JE UNATAKA KUWA MJASIRIAMALI? Hii ndiyo silaha ya mjasiriamali katika kufikia mafanikio
Wahenga walisema: “Maisha ni kuona mbele.” Huu ni usemi
unaompa mjasiriamali matumaini ya kusonga mbele pasipo kutumia muda
mwingi kuwaza yale aliyokwishafanya.
Katika maisha ya
kila siku kwenye ujasiriamali, wajasiriamali wanakumbana na changamoto
nyingi. Changamoto hizi wakati mwingine huwasaidia kuona mbele na
hatimaye kuwa watu wenye mafanikio.
Kwa mfano, kama mtu
anajishughulisha na ujasiriamali halafu akawa anasumbuliwa na mamlaka
zinazohusika na urasimishaji wa biashara kwa sababu za kutorasimisha
shughuli zake, akiamua kurasimisha biashara yake atafanya shughuli zake
bila kubughudhiwa.
Mwisho wa siku atakua kibiashara,
hivyo kuchangia maendeleo ya nchi yake kwa kulipa kodi na kuajiri watu.
Kwa mjasiriamali wa aina hii hatakuwa na muda tena wa kuanza kuwaza yale
yaliyotokea bali atakuwa anaiona dunia yenye matumaini kesho yake.
Atakuwa
anafikiria zaidi juu ya siku za baadaye. Atakuwa na malengo ya
kuhakikisha anaibadili dunia na wala siyo kusubiri dunia imbadilishe. Ni
kwa sababu, akisubiri dunia imbadili, atakuwa miongoni mwa watu
wanaosubiri kutupwa kwenye shimo la sahau.
Hii ina
maana kuwa, mjasiriamali hatakiwi kukumbuka changamoto za jana kwa lengo
la kumpa huzuni na machungu yatakayomsababisha ashindwe kupiga hatua.
Bali anatakiwa kuchukulia changamoto hizo kama somo, ambalo litamwezesha
kufika anakoelekea pasipo kurudi katika hali yake ya jana, ambayo siyo
taswira nzuri katika kichwa chake.
Kama nilivyowahi
kusema katika makala zangu za mwaka jana, mwanzo ni mgumu. Leo narudia
tena kusema kuwa mwanzo ni mgumu. Mwanzo wa shughuli za ujasiriamali,
wakati mwingine utaona kama hakuna anayekujali.
Unaweza kuhangaika siku nzima na hata zaidi ya miezi
kadhaa pasipo kupata kile ulichokusudia. Wakati mwingine unaweza kuwa
unatafuta msaada fulani ili kukamilisha kile ulichokianzisha ukaambulia
patupu! Unaweza kuchekwa na baadhi ya watu, wakiwamo wale uliowategemea
kuwa wangekuunga mkono. Pia, unaweza kukutana na upinzani mkubwa kutoka
kwa wajasiriamali wenzako, hata kwa wivu wake kana kwamba unapigana
vita.
Hata hivyo, ukiamua kuona mbele utavuka vikwazo
hivi vyote na kupata kile ulichokusudia. Kuona mbele ni pamoja na kuwa
na dira au mweleko wa wapi unataka kuwa. Mjasiriamali mwenye dira huwa
hakati tamaa na haogopi vita kutoka kwa wenzake au kwa baadhi ya watu.
Ni mtu mwenye kuangalia ni njia zipi azitumie kufika pale anapotaka
kufika.
Ikumbukwe kuwa ushindi huja kwa mtu mwenye kupambana kwa malengo ya kuiona kesho yenye nuru ya mafanikio.
Ushindi
hupatikana na kujifunza kila hatua na njia anayoipita mjasiriamali ili
kufika kwa mafanikio pale anapopata. Ili kufanikisha hili, mbali ya kuwa
na maono, mjasiriamali anatakiwa kuwa mvumilivu na mwenye kuthubutu.
Uvumilivu
na uthubutu ni miongoni mwa vitu muhimu sana kwa mjasiriamali. Ni vitu
vinavyochangia suala zima la utekelezaji wa dira ya mjasiriamali, ambayo
siku zote huwa ni kuona mbele.
Watu wengi wameshindwa kufika popote kwa sababu ya kukosa uthubutu na uvumilivu wa kufanya yale wanayofikiria.
Kwa
mjasiriamali anayethubutu na kuvumilia, ataiona kesho yake yenye neema
na ambayo itamfaidisha yeye, jamii yake na Taifa kwa ujumla kwani
mwendapole hajikwai, akijikwaa hataanguka wala kushindwa kuendelea na
safari yake.-