CCM kutumia panga la 2005
Vigezo 13 vilivyowekwa na CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 kumpima mwanachama anayefaa kugombea
Dar es Salaam. Vigezo 13 vilivyowekwa na CCM katika Uchaguzi
Mkuu wa 2005 kumpima mwanachama anayefaa kugombea urais, ndivyo
vitakavyotumika kuwaengua makada wanaoendelea kujitokeza kuwania nafasi
hiyo mwakani, imefahamika.
Vigezo hivyo vinaonekana
kuwa kizingiti kwa baadhi ya makada wa chama hicho ambao tayari
wametangaza na wengine wanaotajwa kutaka nafasi hiyo ya juu nchini,
ukiachilia mbali mnyukano unaotarajiwa kutoka vyama vya upinzani
vinavyoonekana kupata nguvu.
Makamu Mwenyekiti wa CCM
(Bara), Philip Mangula amelithibitishia gazeti hili kwamba, “Sifa hizo
13 zilizotumika mwaka 2005 na 2010 ndizo zitakazotumika pia mwaka 2015
na wala hakutakuwa na maboresho wala nyongeza ya aina yoyote.”
Vigezo
hivyo viliwekwa ili kuhakikisha chama hicho kinampata mgombea
asiyetiliwa shaka juu ya vitendo vya uadilifu, mwenye uzoefu wa uongozi
serikalini, atakayedumisha muungano, mwenye upeo wa masuala ya
kimataifa, mtetezi wa wanyonge, asiyejilimbikizia mali na mwajibikaji,
mambo ambayo hata hivyo, bado yameibua mjadala iwapo yanazingatiwa au
la.
Pia anayetakiwa lazima awe mwenye kuzitetea sera za
CCM, anayekubalika na wananchi, asiye na hulka ya udikteta au
ufashisti, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara na kiwango cha elimu
ya chuo kikuu au inayolingana nayo.
Licha ya vigezo
hivyo, baadhi ya makada waliokwishajitokeza na wengine wanaotajwa
wanaonekana dhahiri kukosa baadhi sifa hizo na wengine wako ‘kifungoni’
kwa miezi 12 baada ya kupewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na
kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na jamii.
Vigogo
wa CCM ambao wanatajwa kutaka kupewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya
chama hicho ambao iwapo watachukua fomu, watatazamwa kwa vigezo hivyo ni
Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambao
wamekwishatangaza kuwania nafasi hiyo.
Wengine ambao
wanatajwa ingawa hawajatangaza nia hadharani ni Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Bernard Membe; Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Uhusiano na Uratibu); Stephen Wasira na aliyewahi kuwa Waziri
wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wachambuzi wanavyosema
Akizungumzia
vigezo hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Danford Kitwana
alisema CCM inajua kuwa hakuna mgombea anayeweza kuwa na sifa zote 13,
kwa hiyo inapaswa iangalie ni nani anawazidi wengine.
“Kigezo
cha kuwa na sifa ya maadili ndicho kinachowakwamisha wengi, pia hakuna
mgombea anayeweza kuwa na sifa zote zilizowekwa na chama, mwingine
anaweza kuwa na sifa saba, nne au tano.
“Wakitumia mfumo wa kuwatazama wagombea wao kwa idadi ya sifa, mtu mwenye sifa nyingi ndiye asimamishwe kugombea.”
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema Tanzania
inahitaji kuongozwa na rais mwenye historia ya uadilifu wa matumizi ya
fedha za umma.
“Tunahitaji kiongozi anayeweza kusimamia fedha za umma,
si mtu anayenunua vitu ovyo bila kujali Hazina kuna kiasi gani, hilo ni
tatizo kubwa,” alisema Dk Mallya.
Aliongeza kuwa,
kiongozi huyo lazima awe mchapakazi anayeweza kuwaletea wananchi
maendeleo, lakini watu wengi wamekuwa wakisema wanamtaka mtu mwadilifu
bila kuzungumzia uwezo wake wa kufanya kazi.
Mwalimu
mstaafu wa shule ya msingi, Rehema Mathayo alisema kutokana na baadhi ya
viongozi ndani ya CCM kukumbwa na kashfa za ufisadi, anayetaka kugombea
urais lazima awe ‘msafi’ ndani na nje ya chama.
“Mshindi
ndani ya chama ni mtu atakayekuwa amewashinda wenzake kwa kuwa na
maadili mazuri na asiwe na doa lolote la kujishughulisha na ‘dili’ za
ajabu,” alisema Rehema.
Mwalimu huyo aliongeza kuwa
mgombea huyo lazima awe na uzoefu mkubwa wa masuala la kimataifa kwa
kuwa hata kama atakuwa na maadili, kama hafahamu namna ya kuwaunganisha
wananchi na jumuiya za kimataifa, hatakuwa na manufaa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Ernest Mwasalwiba alisema kutokana na
kuporomoka kwa maadili hususan kwa viongozi wa umma, vitendo vya rushwa
na kadhia mbalimbali, rais ajaye anatakiwa kuhakikisha yale anayoyasema
ndiyo anayatenda na Watanzania hawahitaji Rais dikteta.
“Masuala
ya maadili, rushwa, yote haya yanazuiwa mpaka sasa lakini suala ni
usimamizi tu... ni wakati sasa wa rais ajaye kuonyesha ajenda yake
itakuwa ipi, anapokuwa amesema kitu kila mtu lazima afuate mfano akisema
anachukia rushwa na maadili kwa yaheshimiwe isiwe ni mjadala kila mtu
anafuata kuanzia chini hadi juu.
“Dikteta siyo kiongozi
tunayemtaka, bali tunataka kiongozi atakayesimamia sheria na mifumo
iliyopo iweze kufanya kazi ipasavyo... mfano Rais Jakaya Kikwete kipindi
anaingia aliingia na kaulimbiu ya ‘Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya’
ambayo ilifuatwa hadi na viongozi wa halmashauri.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Romanus Dimoso alisema: “Sifa za rais huwa
zinajulikana. Tunahitaji rais ajaye anayejua hali ya kisiasa ilivyo kwa
sasa, hatutaki rais ambaye hatambui mchango unaotolewa na vyama vingi
vya siasa na jinsi atakavyoweza kufanya navyo kazi hususan kwa
kuhakikisha demokrasia inazingatiwa.”
Aliongeza: “Je,
malengo ya anayetaka urais yale ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 nchi
hii inafikia uchumi wa kati. Amejipanga vipi kama mtumishi wa kwanza wa
Taifa hili kutufikisha huko?... Hatutaki mtu awe rais tu kwa jina.”
Rais
mstaafu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia
alisema: “Tunahitaji rais anayeweza kufanya uamuzi mgumu kwa mustakabali
wa Taifa, asiwe rais wa maneno maneno, bali wa vitendo. Anasema dawa
hospitalini hakuna na kesho zinakuwapo.
“Tunataka mtu
mwenye historia ya uongozi, ameshawahi kufanya nini katika kuboresha
sekta ya afya, elimu, uchumi na kijamii? Alishafanya maamuzi magumu yapi
ambayo kila mmoja aliyaona na aliyaheshimu?”
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Goodluck Eliona na Ibrahim Yamola, Mwananchi