Wahitimu 344 darasa la Saba hawajui kusoma wala kuandika
Wanafunzi 344 waliomaliza darasa la saba mwaka huu
mkoani hapa wamebainika kuwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Ofisa
elimu wa mkoa, Nestory Mloka alitoa taarifa hiyo juzi katika kikao cha
elimu kilichoitishwa kwa ajili ya kuchambua matokeo ya mtihani wa darasa
la saba na kuwapangia shule wahitimu waliofaulu.
Mloka alisema kati ya walihitimu hao ambao hawajui kusoma na kuandika, wavulana ni 163 na wasichana 181.
Alisema
Wilaya ya Ngorongoro yenye wakazi wengi wafugaji wa jamii ya Kimasai,
ndiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi hao wenye tatizo hilo wanaofikia 230.
“Idadi
ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwa Wilaya ya Ngorongoro ni
kubwa kuliko sehemu nyingine zote za Mkoa wa Arusha,” alisema Mloka.
Hata
hivyo, alisema wanafunzi 23,250 wamefaulu mtihani huo wa kumaliza elimu
ya msingi mwaka 2014, sawa na asilimia 67.69 ya waliofanya mtihani.
Mloka alisema wanafunzi wote waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali.
Alisema
wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni kati ya
wanafunzi 34,348 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka
2014 mkoani Arusha.
“Kati ya wanafunzi 34,348
waliofanya mitihani, wavulana walikuwa 16,474, wakati wanafunzi wa kike
walikuwa 18,454,” alisema Mloka.
mwananchi
mwananchi