Siku za ‘wauza unga’ China zahesabika

Siku za wasafirishaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwenda China sasa zinahesabika baada ya Jeshi

 Madawa ya kulevya


Dar es Salaam. Siku za wasafirishaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwenda China sasa zinahesabika baada ya Jeshi la Polisi na kitengo chake cha Dawa za Kulevya kubaini majina ya vigogo wanaofanya shughuli hiyo na kusema imeanza kuwashughulikia kimyakimya.
Majina ya vigogo hao yametajwa na Watanzania waliofungwa katika magereza mbalimbali nchini China kupitia barua zinazoeleza namna matajiri wa hapa nchini wanavyowatumia vijana kusafirisha dawa za kulevya.
Wafungwa hao ambao wengi wanatumikia kifungo cha maisha na wengine kati ya miaka 20 hadi 25 wanalalamika kuwa matajiri wanaowatuma hawachukuliwi hatua za kisheria, licha ya wao kuwataja kwa majina na kuweka wazi ushahidi kwa viongozi wa Serikali wanaowatembelea magerezani, China.
Hata hivyo, Kamishna wa Kikosi cha kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa pamoja na kuthibitisha kupata taarifa hizo, alisema baadhi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuwa vigogo wa unga wameshakamatwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Diwani Athumani alisema Jeshi la Polisi linafuatilia ushahidi wa barua hizo na tayari limeshafanyia kazi baadhi.
“Tunafuatilia na tayari tumeshafanikiwa kwa upande mmoja ila hatuwezi kuweka wazi kila kitu kwa sababu kama ujuavyo suala la dawa za kulevya ni nyeti mno na pengine tunaweza kuharibu ushahidi,” alisema Athumani.
Barua zilizotumwa na wafungwa hao ambazo gazeti hili limeziona, zilitumwa kupitia kasisi anayetoa huduma kwa wafungwa magerezani, Hong Kong na China, John Wotherspoon wa Parokia ya Notre Dame, Shing Tak Street, Kowloon, China ambazo zinawataja baadhi ya wafanyabiashara papa wa dawa za kulevya ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa.
Taarifa zaidi kutoka kwa Mchungaji Wotherspoon, zinaeleza kuwa hivi sasa wapo Watanzania zaidi ya 200 katika magereza hayo na 130 kati yao, wameshahukumiwa vifungo mbalimbali na wengine wapo rumande.
“Kati ya Mei na Juni 2013, zaidi ya Watanzania 50 walikamatwa Hong Kong na China. Ukiwasikiliza wanalia na wanataka kuwasiliana na ndugu zao hata kwa barua,” inasema sehemu ya barua pepe ya Mchungaji Wotherspoon aliyoituma kwa gazeti hili.
Oktoba 18, 2013 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa ziarani China aliambiwa kuwa kulikuwa na vijana 175 ambao walikuwa wamefungwa katika magereza ya nchi hiyo baada ya kukamatwa na dawa za kulevya na kwamba baadhi yao walikuwa wakikabiliwa na adhabu ya kifo.
Barua ya mmoja wa wafungwa, Michael Mmasi Daudi anayetumikia kifungo cha miaka 23 katika Gereza la Stanley, ilimtaja mfanyabiashara mkubwa wa Dar es Salaam ambaye anamiliki maduka ya simu kuwa ni gwiji wa kuwatumia vijana wadogo kubeba dawa hizo.
Wotherspoon alisema anatarajia kuzungumza na viongozi na wanausalama wa Tanzania kuhusu namna ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya.
Alisema kati ya Aprili Mosi hadi Juni 16 mwaka huu, Watanzania 16 walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Hong Kong wakiwa na dawa za kulevya.
Barua
Katika barua hizo wafungwa walisema wamekuwa wakitishwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya iwapo watathubutu kuwataja kwa vyombo vya dola.
Mfungwa Suedi Maulidi ilisema alikamatwa na kilo moja ya dawa za kulevya katika Jimbo la Macau na kumtaja tajiri anayemtuma kuwa ni mkazi wa Magomeni ambaye anamiliki mabasi na biashara nyingine.
Alisema tajiri huyo amekuwa akiwatumia vijana wasio na ajira kusafirisha dawa za kulevya maeneo ya Magomeni na kuwatisha kuwa endapo watamtaja atawaua.
Wafungwa wengine walimtaja Mtanzania anayeishi Guangzhou kwamba amekuwa akitumia mgongo wa biashara ya vipuri vya magari na simu kuficha biashara haramu inayoifanya.
Uchunguzi umebaini kuwa mfanyabiashara huyo anatajwa kuwa na ofisi katika Mtaa wa Dongfeng, Hong Kong na anashindwa kurudi nchini kukwepa mkono wa sheria.
Habari zinasema kuwa licha ya kusakwa na polisi, pia ndugu wa wafungwa wanamtafuta mfanyabiashara huyo ili kumkabidhi mbele ya vyombo vya sheria. Nzowa alisema mkono wa Serikali unajua taarifa zake na kilichobaki na kumfikia tu.
Mfungwa mwingine, Ambrose Mahimbo anayetumikia kifungo cha miaka 24, alieleza jinsi maofisa wa uhamiaji wa China wanavyowanyanyasa Watanzania wanaokwenda nchini humo kwa shughuli mbalimbali.
Mahimbo alisema maofisa hao wanapoona hati ya kusafiria ya Mtanzania, moja kwa moja humpeleka katika chumba cha mahojiano na upimaji wa kina kwa kuwa inafahamika wengi wao hubeba ‘unga’.
Mahimbo anasema baadhi yao huvuliwa nguo na wengine huwekwa uwanja wa ndege kwa zaidi ya saa nane wakifanyiwa ukaguzi.
Pamoja na kuwataja wafanyabiashara hao, barua nyingi za wafungwa hao ziliwaasa vijana wa Kitanzania kuacha biashara hiyo huku zikieleza mateso wanayoyapata katika magereza hayo ikiwamo kazi za suluba na chakula kibaya.
Powered by Blogger.