Ukawa walitaka Bunge kuiwajibisha Serikali
>Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umelitaka Bunge kuiwajibisha serikali ikiwa Rais Jakaya Kikwete atashindwa
Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), umelitaka Bunge kuiwajibisha serikali ikiwa Rais Jakaya Kikwete
atashindwa kutekeleza maazimio ya Bunge ikiwemo kumng’oa Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Akizungumza
jana, Mwenyekiti wa Ukawa Profesa Ibrahim Lipumba akiwa na Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbrod Slaa,
alisema Kikwete anasita kumuondoa Muhongo wakati Bunge lililishatoa
maazimio ya kutaka aondolewe.
Profesa Lipumba alisema
Bunge linalowakilisha wananchi zaidi ya milioni 45 liliazimia uteuzi wa
Muhongo utenguliwe lakini rais anasema bado anachunguza.
Profesa
Lipumba alisema kama Rais Kikwete atashindwa kumwajibisha Muhongo
atakuwa ameshindwa kutekeleza moja ya maazimio ya Bunge na kwamba Ukawa
litaliomba Bunge kuiwajibisha serikali.
Alisema moja ya njia ya kuiwajibisha serikali ni pamoja na wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.
Profesa
Lipumba alisema “ hivi rais anachunguza nini haliamini bunge, kama
anavyoteua mawaziri pia ana madaraka ya kutengua nafasi zao, sasa
anasita nini wakati ni azimio la bunge limemwelekeza, ikumbukwe kuwa
bunge kwa niaba ya wananchi ndilo lenye jukumu la kuisimamia serikali,”
alisema Lipumba.
Alisema hotuba aliyoitoa Jumatatu
wakati akiwahutubia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, haijakidhi matarajio
ya wengi kwani kuna maazimio hayajatekelezwa.
Azimio ambalo halijatekelezwa na rais Kikwete ni lile linalotaka kutaifishwa kwa mitambo ya IPTL na kutengua uteuzi wa Muhongo.
Mwenyekiti huyo alisema rais amekataa kutekeleza azimio
la kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe na kutoa sababu ambazo hazina
maana.
“Tangu mitambo ya IPTL imefungwa taifa limepata
hasara kubwa kwa sababu umeme unaouzwa na ni wa gharama kubwa kuliko
mitambo yoyote ya umeme inayotumika katika bara la Afrika taifa
limeingia hasara kubwa, rais aitaifishe,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema
katika hotuba hiyo rais alionyesha kuipendelea IPTL na kuikandamiza
Tanesco wakati akielezea kuwa fedha za Escrow zilikuwa mali ya IPTL.
Hatua za kuchukua
Lipumba
alisema kama rais atashindwa kutekeleza baadhi ya maazimio, Ukawa
wataitisha maandamano nchi nzima ili kulaani ufisadi wa Tegeta Escrow na
kushinikiza utekelezaji wa maazimio ambayo yatakuwa hayajatekelezwa.
Alisema
hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na ufisadi wa
akaunti ya Tegeta Escrow na wengine walionufaika nazo.
Sheria ya maadili itungwe upya ili iweke uwazi wa mtu yoyote kuona taarifa ya mali za viongozi.
Vyama vya siasa vya Ukawa kwa kushirikiana na wabunge vitaendelea kuelimisha umma kuhusu ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow