Serikali yaanza kugawa nakala milioni mbili Katiba inayopendekezwa
Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha-Rose Migiro.
Dar es Salaam. Waziri wa Katiba na Sheria,
Dk Asha-Rose Migiro amesema kila kata nchini itapata nakala 300 za
Katiba Inayopendekezwa ili kuwawezesha wananchi kuisoma na kushiriki
katika Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu.
Amesema
mpaka kufikia Februari 9, mikoa 11 nchini ilikuwa tayari imepatiwa
nakala hizo na kwamba Serikali imepanga kuchapisha nakala milioni 2 kwa
ajili ya kuzisambaza nchi nzima.
Amesema nchini kuna
zaidi kata 3,800 na lengo la Serikali ni kusambaza nakala hizo kwenye
vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya,
wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na majiji.
Akizungumza na Mwananchi leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, (Terminal one)
akitokea
mkoani Dodoma, Dk Migiro alisema mbali na nakala hizo, Katiba
Inayopendekezwa pia imewekwa katika tovuti za Wizara ya Katiba, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bunge.
“Wananchi
waliokuwa katika miji na vijiji siyo wote wanaweza kupata nakala katika
mtandao. Ukiwa na nakala halisi unaisoma wakati wote kwa hiyo Serikali
imekuwa na nia ya kuwapatia watanzania nakala halisi haraka
iwezekanavyo,” alisema.
Alisema Serikali ilipoanza
mchakato wa uchapaji wa nakala hizo liliibuka tatizo la mitambo kwa
baadhi ya wachapishaji na hivyo kuchelewesha kuzigawa, lakini kwa sasa
nakala nyingi na zinaendelea kusambazwa kadri zitakavyokuwa zikichapwa.
“Karibu
nusu ya mikoa yote imepelekewa nakala hizo. Tumeweka utaratibu mzuri
ambao kila mkoa utapata nakala kutokana na wingi wa kata zake, hatuwezi
kugawa nakala sawa kutokana na kutofautiana kwa idadi ya kata” alisema.
Aliitaja
mikoa ambayo imepata nakala hizo na idadi yake katika mabano: Katavi
(15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu
(34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540) na Kigoma (41,440).
Mikoa
mingine ni Kagera (54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani
ambapo usambazaji umeanza kwa wilaya ya Mafia ambayo imepata nakala
2,400.
Alipotakiwa kufafanua kama nakala hizo zitatosha
ikilinganishwa na idadi ya Watanzania alisema, “Jambo la muhimu ni
utolewaji wa elimu kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Nakala hizi zinatosha
kwa sababu Katiba ni waraka wa kisheria unaweza ukausoma na bado ukabaki
kuhoji baadhi ya mambo.”
Alisema nakala 1,800,000 zinasambazwa Tanzania Bara na nakala 200,000 zinasambazwa Zanzibar.