Mbowe avunja uongozi Chadema Ukonga, Ilala


“Tulichambua kwa kina na kuona huo upungufu, hatukuwafukuza viongozi wale, lakini  viongozi walitakiwa kuwajibika kisiasa na walijiuzulu,” Freeman Mbowe.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameuvunja uongozi wa chama hicho kwenye majimbo ya Ukonga na Ilala kutokana na kutoelewana kwa muda mrefu baina ya viongozi na kutofanya  vizuri kwa chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Habari ambazo Mwananchi imezipata na kuthibitishwa na Mbowe zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo aliuvunja uongozi huo wiki mbili zilizopita baada ya kikao cha siri na viongozi wa majimbo hayo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Klabu ya Billicanas iliyopo katikati ya jiji.
Pamoja na CCM kuibuka na ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo wa ngazi ya mwanzo ya uongozi, Chadema iliongoza kwa upande wa upinzani ingawa haikuwa na matokeo mazuri kwenye majimbo hayo mawili.
Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa asilimia 79.4 katika nafasi ya uenyekiti wa mitaa, Chadema asilimia 15.1 na CUF asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla vilipata asilimia 0.9. 
Matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji yanaonyesha kuwa CCM ilishinda kwa asilimia 79.3, Chadema asilimia 15.6, CUF asilimia 4.3 na vyama vingine vilipata asilimia 0.8. Katika uchaguzi wa nafasi za uenyeviti wa mitaa, CCM ilishinda kwa asilimia 66.5, Chadema asilimia 25.4, CUF asilimia 6.8 na vyama vingine vilipata kwa asilimia 1.3. 
Matokeo ya Wajumbe wa Serikali za vijiji/mitaa yanaonyesha CCM ilipata asilimia 79.3, Chadema asilimia 15.7, CUF asilimia 4.3 na vyama vingine  asilimia 0.7, wakati katika wajumbe wa viti maalum CCM ilipata asilimia 82.1, Chadema asilimia 13.7, CUF asilimia 3.5 na vyama vilivyobaki navyo vilipata asilimia 0.7.
Mbowe akerwa
Chanzo cha habari kinapasha kuwa ushindi wa CCM katika maeneo mengi na zaidi Jimbo la Ukonga ndiyo uliomkera zaidi Mbowe pamoja na misigano ndani ya chama.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mbowe alikiri  kufanya kikao cha uongozi ambapo pamoja na mambo mengine waliangalia uwajibikaji, mafanikio na kushindwa kwa chama hicho katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
Alieleza kuwa, katika kikao hicho waligundua kasoro mbalimbali katika majimbo hayo ya Ukonga na Ilala na kuafikiana kuwa viongozi wao wawajibike kutokana na upungufu huo.
“Tulichambua kwa kina na kuona huo upungufu, hatukuwafukuza viongozi wale, lakini  viongozi walitakiwa kuwajibika kisiasa na walijiuzulu,” alisema Mbowe.
 Kwa maelezo ya Mbowe, sasa majimbo hayo yapo chini ya  Ofisi ya Kanda Maalumu ya Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, ambayo inasimamiwa na Mabere Marando hadi hapo uongozi wa kikatiba utakaporejeshwa.
Mwenyekiti wa Chadema wa Jimbo la Ukonga, Thomas Nyahende alitangaza kwenye ukurasa wake wa facebook kuwa ameamua kuachia ngazi kutokana na hali ya kutoelewana iliyokuwapo baina ya uongozi wake na mratibu wa chama hicho Kanda ya Pwani.
“Napenda kuwafahamisha kuwa jana, Jumamosi tarehe 24 Januari 2015 nimetangaza rasmi kujiuzulu nafasi yangu ya mwenyekiti wa Jimbo la Ukonga. Katika hali hiyo wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji wa Jimbo la Ukonga nao wamejiuzulu ili kuungana na mwenyekiti wao,” aliandika Nyahende kwenye ukurasa huo wa mtandao ya kijamii.
“Hatua hiyo ngumu sana tumeifikia jana baada ya kushauriana na mwenyekiti wetu wa Taifa, Kamanda Mbowe kufuatia hali ya sintofahamu iliyokuwapo kwa muda mrefu baina ya viongozi wa Jimbo la Ukonga na mratibu wa Kanda yetu ya Pwani. Tumefikia uamuzi huo kwa ajili ya kuzingatia maslahi mapana ya Chadema katika Jimbo la Ukonga.”
Mwenyekiti huyo aliwataka wafuasi wa chama hicho kuendelea kuiunga mkono Chadema na hasa uongozi mpya ambao alisema ungeundwa muda mfupi baadaye wakati taratibu za uchaguzi zikiandaliwa.
“Sasa tujielekeze katika kuijenga upya kanda yetu ya Pwani iliyokuwa imedorora, ili iweze kutuunganisha na kuratibu shughuli za chama katika kanda yetu na hatimaye kanda yetu iweze kuwa kitovu na kiongozi wa mabadiliko ya uongozi katika nchi hii tutakapopofanya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu 2015,” alisema.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Mbowe amekerwa na mwenendo mzima wa uongozi huo na kuamua kuuvunja  na kutangaza kuwa  uchaguzi wa viongozi wa jimbo hilo utafanyika Jumamosi ya Februari 14 mwaka huu.
Mmoja wa wanachama wa Chadema alisema kuwa sababu ya kwanza ya viongozi wa jimbo hilo kuondolewa ni kushindwa kusimamia vizuri uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Sababu nyingine kubwa ni kuwapo kwa ushirikiano mdogo baina ya viongozi wa jimbo na pia kutokuwa na ushirikiano mzuri na viongozi wa chini katika sekta mbalimbali.
Mwanachama huyo, ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa sababu maalumu, alisema viongozi wa jimbo hilo walikuwa hawaelewani na viongozi wa chini na kusababisha baadhi ya mitaa kuchukuliwa kirahisi na CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kitu kilichomkasirisha mwenyekiti.
“Mfano Mtaa wa Kigogo Fresh B, uchaguzi ulivurugwa na wanachama wa CCM, hivyo hakuna mwenyekiti aliyeshinda. Lakini kilichotokea Januari 22 mwaka huu  siku walipoapishwa baadhi ya wenyeviti kwenye ukumbi wa Anatoglo, alijitokeza Mariano Maurus wa CCM na kusababisha wafuasi wa Ukawa kumshambulia na kuzuia asiapishwe,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliachwa kiporo kutokana na utata wa matokeo kwenye uapishaji wa wajumbe wa Manispaa ya Ilala.
Alisema baadaye mgombea huyo wa CCM aliitwa kwenye Ukumbi wa  Anatouglo kwa siri na kuapishwa, jambo ambalo ni moja ya sababu ya viongozi wa jimbo hilo kuvuliwa madaraka.
Hivi karibuni wakazi wa mtaa wa Migombani eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam waliamua kumuapisha mwenyekiti wa mtaa huo, Japhet Kembo baada ya mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi kumuwekea zuio kwa madai ya kutekeleza amri kutoka mamlaka za juu.
Hata hivyo,  wakazi hao walidai kutopewa sababu za msingi za kusimamishwa kwa hatua ya kuapisha huku  matokeo yakionyesha aliyeshinda ni mgombea wa Chadema hivyo walichukua hatua ya kumtafuta wakili wa kujitegemea wakidai kuwa shughuli za mtaa huo zinazorota kutokana na kutokuwa na uongozi.
Ujumbe wa Thomas Nyahende alioandika kwenye facebook
Makamanda na marafiki zangu wote, napenda kuwafahamisha kuwa jana Jumamosi tarehe 24 Januari 2015 nimetangaza rasmi kujiuzulu nafasi yangu ya Mwenyekiti wa Jimbo la Ukonga. Katika hali hiyo wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji Jimbo la Ukonga nao wamejiuzulu ili kuungana na Mwenyekiti wao.
Hatua hiyo ngumu sana tumeifikia jana baada ya kushauriana na Mwenyekiti wetu wa Taifa, Kamanda Mbowe kufuatia hali ya sintofahamu iliyokuwepo kwa muda mrefu baina ya viongozi wa Jimbo la Ukonga na Mratibu wa Kanda yetu ya Pwani. Tumefikia uamuzi huo kwa ajili ya kuzingatia maslahi mapana ya Chadema Jimbo la Ukonga.
Nawashukuru sana makamanda na marafiki wote ambao mmekuwa mkiniunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yangu nikiwa Mwenyekiti wa Jimbo la Ukonga. Sasa niwaombe tuendelee kuisupport Chadema na hasa uongozi wa mpito utakaoundwa hivi karibuni wakati taratibu za kuitisha uchaguzi mpya zikiandaliwa.
Sasa tujielekeze katika kuijenga upya kanda yetu ya Pwani iliyokuwa imedorora, ili iweze kutuunganisha na kuratibu shughuli za chama katika kanda yetu na hatimaye kanda yetu iweze kuwa kitovu na kiongozi wa mabadiliko ya uongozi katika nchi hii tunapofanya uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu 2015.
Powered by Blogger.