HATUA ZA KINIDHAMU: Dhoruba la Escrow lamkumba Maswi

>Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amemsimamisha kazi kwa muda, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amemsimamisha kazi kwa muda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma kuhusu ushiriki wake katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Badala yake, Sefue amemteua Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava kukaimu nafasi ya Maswi hadi uchunguzi husika utakapokamilika.
Maswi (pichani), anakuwa kiongozi wa tatu kukumbwa na dhoruba inayotokana na sakata la Escrow baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema na kung’olewa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka juzi.
Hatua ya Balozi Sefue inafanana na ile iliyowahi kuchukuliwa na mtangulizi wake, Philemon Luhanjo Julai 21, 2011 pale alipomsimamisha kazi kwa muda aliyekuwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo, David Jairo na kukaimisha nafasi yake kwa Maswi ili kupisha uchunguzi.
Baadaye Jairo alirejeshwa kazini lakini siku moja baadaye Rais Kikwete alimrejesha nyumbani kutokana na shinikizo la wabunge na tangu hapo hakuwahi kurudi katika utumishi wa umma na badala yake Maswi alithibitishwa kuwa katibu mkuu hadi jana.
Hatua ya kusimamishwa kwa Maswi imekuja siku moja tangu Rais Jakaya Kikwete alipoelekeza mamlaka za utumishi kuchukua hatua dhidi ya Maswi baada ya kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
“Kuhusu katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma, anatawaliwa na sheria na kanuni za utumishi wa umma, hivyo nimeshaelekeza mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa,” alisema Rais Kikwete wakati akilihutubia Taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam juzi.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana, ilisema Balozi Sefue amechukua hatua hiyo kwa kutumia madaraka aliyonayo kama mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa umma wanaoteuliwa na Rais, wakiwamo makatibu wakuu.
Amechukua hatua hiyo kwa mujibu wa Kifungu 4(3) (d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Namba 8 ya 2002 (kama ilivyorekebishwa).
Maswi na watumishi wengine wa umma ambao wametajwa watashughulikiwa na Tume ya Maadili, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) pamoja na Jeshi la Polisi na ikithibitika kuwa walikiuka maadili yao ya kazi, sheria stahiki zitachukuliwa.
Taratibu za uchunguzi
Kwa mujibu wa taratibu, Maswi analazimika kwenda likizo kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa awali ambao unalenga kubaini iwapo ametenda kosa la kinidhamu kwa mujibu wa sheria zinazoongoza utumishi wa umma. Kwa kawaida likizo yake ni ya malipo.
Ikiwa uchunguzi wa awali utabaini kwamba ana makosa ya kinidhamu, atapewa taarifa za tuhuma husika ambayo itaambatana na hati ya mashtaka, ambayo itaeleza kwa kifupi makosa hayo na jinsi yalivyotendekea.
Matokeo ya mchakato huo wa kinidhamu unaweza kuwa kushushwa cheo, kupunguzwa mshahara, kufukuzwa kazi, kuachishwa kazi au kurejeshwa kazini kutegemea matokeo ya taratibu zitakazofuatwa.
Kwa mujibu wa taratibu hizo, taarifa ya tuhuma itatoa maelezo kuhusu lini mtuhumiwa anapaswa awe amezijibu.
Baada ya kupelekewa atalazimika kujibu kwa kuzikubali au kuzikataa na ikiwa atazikubali mamlaka ya nidhamu inaweza kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Kama atakana au kukataa tuhuma husika, mamlaka ya nidhamu inapaswa kuunda kamati ya uchunguzi ambayo itapewa muda maalumu wa uchunguzi wa kuwasilisha tarifa yake kwa mamlaka ya nidhamu ikiwa ni mapedekezo na Katibu Mkuu Kiongozi anaweza kutoa adhabu kwa kuzingatia mapendekezo hayo.
Mamlaka ya nidhamu baada ya kupitia mapendekezo husika inawajibika kuendelea na mchakato wa kutoa adhabu kwa mujibu wa Sheria ya Umma na kanuni zake na iwapo adhabu ni kuvuliwa madaraka, mamlaka ya nidhamu italazimika kuwasiliana na mamlaka ya uteuzi ambaye ni Rais.
Ikiwa mtuhumiwa hataridhika na adhabu aliyopewa, taratibu zinampa fursa ya kukata rufaa kwa Rais.
Powered by Blogger.