‘Houseboy’ jela maisha kwa kubaka mtoto
Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu kifungo cha maisha mfanyakazi wa ndani, Habibu Adamu (20) baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka sita na kumsababishia maumivu.
Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemhukumu
kifungo cha maisha mfanyakazi wa ndani, Habibu Adamu (20) baada ya
kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka sita na kumsababishia
maumivu.
Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Said Mkasiwa
alitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki na kusema kuwa mshtakiwa ambaye ni
mkazi wa Majohe, atatumikia kifungo hicho baada ya Mahakama kuridhishwa
na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano dhidi yake.
“Mshtakiwa
atatumikia kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa vijana na wanaume
wenye tabia za kikatili kama hizi dhidi ya watoto,” alisema na kuongeza
kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi akiwamo daktari
ndiyo uliomtia hatiani.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa kujitetea.
Katika utetezi wake, alisema anaumwa vidonda vya tumbo, hivyo anaiomba Mahakama imhurumie kwa kupunguzie adhabu.
“Hakimu naomba Mahakama yako inipunguzie adhabu, nina vidonda vya tumbo,” alidai mshtakiwa.
Hata hivyo, Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo na kumhukumu kifungo cha maisha jela.
Awali,
Wakili wa Serikali, Silvia Mitanto aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu
kali dhidi ya mshtakiwa kutokana na kuongezeka kwa kwa vitendo vya
ubakaji dhidi ya watoto wadogo.
Mitanto alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 2013 katika eneo la Majohe Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.