Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad amesema atapambana katika vikao na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein iwapo baadhi ya wananchi wataendelea kunyimwa shahada za
wapigakura kwa kisingizio cha ukaazi.
Maalim Seif
alitoa msimamo huo jana alipohutubia mkutano wa hadhara wa CUF
uliohudhuriwa pia na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba katika
Uwanja wa Jarida, Wete Pemba.
Alisema kuna viongozi wa
Serikali za Mitaa (masheha) kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na mikoa
ambao wameanza kupanga mikakati ya kutaka kuwanyima shahada za
wapigakura baadhi ya wananchi kwa madhumuni ya kuibeba CCM katika
uchaguzi mkuu.
“Masheha eleweni nazungumza kama makamu
wa kwanza wa rais, suala la ukiritimba sasa basi na kama hamtaki sisi
tutapambana na Dk Shein katika vikao yeye, ndiye anayewateua,” alisema
Maalim Seif.
Kwa miaka mingi yamekuwapo malalamiko
kutoka CUF kwamba masheha wamekuwa wakiwanyima vitambulisho vya upigaji
kura baadhi ya Wazanzibari, wakisema si wakaazi wa Zanzibar.
Akishangiliwa
na wafuasi wa CUF, Maalim Seif alisema kama mipango itakwenda kama
ilivyopangwa, hakuna wa kuizuia CUF kuingia Ikulu, hivyo akawataka
wana-CUF kuendeleza umoja na mshikamano kabla ya uchaguzi huo.
Alisema
umoja ni nguvu na ndiyo maana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
umefanikiwa kuandika historia mpya katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
baada ya kupata matokeo ya kuridhisha.
Mwanasiasa huyo
alisema madhara ya kukataa umoja ndiyo yaliyoiathiri Zanzibar katika
Bunge la Katiba baada ya wajumbe wake kutetea masilahi ya chama badala
ya nchi.
Akihutubia mkutano huo, waziri wa zamani wa SMZ, Mansoor
Yusuph Himid alisema njia ya Maalim Seif kuingia Ikulu mwakani ni
nyeupe.
Alisema CUF kipo imara na kwamba jambo muhimu
ni wanachama na wafuasi wake kuendeleza umoja na mshikamano kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi huo.
“Njia ya kuingia Ikulu nyeupe, muhimu tukaze buti kufikia malengo ya kuleta mabadiliko ya kweli,” alisema Mansoor.
Profesa
Lipumba alisema suala la Katiba ndiyo limeimaliza CCM katika Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa kutokana na wananchi wengi kupinga kitendo cha
rasimu ya Jaji Warioba kubadilishwa na kuondoa vifungu muhimu
vilivyokuwa vikiwabana mafisadi na viongozi wasiokuwa waadilifu.
“Matokeo
ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yameonyesha dalili kuwa CCM ipo katika
hatari ya kufa na kukifuata chama cha Kanu cha Kenya,” alisema Lipumba.
Alisema
Serikali imeshindwa kusimamia utawala wa sheria na ndiyo maana
watuhumiwa wa wizi wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow
wameendelea kutamba bila ya kuchukuliwa hatua.
Alisema
Bunge lilipitisha maazimio la kutaka watuhumiwa hao wafukuzwe katika
nyadhifa zao na kuchukuliwa hatua za kisheria lakini hadi sasa hakuna
utekelezaji, wameendelea kubakia katika ofisi za umma licha ya
kukabiliwa na kashfa nzito.
Alisema kutokana na
kushindwa kusimamia utawala wa sheria, ndiyo maana hata watuhumiwa
katika kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) hawakuchukuliwa hatua za
kisheria na badala yake kutakiwa kurejesha fedha.
mwananchi
mwananchi