Mwanasheria Mkuu: Ripoti ya mabilioni ya Uswisi ipo tayari
Dar es Salaam. Kamati iliyoundwa na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), kuchunguza mabilioni ya fedha yaliyofichwa na
baadhi ya Watanzania katika benki mbalimbali nchini Uswisi, imekamilisha
uchunguzi na inasubiri kukabidhi ripoti ya kazi hiyo kwa Spika wa
Bunge.
Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari, Dar es Salaam.
Masaju alisema
kamati hiyo ilikamilisha kazi yake baada ya kuwahoji watu mbalimbali na
kukamilisha kazi hiyo kama walivyoagizwa na Bunge na kinachosubiriwa ni
kuikabidhi kwa chombo hicho cha kutunga sheria.
“Ofisi
yangu kupitia kamati iliyoundwa tulikwishamaliza kazi hii, lakini
hatuwezi kutoa taarifa kupitia sehemu nyingine zaidi ya ofisi
iliyotupatia kazi kama utaratibu unavyoelekeza.
“Sasa
wananchi na nyie waandishi wa habari msubiri taarifa hiyo itolewe kule
bungeni ambako tuhuma hizi zilianzia,” alisema Masaju.
Watuhumiwa
Vigogo
10 wametajwa kuhusika katika kashfa hiyo. Inadaiwa kuwa katika orodha
hiyo, yupo kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi
yao bado ni wabunge na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu
Tanzania (BoT).
Kamati ilivyoundwa
Kamati
hiyo maalumu iliundwa kwa Azimio la Bunge baada ya Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe kuibua tena tuhuma hizo bungeni mapema mwaka
jana, akidai kuna vigogo walioficha Sh323.4 bilioni katika benki
mbalimbali za Uswisi.
Kiasi hicho cha fedha kinaweza
kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 300 ambao ni sawa na
kutoka Morogoro hadi Iringa.
Kwa mara ya kwanza, tuhuma
hizo zilitolewa bungeni na Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), mwaka 2012.
Katika
kikao cha Tisa cha Bunge, Zitto aliwasilisha hoja binafsi kulitaka Bunge
kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania
aliowaita vigogo walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Kutokana
na hoja hiyo, Bunge chini ya Spika Anne Makinda, liliipa Serikali muda
wa mwaka mmoja ambao ulimalizika Oktoba mwaka jana iwe imekamilisha
uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake bungeni.
Wakati
sakata hilo lilipokuwa limepamba moto, Serikali ya Uswisi kupitia kwa
Balozi wake nchini, Olivier Chave iliwahi kusema Serikali ya Tanzania
haijaonyesha nia ya dhati kutaka kuchunguza na kurejesha mabilioni ya
fedha hizo.
Balozi Chave alikaririwa wakati huo akisema
hawajaona jitihada zozote zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kutaka
kuzipatia ufumbuzi tuhuma hizo.
Chave alisema nchi yake
iko tayari kushirikiana na Tanzania kujua uhalali wa fedha hizo na
endapo zitagundulika ni chafu watakuwa tayari kuzirejesha nchini.
Taarifa
kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonyesha kuwa baadhi ya fedha hizo
zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi
zilizopo nchini.
Hata hivyo, Machi mwaka jana ilielezwa
kuwa mabilioni ya shilingi yaliyowekwa na Watanzania katika benki za
Uswisi yalikuwa yameanza kuhamishwa kimyakimya.
Ripoti
ya Benki za Uswisi ya 2012 ilionyesha kuwa fedha zinazotoka Tanzania
zilipungua kwa karibu Sh36.4 bilioni ikilinganishwa na zilizokuwapo 2011
nchini humo, lakini haielezi sababu ya kupungua kwake.
Watanzania 99
Hivi
karibuni, Timu ya Wanahabari wa Kimataifa wanaoandika Habari za
Uchunguzi (ICIJ) ilitoa ripoti ikisema Watanzania 99 wanamiliki Dola za
Marekani 114 milioni (Sh193bilioni) kwenye akaunti za benki nchini
Uswisi.
Ripoti hiyo inayoitwa SwissLeaks iliyotolewa
Marekani, imesheheni taarifa za Benki ya HSBC ya Uswisi na namna watu
maarufu wakiwamo wanasiasa, wachezaji, viongozi wa dini na
wafanyabiashara walivyoficha mamilioni ya fedha na kufanikiwa kuzikwepa
mamlaka za mapato katika nchi zao.
Katika orodha hiyo,
Tanzania inashika nafasi ya 100 duniani na nafasi ya pili Afrika
Mashariki ikiwa nyuma ya Kenya inayoshika nafasi ya 58 duniani kwa
kuweka zaidi ya Sh950 bilioni nchini Uswisi.
Ingawa
taarifa hiyo haikutaja majina ya watu wote walioweka fedha Uswisi,
imemtaja mfanyabiashara Shailesh Vithlani ambaye anadaiwa kuwa dalali
wakati Tanzania iliponunua rada kutoka kwa kampuni ya BAE system kuwa ni
miongoni mwao.
Hivi karibuni, Waziri wa Fedha Saada
Mkuya alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akitahadharisha kwamba
si kila aliyeweka fedha Uswisi amezipata kwa njia haramu.