Mwanafunzi afa kwa kunyongwa

Handeni. Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kivesa wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, Isiyaka Beda (14) amefariki dunia baada ya kunyongwa na kuvunjwa shingo na watu wanaodaiwa kuwa ni wezi.
Mama wa marehemu, Abida Zuberi alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku. Alisema siku hiyo mtoto huyo alikwenda kulala kwenye nyumba ya dada yake ambaye amelazwa hospitali.
Zuberi alisema mwanaye aliombwa na shemeji yake akalale huko kwa kuwa yeye amesafiri kikazi.
Alisema usiku wakati Beda amelala waliingia watu katika nyumba hiyo yenye vyumba viwili na sebule na kwenda chumbani alimolala kisha wakamnyonga na kuiba magodoro na runinga na wakatokomea.
Alisema asubuhi yake alipigiwa simu na mkwe wake (mume wa mtoto wake) kuwa amerudi safari ila hali aliyoikuta kwake siyo nzuri.
“Aliniambiwa kuna wezi wamevunja milango na kuiba, lakini nikamuuliza Beda mzima...Hakutoa jibu la moja kwa moja ndiyo nikaamua kurudi nyumbani nikamkuta amefariki dunia,” alisema.
“Wezi hao walivunja chumba cha kwanza na baadaye kuingia alikolala Beda. Mimi nipo hospitali kwa wiki nzima sasa ninamuuguza mwanangu mwingine,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraisser Kashai alisema uchunguzi wa kifo hicho bado unaendelea ili kuwabaini waliohusika.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa polisi kwa kuwataja watu wanaodhani kuwa ndiyo wahusika wakuu kwenye masuala ya uhalifu katika jamii ili sheria ichukue mkondo wake.
Powered by Blogger.