Kuanguka kwa Mugabe kwageuzwa utani
Baada ya Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kuteleza na kuanguka
katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Harare, watu wengi duniani
wamechukulia kitendo cha kuanguka kwa rais huyo kama staili ya kutembea
wakiwa na lengo la kumdhihaki.
Katika nchi mbalimbali
za Afrika na Ulaya watu wamekuwa wakitembea kama vile wanataka kuanguka
wakimuigiza Rais Mugabe. Rais Mugabe ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu
mwaka 1980, alizaliwa Februari 21, 1924, ambapo mwezi huu atatimiza umri
wa miaka 91.
Picha mbalimbali kwenye mitandao ya
kijamii zinaonyesha Mugabe akishiriki shughuli mbalimbali, lakini kwa
stahili kama alivyoanguka uwanja wa ndege.
Kutokana na
picha zilizotengenezwa kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii,
rais huyo aliagiza picha hizo zifutwe kwakuwa hazina maana.
Baadhi
ya picha za Mugabe kwenye mitandao ya kijamii, zinaonekana akikimbizwa
na polisi, nyingine akiteleza kwenye barafu na akishangilia mchezo wa
kriketi uwanjani.
Picha zake kila mtu alizitumia kwa
namna alivyoona inafaa kwani watu wengine walizitengeneza na kuonyesha
kwamba anacheza muziki.
Moja ya picha iliyoonekana
kuwavutia watu wengi ni ile iliyotengenezwa na kuwekwa kwenye moja ya
picha Hussein Bolt akiwa anachomoka kwenye mbio za mita 100, huku akiwa
sambasamba na mkimbiaji huyo maarufu duniani.
Pia,
picha nyingine ambayo ilionekana kuwavuta watu wengi na kusambazwa
kwenye mitandao ya kijamii ni ile Mugabe anaonekana akikimbizwa na
kiboko katika moja ya mbuga za wanyama za Afrika.
Rais
huyo alianguka hivi karibuni kwenye uwanja huo wakati akirejea Zimbabwe
akitoka Ethiopia ambako alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika
(AU), akichukua nafasi ya Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz.
Mugabe alianguka kwa bahati mbaya wakati akijiandaa kuingia kwenye gari yake kuelekea Ikulu mjini Harare.
Baada ya kuanguka chini, rais huyo alisaidiwa na wasaidizi wake ambao walimuinua na kundelea na ratiba yake kama kawaida.
Kutokana
na tukio hilo, vyombo vya habari viliripoti kwamba, Ikulu ya nchi hiyo
iliwasimamisha kazi walinzi 27 wa Rais Mugabe, kwa kushindwa kuthibiti
tukio hilo.