DC abaini mchezo mchafu wa wauguzi
Bagamoyo. Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Ahmed
Kipozi amesema atawachukulia hatua baadhi ya wahudumu wa Hospitali ya
Bagamoyo wanaolalamikiwa na wagonjwa kuwa huwalazimisha kwenda kununua
dawa nje wakati zinapatikana hospitalini hapo.
Alisema
hayo jana alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa afya
uliolenga kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo
ya wilaya.
Kipozi alikiri kuwapo malalamiko ya mara
kwa mara kuhusu wananchi kunyimwa dawa hospitalini hapo na baadhi ya
wahudumu ambao huwataka kwenda kununua kwenye duka moja la jirani na
eneo la hospitali.
Alisema wilaya imefanyia kazi
malalamiko na kubaini kuna udhaifu wa kiutendaji unaowahusu baadhi ya
wahudumu ambao alisema wameamua kuchafua sifa ya hospitali hiyo na
Serikali. Alisema hatakubali kuona hali hiyo ikiendelea na kwamba
umefika wakati wa kuchukua hatua stahili dhidi ya wahusika wote.
“Kamwe
hatuwezi kuwavumilia tena wahudumu wenye tabia hii. Wamekuwa kero kwa
wakazi wa wilaya na wale wanaotoka nje ya wilaya wanaofika kupata huduma
za afya katika hospitali yetu. Mimi binafsi nimekuwa shuhuda wa haya
ninayoeleza na bahati nzuri leo hii wadau pia wanazungumzia hilo,”
alisema Kipozi.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo, Kusekwa Mashaka
alisema kinachochangia hospitali nyingi za Serikali kushindwa kufanya
kazi kwa ufanisi ni kutokana na urasimu wa utoaji wa vibali vya
kuchukulia dawa unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Bohari ya Dawa
(MSD).
Alisema hospitali yake hushindwa kununua dawa nje ya utaratibu wa kawaida wanapokuwa wamepungukiwa.
Daktari
huyo ameongeza kuwa kama huduma ya afya katika Serikali ya wilaya ya
Bagamoyo zikiboreka basi malalamiko ya wakazi wa wilaya hiyo yatapungua .
Aidha
kwa upande wake mratibu wa asasi ya Uhakika kituo cha ushauri nasaha
UKUN-PHI Charles Njonjele ambao ndio walioratibu mkutano huo chini ya
ufadhili wa shirika la Action Aid alisema lengo la mkutano huo ni
kujadili changamoto na matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya afya
wilayani humo na pia kupata majawabu ya nini kifanyike kuzitatua ama
kuzipunguza kabisa.
“Lengo kubwa hasa ilikuwa ni
kujadili changamoto mbalimbali katika sekta ya afya wialayani hapa na
zaidi tulilenga kujadili changamoto zlizopo hospitali ya wilaya haswa
suala zima la utoaji wa huduma na kutafuta mbinu mbalimbali za
kukabiliana na changamoto hizo, ili jamii iweze kuamini hudumu
wanazipatiwa, kama dawa hakuna waamini hivyo na kama zipo basi zitolewe
kwa wagonjwa na sio kuleta usumbufu kwao ”alisema Njonjele.