Mchakato Uchaguzi Serikali za Mitaa umevurug
Mchakato Uchaguzi Serikali za Mitaa umevurugwa0
Mchakato huo ulianza kwa wananchi kujiandikisha
ili kupiga kura Desemba 14, mwaka huu. Kwa utaratibu wa kawaida, muda
huo wa siku saba kujiandikisha ulikuwa mfupi mno. Muda huo ulikuwa
hautoshi kwa watu wengi kujiandikisha kutokana na kubanwa na shughuli za
kazi na mazingira magumu wanayoishi.
Ndiyo maana yaliibuka malalamiko mengi kutoka kila
kona kwamba Serikali pengine ilikuwa imedhamiria kukinufaisha chama
tawala ambacho kina mifumo ya kuwafikia wafuasi wake katika muda mfupi,
tofauti na vyama vya upinzani.
Kampeni za uchaguzi huo zilianza siku nne
zilizopita na zitaendelea hadi Desemba 13, siku moja kabla ya kufanyika
kwa uchaguzi huo. Lakini wakati mchakato huo ukiendelea na wanachama wa
vyama vya siasa wakijitokeza kugombea nafasi mbalimbali, yametokea
matukio mengi ambayo yamedhihirisha kwamba siyo tu kuna ubabaishaji
mkubwa katika uendeshaji wa mchakato huo, bali pia kwamba Serikali
haikuwa imefanya matayarisho ya kutosha au kuweka mazingira mazuri ya
kufanyika kwa uchaguzi huo muhimu. Jambo la kusikitisha ni kwamba
Serikali imebakia kuwa mtazamaji badala ya kuhakikisha kwamba kasoro
zinazojitokeza zinapewa suluhisho stahiki na kwa wakati.
Wananchi wamebakia kujiuliza kama kasoro hizo
zinatokea kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Mbali na vurugu zinazotokana
na waratibu wa uchaguzi huo kukiuka taratibu, kanuni na miongozo
iliyowekwa, umejitokeza utamaduni wa watendaji wa serikali za mitaa na
kata katika maeneo mengi nchini kuegemea upande mmoja.
Moja ya mikakati inayoharibu mchakato huo ni
wagombea wa upinzani kuwekewa pingamizi, huku kamati za rufaa
zikionekana wazi kutoa uamuzi unaopendelea baadhi ya wagombea au kukataa
kabisa kusikiliza rufani hizo.
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) imetoa miongozo na
kanuni ambazo kinadharia zinaonekana zinaweza kuendesha mchakato huo
kwa haki. Hata hivyo, ni vyema kutambua kuwa, kuweka kanuni na miongozo
ni jambo jema, lakini suala la msingi ni usimamizi na utekelezaji wake.
Vinginevyo, hakuna sababu ya kuwapo msululu wa watendaji na kamati
mbalimbali za kusimamia mchakato huo, kama hakuna mifumo inayowezesha
wagombea wote kutendewa haki bila ubaguzi wowote, kwa maana ya kuangalia
vyama wanavyotoka.
Sisi tunadhani kwamba hali hiyo ni matokeo ya
Serikali kutojiandaa vya kutosha au kutokuwa na utashi. Uchaguzi
umeahirishwa katika baadhi ya sehemu kutokana na ugomvi wa mipaka, huku
katika sehemu nyingine vurugu zimetokea kutokana na mamlaka husika
kushindwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya kanuni na miongozo.
Ni wajibu wa Serikali kuondoa kasoro hizo na
nyingine nyingi katika siku 10 zilizobaki kabla ya uchaguzi huo.
Vinginevyo ni kuweka mazingira ya uchaguzi huo kutokuwa huru na wa haki
kwa kuruhusu matatizo ambayo yanaweza kuepukika.
chanzo;mwananchi