaguzi kwa chama hicho, ambayo hueleza tarehe ya kuanza
kuchukua fomu na kurudisha, muda wa kampeni, tarehe za vikao vya
kupitisha wagombea kwenye ngazi ya ubunge na urais na tarehe ya vikao
vya mwisho vya kitaifa kwa ajili ya kupitisha wagombea wa ngazi zote.
Kamati
ndogo ya Maadili inayoongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip
Mangula ndiyo iliyopewa jukumu la kufanya tathmini ya vigogo hao sita
kuona kama walitekeleza ipasavyo adhabu waliyopewa, kisha kupeleka
mapendekezo yake katika kikao cha Kamati Kuu.
Mbali na
vigogo hao, kamati hipo pia imeshamuhoji aliyekuwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge
kutokana na kuhusika katika sakata la uchotwaji fedha kutoka kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika mgawo huo wa Escrow,
Profesa Tibaijuka alipokea Sh1.6 bilioni, sawa na Chenge wakati Ngeleja
alipokea Sh40.4 milioni. Profesa Tibaijuka na Chenge wamefikishwa mbele
ya Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu tuma
hizo.
Chenge na Ngeleja wote ni wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), ambapo kwa mujibu wa mazimio ya Kamati Kuu
iliyokaa Zanzibar, makada hao pamoja na Tibaijuka ikiwa watakutwa na
hatia, suala hilo litafikishwa mbele ya Kikao cha leo na kupewa adhabu,
ikiwamo kuvuliwa nyadhifa zao ndani ya chama.
Hatma ya
vigogo hao imebaki mikononi wa kamati ya Mangula ikitegemea zaidi kile
ambacho makamu mwenyekiti huyo atakiwasilisha katika kikao hicho cha
Kamati Kuu.
Kamati Kuu inaundwa na mwenyekiti wa CCM,
makamu wake na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye ni Rais wa
Zanzibar. Wengine ni wajumbe 14 waliochaguliwa na Mkutano Mkuu, ambao ni
Stephen Wasira, Pindi Chana, Professa Tibaijuka, Jerry Slaa, Adam
Kimbisa, Dk Emmanuel Nchimbi na William Lukuvi kutoka Bara.
Wengine
ni Shamsi VuaiNahodha, Dk Hussein Mwinyi, Profesa Makame Mbalawa, Dk
Salim Ahmed Salim, Dk Maua Daftari, Hadija .H. Abuu na Samia Suluhu
Hassan kutoka Zanzibar.
Wakati huohuo, katibu Mkuu wa
CCM, Abdulahman Kinana kesho anaanza ziara ya siku tisahuku akitarajia
kukutana na kero ya ardhi wilayani Kondo.
Taarifa
iliyotolewa jana na katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Albert Mgumba,
Kinana atapelekwa maeneo ya Bahi, Mnemia na Itaswi ambayo yana migogoro
ya wakulima na wafugaji.
Ziara ya hiyo inaanzia Wilaya ya Mpwapwa kesho asubuhi na itaanzia jimbo la Mpwapwa kabla ya kwenda Kibakwe.
“Kila kitu kimekamilika na sina shaka. Katibu atafanya ziara kama alivyotarajia kwenye maeneo hayo,” alisema Mgumba.
Alitaja lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi na kuhimiza utekelezaji wa Ilani.