Safari ya Ukawa kwenda Ikulu 2015
Fukuto la kumpata mgombea wa kiti cha urais kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa tiketi ya Umoja
Dar es Salaam. Fukuto la kumpata mgombea wa kiti cha urais
kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), linazidi kupamba moto huku ikielezwa kuwa jina la
mgombea litatajwa kabla ya Mei mwakani.
Hatua hiyo
inatarajiwa kufikiwa baada ya vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na
NLD vinavyounda Ukawa kukubaliana njia ya kumpata kiongozi huyo.
Kwa
mujibu wa Utafiti wa Taasisi ya Twaweza uliotolewa Novemba mwaka huu,
kama mgombea hatapatikana nje ya umoja huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willbrod Slaa ndiye anayepewa nafasi zaidi ya kupeperusha bendera.
Pia,
iwapo Chadema watatoa mgombea urais, mwelekeo unaonyesha kuwa CUF
italazimika kutoa mgombea mwenza kutokana na nguvu na ushawishi ilionao
upande wa Zanzibar.
Tayari Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia ameshatangaza kuwania ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani
Kilimanjaro na ikielezwa kwamba Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu
Lipumba ananyemelea jimbo moja la ubunge kati ya Dar es Salaam au
Tabora.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya vyama
hivyo, mpaka sasa hakuna ratiba zozote za uchaguzi zilizoandaliwa,
ingawa kampeni za uchaguzi zinaendelea kufanywa chini kwa chini.
Mkurugenzi
wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya alisema ratiba ya chama
hicho inatarajiwa kuwa tayari kuanzia Februari mwakani, ingawa mambo
mengine yatategemea makubaliano na wanachama wa Ukawa.
Kambaya alisema kuwa anaamini mchakato wa suala hilo kwa upande wa Ukawa utakuwa umekamilika kabla ya Mei mwakani.
Hata
hivyo, Kambaya alisema kuwa haitakuwa jambo la ajabu iwapo Ukawa
wakasimamisha mgombea asiyekuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa
kwa kuwa wapo baadhi ya watu wanaowaunga mkono lakini siyo wanasiasa.
Iwapo
jambo hilo litatokea, itabidi mtu huyo asajiliwe kwenye chama kimoja
kama itakavyopendekezwa kwa kuwa mgombea wa urais lazima awe mwanachama
wa chama cha siasa.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
Julius Mtatiro, alisema njia pekee ya Ukawa kumpata mgombea wake kwa
njia ya amani ni kuwa vyama vyote kukaa chini na kuweka vigezo vya
mgombea vinavyohitajika.
Alisema baada ya kukubaliana
vigezo hivyo, ndipo watakapoangalia ni mgombea wa chama gani anasifa
nyingi kati ya zote zilizopendekezwa.
“Ukisema CUF,
Chadema, NCCR-Mageuzi au NLD kila mmoja alete mgombea wake, hilo jambo
haliwezekani. Kinachotakiwa ni kuangalia mtu anamvuto kiasi gani au
anakubalika kiasi gani,” alisema Mtatiro.
Baada ya kila
vyama vyote kumpata mgombea wanayempendekeza, ndipo kila chama
kitakwenda kumnadi kwa wanachama wake na atakapokubalika ndipo Ukawa
itamtembeza mikoani
Kuhusu muda wa kumchagua mgombea, Mtatiro alisema ni
vyema zoezi hilo likafanyika mapema kwa ajili ya mgombea kujiandaa na
pia kufahamika kwa wananchi.
“Urais siyo jambo la
kushtukiza, mgombea ateuliwe mapema, Ukawa ina wagombea wengi wenye sifa
ukilinganisha na CCM kwa hiyo ni vyema akafahamika mapema,” aliongeza.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alisema kuwa ratiba ya
uchaguzi ya chama hicho itategemea makubaliano na wanachama wa Ukawa.
“Zingatia
pia kwamba sasa kuna makubaliano ya ushirikiano wa Ukawa, hivyo
tutaeleza ratiba nzima ya mchakato wakati mwafaka ukiwadia,” alisema
Mnyika.
Aliongeza: “Kwa sasa kitu kinachopewa umuhimu
ni kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la
wapiga kura na kujiandaa kwa ajili ya kura ya maoni ya Katiba Mpya.”
Hata
hivyo, alisema kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, ratiba inapangwa
mwakani na Kamati Kuu itakapokaa katika siku itakayoandaliwa na
sekretarieti.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Ubungo aliongeza kuwa kwa mujibu wa katiba ya Chadema, Kamati Kuu ya
chama inafanya utafiti na kupendekeza kwa Baraza Kuu, ambapo baraza hilo
linafanya uteuzi wa awali na kupendekeza kwa mkutano mkuu.
Kwa
upande wa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema chama
bado kinatafakari Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi
karibuni na kwamba ratiba hiyo bado haijawekwa wazi.
Kafulila alipendekeza
Mapema
mwezi huu, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila
alijitokeza hadharani na kumpigia debe Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa kuwa ndiye anayefaa kupeperusha bendera ya umoja huo.
Kafulila
alisema, Dk Slaa ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 aliitikisa
CCM, anafaa kwa sababu ana sifa ya ziada ya kuwa na mvuto.
Hata
hivyo, mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Mkoba alionya kuwa
mapendekezo hayo yanaweza kuwa na madhara kwa Ukawa kwa kuwa kila chama
kinaamini mgombea wake anafaa zaidi.
“Kumpendekeza mtu
tu kunaweza kuwagawa wapiga kura, CUF wakataka kiongozi wao na Chadema
pia wakataka wao. Mgombea ni lazima apendekezwe na kupitishwa na siyo
kuchaguliwa tu. Pia, siku ya kufanya hivyo inapasa mchakato uwe wa wazi
na wananchi wote wahusikie,” alisema Mkoba.
Mkazi wa
Kinondoni, Musa Hussein alisema Ukawa wanapaswa kufanya utafiti wa kina
wa kujua sifa na nguvu alizonazo kila mgombea kwa wananchi na nafasi
aliyonayo ya kumshinda mgombea wa CCM.