SHIDA YA USAFIRI DAR









Dar es Salaam. Uhaba wa mabasi yanayokwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha umeendelea kuwatesa abiria wa mikoa hiyo hali iliyowalizimu wagombee mabasi ya usafiri wa jijini hapa maarufu kama ‘daladala’ ambayo yameruhusiwa kufanya safari katika mikoa hiyo.

Mapema juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Gilliard Ngewe alinukuliwa na gazeti hili kuwa jana wangeongeza mabasi makubwa matano ili kukidhi mahitaji ya abiria lakini jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya mabasi hayo kudai kuwa yamejaa.

Akikagua na kutoa vibali kwa daladala hizo katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani kilichopo Ubungo, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra, Conrad Shio alisema jana kuwa kila jitihada za kuyapata mabasi mengine makubwa lakini ilishindikana na kuamua kuendelea kutumia usafiri wa daladala hizo aina ya Eicher kusafirisha abiria.

“Leo (jana) kuanzia saa moja asubuhi hali ilianza kuwa mbaya tofauti na siku zingine ndiyo maana tunazikagua hizi daladala ili ziwasafirishe hawa abiria, tukishatoa kibali abiria wanaanza kugombania.

“Hatuna jinsi tutaendelea kuzitumia hizi daladala maana mabasi ya njia nyingine tuliyokuwa tukiyatagemea kurahisisha kazi hii nao wana kilio chao cha abiria kuwa wengi wanaelekea katika mikoa wanayokwenda,” alisema.

Shio alisema daladala hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 41 zilianza kuruhusiwa juzi na zaidi ya Eicher 25 zimepewa vibali na kutoza nauli ya Sh25,000 iliyopangwa na Sumatra.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Awath Haji alisema polisi wamejipanga kuhakisha abiria hao wanalindwa kwa kipindi chote watakachokuwa wakisubiri usafiri kituoni hapo.

“Tangu asubuhi nipo hapa nikikagua magari zikiwamo hizi daladala na sijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa abiria,” alisema Haji.

Albert Kitale ni miongoni mwa abiria waliokuwa wakisubiri mabasi kuelekea Same mkoani Kilimanjaro, alisema hali ya usafiri ni mbaya, kwani mabasi yote yamejaa hadi Desemba 27.

“Huu umati wa abiria unaonekana upo toka saa 11 alfariji mabasi ya kuunganisha hakuna na sidhani kama hizi daladala zilizopo zitatosha. Jana (juzi) nilisikia kulikuwa na utaratibu wa kupanga foleni ya kupanda katika daladala lakini leo suala hilo hakuna gari likishakaguliwa na kupewa kibali abiria tunagombania,” alisema Kitale
Powered by Blogger.