INASIKITISHA SANA,MAITI 5 ZA FAMILIA MOJA ZA ZIKWA KABURI MOJA





INATISHAAAA   MAITI 5   ZA   FAMILIA MOJA ZA ZIKWA KABURI MOJA


DIMBWI la simanzi lilitanda katika kijiji cha Kimuchu, eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, wakati wa mazishi ya watu watano wa familia moja waliokufa katika hali ya kutatanisha.
Jamaa za marehemu Paul Magu, 35, mkewe Lydia Wangui, 35 na watoto wao Allen Muhiu (9), Ryan Ndau (8) naTiffany Wambui (5) walishindwa kuzuia machozi na baadhi yao kuzirai wakati wa mazishi hayo.
Kasisi James Kamura wa Kanisa la Kiangilikana Thika, alitoa mahubiri yaliyogusa wengi huku akiitaka serikali iwaadhibu waliowaua watoto hao na mama yao.
"Ni jambo lenye uchungu sana kwa familia kuweza kuvumilia. Ni vigumu kuelewa kilichotendeka kwa sababu wote wamekufa. Damu ya binadamu haifai kumwagwa kama ya mnyama," akasema Kamura.
Magu aligongwa na basi kwenye barabara ya Thika-Garissa nao mwili wa mkewe uliokuwa na majeraha ukapatikana karibu na hoteli ya Paradise Lost Resort, Kiambu.
Miili ya watoto wao ilipatikana kichakani siku chache baadaye karibu Tatu City, eneo la Ruiru.
Jumanne, miili ya familia hiyo ilipelekwa eneo la mazishi kwa magari matatu ya kubebea maiti kisha ikapelekwa kwenye kaburi la pamoja ambapo ilizikwa.
Waombolezaji kadha walizirai na kuondolewa eneo la mazishi.
"Haiwezekani kwamba mauaji haya yalitekelezwa na mtu mmoja. Kuna watu walio hai waliohusika na uhalifu huu wa kikatili na ni lazima serikali ichukue hatua," akasema Kasisi Kamura akiongoza ibada ya wafu katika nyumba ya wazazi wa Magu, karibu na mji wa Thika.
Wakazi walifika kwa wingi kwa ibada na mazishi ambayo yalihudhuriwa na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa na Mbunge wa Juja Francis Munyua. Gavana wa Kiambu William Kabogo aliwakilishwa na msaidizi wake Sammy Onyango.
Kukatiza ibada
Mhubiri alilazimika kukatiza ibada mara kadha na kuomba jamaa waliolemewa na huzuni wasaidiwe.
Wazazi wa mama ya watoto hao, Francis Ndau na Mary Muthoni na jamaa zao wa karibu kutoka Kaunti ya Nyandarua walishindwa kusimama wakati wa kuimba kwa kulemewa na majonzi.
Kasisi aliwagusa zaidi waombolezaji aliposimulia matukio yaliyotangulia kupatikana kwa miili ya watoto hao siku chache baada ya wazazi wao kufa katika hali ya kutatanisha. 
"Mimi binafsi niliomba watoto hao wapatikane wakiwa hai. Lakini nililia walipopatikana wamekufa. Kwa nini mtu afanye hivi," akashangaa.
Kasisi Kamura alisema mauaji hayo yalihusu imani na kuwataka polisi wachunguze kilichotendeka.
"Wakenya wana haki ya kujua yanachofunza mashirika ya kidini na vitendo vyake na ni jukumu la serikali kuwaondoa wahubiri wanaopotosha," akasema.
Aliongeza kuwa wakati umefika kwa serikali kudhibiti mashirika ya kidini kwa sababu vitendo vya baadhi yake ni vya kutiliwa shaka.
Aliwataka wafuasi wa makanisa wakatae baadhi ya wahubiri wanaotumia dini kujitajirisha
Powered by Blogger.