Rushwa yaitesa CCM kuelekea urais 2015
Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM kinaonekana kuteswa
WanaCCM wakishangilia katika moja ya mikutano ya kampeni, Picha na Maktaba
WanaCCM wakishangilia katika moja ya mikutano ya kampeni, Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya kufanyika
kwa Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na tuhuma za rushwa
inayodaiwa kutolewa na makada wake wanaotajwa kutaka kuwania nafasi
mbalimbali ukiwamo urais.
Hali hiyo inabainishwa na
kauli za baadhi ya makada wa chama hicho katika ngazi mbalimbali ambao
wameamua kulalamika waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au kwenye
mitandao ya kijamii.
Moja ya kauli hizo ni ile
iliyotolewa juzi na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki
kwenye akaunti yake ya Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya
kwa wajumbe husika wa CCM ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni
ununuzi wa nafasi na si uwezo wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa
kufafanua kauli yake, Kagasheki alisema kwenye maoni yake hakutaja mtu
licha ya kwamba wapo wengi wanaotoa zawadi, lakini baada ya kuandika
katika mtandao ameandamwa na baadhi ya watu huku wengine wakimtolea
lugha chafu.
“Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo
siku zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo
mpaka wengine wanatumia lugha kali... sijamtaja mtu kwa sababu najua
wapo watu wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki aliyewahi
kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa hayo ni mawazo
huru ambayo anayaamini.
Waliyonena kuhusu rushwa
Kauli
ya Kagasheki haina tofauti na zile zilizowahi kutolewa na makada
wengine, akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na wengine
waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya chama hicho na Serikali yake
juu ya kukithiri kwa rushwa katika kusaka madaraka.
Makamu
Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alimwambia mwandishi wetu jana kuwa
suala hilo linafuatiliwa kwa karibu na dawa yake itaiva Februari baada
ya kamati yake ya maadili iliyofuatilia kutoa tathmini yake.
“Tulipotangaza
kuwafungia, tuliunda kamati ya ufuatiliaji harakati za kila mmoja kuona
je, yale tuliyomtaka kutoyafanya ametekeleza? Sisi tunaheshimu vikao
vyetu, hivyo tunasubiri kamati hiyo itakapotuletea taarifa yake.
“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo wa kusamehewa watasamehewa na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”
Kauli
ya Mangula ilikuwa inafafanua makada wa chama hicho waliopewa onyo kali
kwa kufanya kampeni mapema na kujihusisha na vitendo vinavyokiuka
maadili ndani ya chama na ndani ya jamii.
Mangula
alisema hayo wakati kukiwa na madai kuwa baadhi ya wanachama wake
kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano mkuu na Halmashauri Kuu ya
Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya nchi.
Mangula
jana alikaririwa na gazeti la CCM, Uhuru, akijibu madai hayo kuwa,
“hakuna mwanachama aliye juu ya katiba, kanuni na miongozo ya chama na
hivyo hakitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia fedha.”
Kwa
mujibu wa madai hayo, kada mmoja wa CCM anadaiwa kugawa kati ya Sh1
milioni na Sh500,000 kama zawadi ya sikukuu ya Krismasi kwa wajumbe wa
vikao vya chama visiwani humo.
Mangula alisema kutokana na malalamiko hayo, CCM
itapeleka timu ya uchunguzi kupitia kitengo cha usalama na maadili
kuchunguza tuhuma hizo.
Oktoba 25, mwaka jana Rais
Kikwete alisema endapo rushwa haitakomeshwa ndani ya CCM, kitaanguka
vibaya katika Uchaguzi Mkuu 2015 na iwapo kitanusurika hakitapita mwaka
2020.
Kauli hiyo pia inaungwa mkono na Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye aliyewahi kuliambia gazeti hili kuwa iwapo
misingi ya uchaguzi ndani ya CCM itaendelea kulalia kwenye rushwa,
hataendelea kuwa sehemu yake na kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya
na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete
alitangaza mkakati wa ‘kujivua gamba’ akiwataka makada wa chama hicho
wanaotuhumiwa kwa ufisadi kutafakari na kujiondoa ndani ya siku 90,
lakini hata baada ya muda huo kumalizika, mkakati huo uliyeyuka na
viongozi wakaanza kubadili maudhui yake.
Waliopigwa ‘stop’
Vigogo
waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Wanavyoitazama CCM
Wachambuzi
waliozungumza na gazeti hili walisema CCM hakiwezi kupambana na rushwa
kwa sababu baadhi ya viongozi wake ni walarushwa na wamekiondoa katika
misingi ya kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu
Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema: “Chama hakiongozwi kwa
makaripio, mkakati wa kujivua gamba na matamko katika vyombo vya habari.
Kinaongozwa kwa mifumo imara, fikra sahihi, dira na historia yake
nzuri.
“Ndiyo maana wanachama wa CCM wamekuwa wakitenda
mambo kinyume na katiba ya chama chao na hakuna wa kuwachukulia hatua.
Kolimba (marehemu) aliwahi kusema kuwa CCM haina dira wala mwelekeo.
Hilo linaonekana sasa, kimeshindwa kukemea rushwa.”
Alisema
ni vigumu kwa CCM kuikataa rushwa wakati baadhi ya wanachama wake, tena
wenye nyadhifa za juu ndani ya chama hicho wakituhumiwa kwa rushwa.
“Mchawi
yupo ndani ya CCM yenyewe. Profesa Tibaijuka ni mjumbe wa Kamati Kuu na
amepewa mgawo wa escrow lakini chama kipo kimya. Jimbo la Bukoba
Vijijini limegawanyika kwa sababu ya rushwa inayotolewa na wanaotaka
ubunge, hayo yote CCM hawayaoni na kukimbilia yanayotokea Zanzibar,”
alisema. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana
alisema: “CCM ni chama ambacho kinajibu mapigo ila hakitoi mapigo.
Kinachotokea sasa ni dalili mbaya kwake kwani kimekuwa dhaifu katika
kuwashughulikia wanachama wake wasio waadilifu.”
Alisema
matamko mengi ya chama hicho ni ya kisiasa zaidi na mengi huishia
katika vyombo vya habari. “Hayo yanamaanisha kuwa uwezo wa CCM
umepungua. Mfano ni Chadema kwa sasa kinatoa mapigo na si kujibu mapigo
pekee. Hiyo ndiyo inatakiwa kufanywa na chama cha siasa,” alisema.
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema Mangula alipotangazwa kuwa
Makamu Mwenyekiti wa CCM aliahidi kupambana na rushwa na mpaka leo
kashindwa.