Mfuko wa Rais kutoa mikopo kwa wahitimu

Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) utatoa mikopo kwa wahitimu wa vyuo vinavyotambuliwa na Mamlaka

Rais Kikwete akipata somo kutoka kwa mwanafunzi

Dar es Salaam. Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) utatoa mikopo kwa wahitimu wa vyuo vinavyotambuliwa na Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Tanzania (Veta) kuanzia Januari mwakani.
Ofisa Uendeshaji na Masoko wa PTF, David Maluila alisema katika semina ya wanufaikaji wa mkopo huo wenye masharti nafuu kuwa wahitimu watatakiwa kuunda vikundi vya watu watano na kiingilio ni Sh5,000.
Alisema riba kwa kila mkopo ni asilimia mbili huku kiwango cha mwisho cha kukopa ni Sh500,000.
“Mikopo hii itawahusu wale tu wenye biashara, kama tukimpa urejeshaji wake ukiwa mzuri, basi tunampa zaidi ya hapo. Lakini tunaandaa mafunzo ya siku saba yatakayowawezesha kutambua umuhimu wa kuchukua mkopo,” alisema Maluila.
Alisema mikopo hiyo itatolewa nchi nzima isipokuwa itaanzia Kanda ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Makambako.
Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam, Ramadhan Dongwala alisema kutokana na mkopo huo kuwalenga wahitimu wenye biashara, utaratibu unaandaliwa ili wasiokuwa na biashara pia wanufaike.
Mshiriki wa semina hiyo, Juma Omary alisema: “Mikopo hii ni mizuri, itatuinua kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kama ulivyosikia riba itakuwa chini.
“Ni jambo jema, lakini utaratibu wa kila mmoja kunufaika uandaliwe usiishie tu kwa hawa wenye biashara.”
Frank Mwaisemba alisema: “Nimekuwa nikikopa benki, lakini huu ni mkopo wa gharama nafuu kuanzia riba na ada zake, ninawasihi wenzangu wajitokeze kuchukua mikopo hii.”
Powered by Blogger.