Mtoto wa Sokoine ataka Jimbo la Lowassa
Namelock Sokoine.
Monduli. Viongozi wa Mila ya kimasai, maarufu kama
Laigwanani wa Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha wamesema wanamruhusu
kuwania ubunge wa Jimbo la Monduli, mtoto wa kike wa Waziri Mkuu wa
zamani, hayati Edward Moringe Sokoine, Namelock Sokoine.
Mbunge
wa sasa wa jimbo hilo, Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametangaza
nia ya kutogombea tena jimbo hilo, hali ambayo imeibua mvutano kwa
makada kadhaa wa CCM wilayani Monduli. Namelock alikuwa mmoja wa watoto
kipenzi cha hayati Sokoine,
Katibu wa viongozi hao wa
kimasai, Buluka Ngaimeria na Makamu Mwenyekiti wake, Mepukori Mberekeri,
kwa nyakati tofauti alisema wao kama viongozi wa mila, hawajatoa
msimamo wa kumkataa Namelock kwa kuwa ni mwanamke.
Ngaimeria
alisema, hivi karibuni walikutana katika Kata ya Makuyuni, lakini
hakukupitishwa azimio la kumkataa Namelock kwa kuwa ni mwanamke.
“Mimi
kama Katibu wa viongozi wenzangu, hatukufikia maamuzi ya kumkataa mtu,
kile kikao kilikuwa cha kujadili mambo yetu ikiwepo kutokuwa na ofisi na
masuala ya siasa haikuwa hoja kuu,” alisema.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa viongozi hao, Mepukori Mberekeri alisema, yeye
ndiye alitoa taarifa kwenye kikao hicho, juu ya tangazo la Namelock
kuwania ubunge alilotoa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya
ya Monduli.
“Baada ya kuwapa taarifa mjumbe mwingine
alisema pia kuna mgombea mwingine, Loota Sanare na baada ya majadiliano
suala hilo liliachwa lije kuamuliwa na wananchi,” alisema.
Alisema
sio kweli kuwa wao, wametangaza kupinga kuongozwa na Mbunge mwanamke na
sio kweli kuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Edward Lowassa anawashinikiza
kumtaka Sokoine.
Uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Monduli, umeibua gumzo kubwa hasa kutokana na uamuzi wa Lowassa kutajwa kuutaka urais.