Ndege ya JWTZ yaanguka, rubani wake ajiokoa kwa parachuti
Ndege ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuanguka katika uwanja wa ndege Mwanza. Picha kwa hisani ya Ray Naluyaga.
Mwanza. Hali ya taharuki ilitanda kwenye Uwanja wa Ndege wa
Mwanza baada ya ndege ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
kuanguka na kuteketea kwa moto.
Ndege hiyo ambayo
ilidaiwa kuwa ni ya kivita na ilikuwa mpya ilianguka saa mbili asubuhi
na kuteketea kwa moto, huku rubani wake akinusulika kifo baada ya kuruka
kutoka angani kwa kutumia parachuti.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatika uwanjani hapo zilidai kuwa ndege hiyo ilikuwa inaongozwa na rubani ,Peter Augustino Lyamunda.
Waandishi
wa habari mkoani hapa walifika kwenye uwanya huo muda mfupi baada ya
kutokea kwa ajali hiyo, ambapo baadhi ya maofisa wa JWTZ walikataza
wanahabari wasipige picha wala kuripoti kitu chochote kuhusu ajali hiyo.
Kutokana
na kuzuiliwa kwa waandishi wa habari, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa
kuhusu ajali hiyo. Gazeti hili jana lilimtafuta Meneja wa Uwanja wa
Ndege wa Mwanza, Esther Madale hakupatikana, lakini baadhi ya maofisa wa
uwanja huho ambao hawakutaja majina yao walidai kuwa suala hilo
linahusu mamlaka nyingine, na wao hawawezi kulizungumzia.
Hata
hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo naye alipotafutwa
kuzungumzia tukio hilo hakuweza kupatikani kwa kuwa alikuwa kwenye
kongamano la viongozi wa dini.
Uwanja wa ndege wa
Mwanza umekuwa na matukio kaadha ya ajali za ndege ikiwamo ndege
kushindwa kuruka kutokana na hitilafu mbalimbali.