Maambukizi kutoka kwa mama kwenda mtoto yapungua Moro Vijijini
Wednesday Dec 3, 2014
Na Waandishi wetu
3rd December 2014
B-pepe
Chapa
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Seif Seleman Rashid.
Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto 106 waliozaliwa na wajawazito wenye VVU nane wamekutwa wameambukizwa Ukiwmi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Maambukizi hayo yamepungua kutoka watoto 16 walioambukizwa katika kipindi cha mwaka uliopita kutokana na jitihada zilizofanywa na halmashauri ya hiyo kwa kushindirika na wadau wa mapambano na viti dhidi ya Ukimwi.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyoandaliwa na Mtandao wa Wakulima Wadogowadogo Tanzania (Mviwata) na kufanyika kiwilaya katika kata ya Tawa, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi, alisema takwimu hizo zimeifanya wilaya yao kuwa na maambukizi ya asilimia 2.5 hadi kufikia Oktoba mwaka huu.
Alifafanua kuwa watoto hao nane wamepata maambukizi hayo baada ya mama zao kushindwa kufata masharti ya kumeza dawa za kuzuia maambukizi.
SIMANJIRO WATAKA ELIMU
Jamii ya wafugaji ya Wamasai wilayani Simanjiro mkoa wa Mara, wameiomba serikali kufikisha elimu ya kupambana na ukimwi kwenye maeneo yao ili kupunguza maambukizi mapya.
Ombi hilo limetolewa na Kiongozi wa kimila wa Jamii ya Kimasai Tarafa ya Einduimenti, Olekatoe Olesokooi wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.
Alisema ametoa ombi hilo kutokana na Ukimwi kuwa bado changamoto kubwa kwa wafugaji kutokana na kukosa elimu.
Olesokooi alisema jamii ya Wamasai imesahaulika kupatiwa elimu dhidi ya Ukimwi na kuwa hatarini kuangamia kwa janga hilo.
Rukwa washauriwa kuacha kurithi wajane
Nao wakazi wa mkoa wa Rukwa, wameshauriwa kuachana na mila na desturi potofu za kurithi wajane na wageni kwa sababu zinachangia maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kukithiri kwa umaskini miongoni mwao.
Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Rukwa, Azizi Kalyatila wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Kirando wilaya ya Nkasi..
Aliitaja vyanzo vya maambukizi hao kuwa ni ngono zembe, ulevi na mila hizo na desturi potofu.
Alisema maadhimisho hayo yamefanyika katika kata hiyo kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi hayo mkoani humo.Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Idd Kimanta, alisema maambukzi hayo yamekuwa tishio hasa kwa wakazi wa Kirando ambao wapo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Mwisho.
KIBAHA MAAMBUKIZI YASHUKA
Maambukizi mapya ya VVU katika Halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani yameshuka ikilinganishwa na takwimu zilizotolewa mwaka 2013.
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi wa Halmashauri hiyo, Siwema Cheru akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kudhibiti virusi vya Ukimwi na Ukimwi kwa mgeni rasmi kwenye Maadhimisho hayo, Silvestry Koka, alisema kuwa kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu watu 11,996 walijitokeza kupima afya zao, kati yao 1,064 sawa na asilimia 8.7 walipatikana na maambukizi mapya ya ukimwi
“Maambukizi haya yamepungua kwa asilimia moja kwani mwaka 2013 ilikuwa na asilimia 9.7, ”alisema.
Alizitaja sababu zinazochangia maambukizi hayo kuwa ni ngoma za usiku maarufu kama vigodoro, kangamoko, mabanda ya video yanayoonesha picha zisizokuwa na maadili kwa watoto wadogo na jamii kutozingatia elimu dhidi ya Ukimwi.
Imeandikwa na Ashton Balaigwa, Morogoro; Mary Mosha, Simanjiro; Arafa Masingo, Sumbawanga na Innocent Byarugaba, Kibaha
CHANZO:
NIPASHE
Habari Zaidi